Burundi kulipokea kundi la kwanza la wakimbizi 2000 walioko Tanzania

Tanzania ndio nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi
Maelezo ya picha, Tanzania ndio nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi

Leo Jumanne Burundi imekujbali kuwa kundi la kwanza la wakimbizi wake walioko nchini Tanzania watarejea nyumbani Alhamisi, kama sehemu ya mpango wa serikali za nchi mbili, maafisa wa Burundi wamelieleza shirika la habari la Rheuters. Leo Oktoba mosi ndio tarehe iliotolewa na serikali ya Tanzania kuwarudisha wakimbizi 2000 wa Burundi nyumbani kutoka kwenye kambi za wakimbizi nchini humo.

Takriba wakimbizi 1,000 wako wako katika kundi la kwanza litakalorejea nyumbani , amesema meneja mkuu wa shughuli ya kuwarejesha wakimbizi nchini Burundi Nestor Bimenyimana. Amesema kuwa mchakato huo ni wa ''hiari''

Burundi na Tanzania zilikubaliana mwezi Agosti kwamba mchato wa kuwarudisha nyumbani wakimbizi zaidi ya 2000 wa Burundi waliopo nchini Tanzania utaanza Oktoba 1, jambo lililoibua hofu ya kulazimishwa kurudi nyumbani miongoni mwa wale waliovuka mpaka kuepuka ghasia.

Wakimbizi wamekuwa wakieleza hofu yao huku utaratibu huo ukitarajiwa kuanza.

"Tunahofia wakati wowote ... watatushtukizia na kutulazimisha turudi Burundi." anasema Jean Bizimana, mkimbizi katika kambi ya Nduta iliopo katika eneo la kaskazini magharibi la Kigoma.

Lugola alisema majadiliano hayo hayawahusu wakimbizi wenyewe moja kwa moja kwa sababu ''hawakuja Tanzania kwa hiari yao''.

''Tukisubiri urudi nchini kwako kwa hiari tutakuwa tunategemea hiari yako wewe binafsi lakini sisi tunaangalia sababu iliyokufanya utoroke nchi yako ilikuwa hoja ya amani na usalama'' alisema.

Katika kambi kuu ya Nyarugusu, tbaadi ya wakimbizi wameeleza kwamba matangazo yametolewa, kuwataka wajiwasilishe kwa hiari kusajiliwa kurudishwa nyumbani Burundi.

kambi ya Nyarugusu
Maelezo ya picha, Tangazo lililotolewa kwa wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu

"Wametuambia tutaamka siku moja na tutapata mabasi yanasubiri kutuchukuwa", mmoja ya wakimbizi ameiambia BBC.

Shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limeziomba Tanzania na Uganda kutowarudisha wakimbizi kwa lazima.

"UNHCR linaomba mataifa kuhakikisha kwamba hakuna mkimbizi anarudishwa Burundi kwa kushurutishwa na kwamba hatua zinachukuliwa kuifanya hali kuwa bora zaidi Burundi kuweza kuwapokea wakimbizi wanoarudi, ikiwemo kujenga imani na miradi kwa wanaoamua kurudi nyumbani."

Shirika hilo linaeleza licha ya kwamba usalama umeimarishwa Burundi tangu kuzuka ghasia kufuatia uchaguzi mkuu mnamo 2015 " hali hairuhusu kushinikiza wakimbizi warudi Burundi".

Kwa nini Tanzania inawakataa wakimbizi wa Burundi?

Waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Kangi Lugola ametangaza kuwa wakimbizi 2,000 watarudishwa Burundi kufikia October mosi.

''Azimio la msingi lilikuwa kila wiki lazima wakimbizi elfu mbili wawe wanarejeshwa nchini Burundi lakini tulipokutana na Mamlaka ya Burundi tuligundua kuwa UNHCR ndio wamekuwa wakikwepa jukumu hilo likisema Burundi haina uwezo wakuwapokea wakimbizi 2000 kwa wiki'' Waziri Lugola aliiambia BBC katika mahojiano ya kipekee.

Aliongeza kuwa serikali ya Burundi kupitia waziri wao wa mambo ya nje Pascal Barandagie waliwasilisha ombi lao kwa Tanzania kuelezea kutoridhishwa kwao na utekelezajiwa makubaliano waliofikia hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili na shirilka la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR.

Kangi Lugola
Maelezo ya picha, Waziri wa Mambio ya ndani wa Tanzania, Kangi Lugola

Bw. Lugola anadai kuwa shirika hilo la wakimbizi lina ajenda ya siri kwasababu linaleta kisingizio ambacho sio cha kweli.

Mbali na maelezo iliyopata kutoka wizara ya mambo ya nje ya Burundi kwamba nchi hiyo ni salama waziri Lugola anasema kuwa imeridhishwa kuwa wakimbizi hao watakuwa salama wakirudi makwao kwa sababu tangu mwaka 2015 hakuna hata mkimbizi mmoja aliyeingia nchini humo kutoka Burundi kwa kuhofia usalama.

Mvutano kati ya shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa mataifa na serikali ya Tanzania kuhusu suala la kuwaregesha makwao wakimbizi wa Burundi umekuwa ukiendelea kwa miaka kadhaa sasa.

Mwezi Agosti mwaka mwaka 2017, Serikali ya Tanzania ililipatia shirika la UNHCR siku saba kuanza kuwarudisha wakimbizi wa Burundi ambao wanataka kurudi kwao kwa hiari, ama sivyo serikali ifanye zoezi hilo yenyewe.

Tanzania ina zaidi ya wakimbizi 220,000 kutoka Burundi katika kambi za Nyarugusu, Nduta na Mtendeli mkoani Kigoma na ndio nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi kuliko nchi nyingine yoyote ile katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Wengi wao walitoroka mzozo nchini Burundi mnamo 2015.