Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tanzania: Uvumbuzi wa teknolojia ya maji salama waokoa maisha
- Author, Eagan Salla
- Nafasi, BBC Swahili
Katika jitihada za kupambana na uchafuzi wa mazingira sambamba na upatikanaji wa maji safi na salama, nchini Tanzania kuna vijana wawili ambao wameanzisha teknolojia ya mashine za digitali ambazo zinasafisha maji kutoka kwenye vyanzo vya maji kwa haraka na kuyasambaza.
Mashine hizo ambazo zimewekwa kwenye maeneo mbalimbali jijini Mwanza nchini humo hasa penye mkusanyiko wa watu wengi zimelenga kutatua changamoto za kimazingira na kiafya.
Mashine hizo hazihitaji uwepo wa mhudumu muda wote bali wateja hutumia kadi maalumu kufanya manunuzi.
Mashine hii ina uwezo wa kukisafisha chombo kwa kutumia gesi maalumu kabla ya mteja kuchota maji.
Baada ya mteja kukinga maji ,yale yanayomwagika kuna chombo maalum kinachoyapokea kwa chini na hivyo kutumika kwa ajili ya kumwagilia bustani.
Shirika la Afya duniani (WHO) linaonesha asilimia 37 ya Watanzania wanategemea vyanzo vya maji visivyo salama.
Na Kutokana na miundombinu isiyo rafiki upatikanaji wa maji safi na salama bado ni kitendawili.
Lakini mashine hizi ambazo zimewachukua kipindi kirefu kuunda zimeleta matumaini kwa wakazi wengi jijini humo.
" sio kila mtu ana uwezo wa kununua maji dukani kwa sababu ya gharama, kiafya mtu anatakiwa kunywa zaidi ya lita mbili kwa siku ambapo kama unanunua dukani hiyo ni dola 1.5."
Licha ya huduma hii kupunguza gharama lakini pia inaendana na mkakati wa mazingira.
"Takwimu zinasema kuwa kati ya chupa 20 ni chupa mbili tu ndio zinaweza kufanyiwa uchakatikaji na kurudufishwa, na hizo chupa nyingine 18 zinaenda kuharibu mazingira," Victor Venance - Afisa Masoko wa mradi.
Vilevile wavumbuzi hawa wamelenga wateja kutumia vyombo ambavyo wanaweza kutumia zaidi ya mara moja na sio chupa za plastiki au mifuko ya lailoni.
Malengo ya milenia ya umoja wa Mataifa ni upatikanaji wa maji safi na salama nchini Tanzania maji safi na salama yakunywa dukani yanapatikana kwa nusu dola kwa lita lakini uvumbuzi wa huduma hii sasa lita tano ya maji safi na salama yatapatikana kwa bei hiyo hiyo ya nusu dola.
Mashine hizi zimesambazwa maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vyuoni, sokoni na hata barabara zinazotumiwa na wengi.
Kwa sasa huduma hii ambayo huwapa wakazi mkoani humu si maji baridi tu lakini hata moto, na mbali ya yote maji safi na salama yameshawafikia zaidi ya wakazi elfu kumi.
Hata hivyo ubunifu huu unaweza kuzidi kufanikiwa ikiwa mamlaka husika za maji zitahakikisha kuwepo upatikanaji wa maji ili huduma hii iwe endelevu.
Tafiti zinaonesha fedha nyingi zitumikazo sekta ya afya hutumika kutibu watu wenye magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama, hivyo huenda teknolojia hii mpya ya vijana hawa ikawa ndio nuru na matumaini ya kupambana na maradhi hayo.