Wakimbizi wa Burundi Tanzania wasema 'wametishiwa kurudishwa nyumbani‘

Chanzo cha picha, STEPHANIE AGLIETTI
Wakimbizi kutoka Burundi katika kambi moja nchini Tanzania wanasema kwamba maafisa wasimamizi katika eneo hilo wamewatishia kuwarudisha kwa lazima nyumbani.
Wakimbizi hao wameiambia BBC kwamba hawatokuwa salama iwapo watarudishwa Burundi.
Serikali ya Tanzania imekana kuwa kuna mpango wa kuwarudisha nyumbani wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu iliyo karibu na mpaka na Burundi.
Wakimbizi hao wameileza idhaa ya BBC ya maziwa makuu kwamba mkuu wa kambi hiyo, Jumanne Singani, aliwataka warudi kwa hiari kabla ys kushurutishwa kurudi nchini humo.
Bwana Singani anasikika kwenye kanda ya sauti iliyotumwa kwa BBC na baadhi ya wakimbizi, akiwaomba waondoke kwasababu wanachangia matatizo kwa wakaazi wa eneo hilo.
BBC imewasiliana na Singani kuomba ufafanuzi wa kauli hiyo, alikataa kutoa maoni na kutuelekeza kwa afisa katika wizara ya mambo ya ndani nchini.
"Tanzania haina mpango wa kuwalazimisha wakimbizi Warundi kurudi nyumbani," Christina Mwangosi, msemaji wa wizara hiyo ameiambia BBC.
Mchango wa Tanzania katika kuwahifadhi wakimbizi wa Burundi ni upi?
Zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Burundi wanaishia Tanzania, wengi wao wakiwa wametoroka ghasia nchini mwao zilizozuka mnamo 2015.
Mwaka jana Serikali ya Tanzania ilisema kuwa inajiondoa katika mpango wa Umoja wa mataifa wa kuwasaidia wakimbizi kuanza maisha mapya katika mataifa yanayowahifadhi.
Tanzania limekuwa eneo salama kwa wakimbizi wengi.
Mwaka 2017 taifa hilo lilisimamisha kwa muda usajili wa wakimbizi wapya na kuwataka wakimbizi wa Burundi kurudi nyumbani, hatua ambayo ilishtumiwa na makundi ya kupigania haki za kibinaadamu.

Chanzo cha picha, BBC Sport
Shirika la wakimbi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kuna wakimbizi Laki 2 kutoka Burundi wanaopatiwa makazi nchini Tanzania.
Katika idadi kubwa ya watu waliokimbia nchi yao, shirika hilo linaeleza kwamba asilimia 60 ni watoto.

Serikali ya Tanzania imesifiwa kwa kuendelea kubeba mzigo huu mkubwa wa wakimbizi lakini zaidi kwa kukubali kutekeleza mkakati wa kimataifa ujulikanao kama Comprehensive Refugee Response.
Ni mkakati uliolenga kutafuta namna endelevu ya kuwasaidia wakimbizi kupata ulinzi na mahitaji mengine ya msingi ya kibinadamu.
Lakini zaidi katika kutafuta namna ya kuwashirikisha wakimbizi hawa katika shughuli mbali mbali za maendeleo katika nchi wanazokimbilia.













