Tanzania: Mahakama kuu yadumisha adhabu ya kifo

Kitanzi

Chanzo cha picha, Getty Images

Mahakama Kuu ya Tanzania imesema hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa hukumu ya kifo ni kinyume na katiba ya nchi.

Watetezi wa haki za binadamu walifungua kesi kutaka adhabu hiyo ifutwe kwani inakiuka haki ya msingi ya kuishi.

Hukumu hiyo haijatekelezwa tangu mwaka 1994.

Wafungwa 500 wanakabiliwa na adhabu ya kifo au kkifungo cha maisha.

Baada ya kuahirishwa kwa mara mbili mfululizo hatimaye majaji wa mahakama hiyo walitoa uamuzi wao kuhusu kesi hiyo ambayo iliwasilishwa na na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Tanzania wakitaka hukumu ya kifo ifutiliwe mbali.

jELA

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuna zaidi ya wafungwa 400 wanaosubiria kunyongwa Tanzania

Hukumu hiyo iliyosomwa na jaji Benhajj Masoud imeeleza kwamba hukumu ya kifo itaendelea kuwepo kwa sababu ipo kikatiba

''Hatujaridhika na maamuzi na tutainda mbele kwasababu ni suala ambalo kidogo limekosa uelewa mzuri kujibu tofauti ya kupinga adhabu ya kifo na na kupinga adhabu ya lazima yakifo'', wakili Fulgence Masawe aliimbia BBC.

Bw.Masawe ambaye alikuwa anakiwakilisha kituo cha sheria ameongeza kuwa adhabu ya lazima ya kifo inayotolewa katika kifungu cha 197 inasema ukishapatikana na hatia ya kosa la mauaji jaji, jaji au yeyote aliyekusikiliza hana adhabu nyingine na iliyobaki ni adhabu ya kifo tu.

Anasema katika nchi ambazo zimeendelea anaruhusa ya kuingilia kati kutafuta suluhisho kwa kufanya utetezi maanake mwisho wa siku yule ambaye amepatikana na hatia atapewa adhabu nyingine yoyote mbadala kulinganana na mazingira ya mauaji na kosa alililofanya kwasababu makosa yote hayafanani.

''Ukisoma hukumu nyingi za mahakama kuu tumeona majaji wanalalamika wanapomtia mtu hatiani kwenye kesi ya mauaji wanasema mkono wetu umefungwa, hatuna namna nyingine zaidi ya kutoa adhabu ya kifo'' alisema wakili huyo.

Aidha wakili Fulgence Masawe anapendekeza majaji wapewe uhuru kutoa hukumu kutokana na kesi iliyo mbele yao.

Hukumu ya kifo Afrika

Mambo yalivyo kufikia sasa suala hilo linaelekezwa katika mahakama ya rufaa.

Je mahakama hiyo itabatilisha uamuzi huo wa mahakama Kuu?

Mara ya mwisho kwa mfungwa kunyongwa ilikuwa mwaka 1994, enzi za utawala wa Rais wa awamu ya pili wa nchi hiyo, Ally Hassan Mwinyi.

Baada ya Mwinyi akaja rais Benjamin Mkapa ambaye akamwachia kijiti Jakaya Mrisho Kikwete na wote hao hawakusaini mfungwa yeyote kunyongwa.

Mwaka 2017, Magufuli akiwa anamuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamisi Juma alivunja ukimya juu ya suala hilo.

Hukumu ya kifo duniani

Harakati za kupinga hukumu ya kifo duniani zimepamba moto.

Kwa mujibu wa shirika la kmataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International mpaka kufikia 2017 nchi 142 zimeacha kutoa hukumu ya kifo kisheria na/au kiutekelezaji.

Umoja wa Mataifa (UN) unakadiria kuwa nchi 170 zimeachana na adhabu hiyo kwa nman moja au nyengine.

UN ina wanachama 193, hivyo ni mataifa 23 tu ndio ambayo inawezekana walitoa hata hukumu moja ya kifo katika muongo uliopita.

Kunyongwa

Mataifa ambayo yametekeleza hukumu ya kifo kati ya mwaka 2013 na 2017

Afghanistan, Bahrain, Bangladesh, Belarus, Botswana, Chad, China, Egypt, Equatorial Guinea, India, Indonesia, Iran, Iraq, Japan, Jordan, Kuwait, Malaysia, Nigeria, Korea Kaskazini, Oman, Pakistan, Palestina,

Saudi Arabia, Singapore, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Taiwan, Thailand, United Arab Emirates, Marekani, Vietnam na Yemen.

Nchi ambazo hazijatekeleza adhabu hiyo licha kuwepo kisheria kati ya 2013 na 2017

Tanzania si nchi pekee ambayo haitekelezi adhabu hiyo licha ya kuwepo kisheria.

Nchi nyengine zinazofanya hivyo ni pamoja na Antigua na Barbuda, Bahamas, Barbados, Belize, Comoros, Cuba, Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Dominica, Ethiopia, Gambia, Guyana, Jamaica, Lebanon, Lesotho, Qatar, Saint Kitts na Nevis, Saint Lucia, Saint Vincent na Grenadines, Trinidad na Tobago, Uganda na Zimbabwe.