Mbunge wa Kenya Charles Kanyi Jaguar azuru Tanzania

Chanzo cha picha, JAGUAR/FACEBOOK
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
Siku chache tu baada ya kutoa matamshi yaliozua utata nchini Tanzania, mbunge wa Starehe nchini Kenya Charles Kanyi Jaguar yupo nchini Tanzania .
Akizungumza na BBC kupitia njia ya simu, kiongozi huyo ambaye picha zake za mtandao wa Instagram zimemuonyesha akiwa mjini Dar es Salaam na Dodoma nchini Tanzania amesisitiza taarifa yake ya awali akisema kwamba aliyeleweka vibaya kuhusu matamshi aliyotoa kuhusu raia wa kigeni wanaoishi nchini Kenya.
''Mimi nilimaanisha wale wanaofanya biashara haramu nchini Kenya ndio wanaopaswa kufurushwa. Mimi hakuna mahali nilikosea na hakuna nchi inayoweza kuruhusu watu wasio na vibali kuingia na kufanya biashara haramu'', alisema mbunge huyo wa kaunti ya Nairobi

Chanzo cha picha, Instagram/jaguar
Kiongozi huyo ambaye pia ni msanii wa muziki wa kizazi kipya amesema kwamba yuko nchini Tanzania kwa siku nne kuijulia hali familia yake mbali na kuwatembelea marafiki zake.
''Mimi naipenda Tanzania kwa sababu ni nchi nzuri na kama unavyojua nina kijana huku. Nawaambia Watanzania kwamba nawapenda sana na ndio sababu nimetembea hapa pia kama mtalii ili kuipatia kipato nchi hii'', aliongezea kiongozi huyo.
Msanii huyo wa wimbo wa 'Kigeugeu' amesema kwamba anapanga kukutana na wabunge marafiki zake wa taifa hilo kama vile Profesa J na Sugu pamoja na wasanii tofauti.
Kiongozi huyo alizua utata nchini Tanzania aliponukuliwa katika kanda moja ya video iliosambaa katika mitandao ya kijamii akiwataka raia wa kigeni wanofanya biashara nchi humo kufurushwa.
"...Ukiangalia soko zetu, Watanzania na Waganda wamechukua biashara zetu, sasa sisi tumesema enough is enough".
Hatahivyo mbunge huyo alijitokeza tena na kukana madai hayo na kusisitiza kwamba alimaanisha raia wa kigeni walioingia nchini humo kwa njia haramu.

Chanzo cha picha, Instagram/ Jaguar
Matamshi hayo yalizua mjadala katika bunge la Tanzania huku waziri mkuu wa taifa hilo akimtaka balozi wa Kenya nchini Tanzania kutoa kauli ya serikali ya kenya
Hatahivyo Kenya ilijitenga na matamshi hayo ikisema yalikuwa ya kibinfasi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Na licha ya matamshi hayo yaliodaiwa kuwa ya chuki kuzua mjadala mwengine katika bunge la Kenya, huku baadhi ya wabunge wakimuunga mkono mwenzao, kiongozi huyo wa Starehe alikamatwa na kuzuiwa kwa siku kadhaa kabla ya kuwasilishwa mahakamani ambapo alishtakiwa kwa kufanya uchochezi.
Hatahivyo aliwachiliwa kwa dhamana baada ya mawakili wake kuwasilisha ombi hilo.
Lakini mjadala huo hakuishia hapo kwani rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alifunga safari kuelekea nchini Tanzania ambapo alikutana na mwenyeji wake Pombe Magufuli nyumbani kwake huko Chato.
Kati ya mambo yaliozungumzwa na kiongozi huyo ni kuwarai Wakenya na Watanzania kuishi kwa pamoja kama ndugu huku akisisitiza umuhimu wa kuona ili kujenga udugu zaidi.
Jaguar ni nani?

Chanzo cha picha, CHARLES KANYI/FACEBOOK
Charles Njagua Kanyi al maarufu Jaguar ni mwanamuziki, mwanasiasa na mjasiliamali na inaaminiwa kuwa mmoja wa wasanii tajiri nchini Kenya na katika eneo la Afrika Mashariki
Alizaliwa katika familia ya maskini katika familia ya watoto watatu. Jaguar alisomea katika shule ya msingi mjini Nairobi na akiwa na umri wa miaka 11 alifiwa na mama yake ambaye wakati huo alikuwa ndiye mlezi wake pekee.
Alilazimika kufanya kazi za vibarua ili kujikimu kimaisha na moja ya kazi alizozifanya ilikuwa ni kazi ya ukondakta wa mabasi ya abiria, maarufu daladala au matatu, na kwa msaada wa marafiki aliweza kumaliza shule.
Maisha ya kimuziki:
Rekodi Jaguar ya kwanza ilifanyika namo mwaka 2004 na baadae akajiunga na kampuni ya muziki ya Afrika mashariki Ogopa Deejays mnamo mwaka 2005 ambapo na miziki mmoja baada ya mwingine miongoni mwake "kigeugeu." Uliovuma sana na kupokea tuzo nyingi.
Katika kazi yake ya Muziki Jaguar ameweza kupata tuzo mbali mbali.
Tuzo za muziki:
Mwaka 2011-Tuzo ya muziki wa Afrika mashariki- Mwanamuziki bora wa kiume Afrika mashariki
Mwaka 2011- Tuzo yaNzumari- Mwanamuziki bora wa kiume Kenya
Mwaka 2012 -Tuzo ya Kisima-Wimbo bora Kenya
Mwaka 2012 - Tuzo ya Pearl (Uganda)-Mwanamuziki bora wa kiume
Mwaka 2012- Tuzo ya muzikila kilimanjaro (Tanzania)-Wimbo bora Afrika Mashariki- Kigeugeu
Mwaka 2012- Tuzo ya Nzumari-Mwanamuziki bora Afrika Mashariki
Mwaka 2012-Mshindi wa tuzo ya Channel O- Wimbo bora wa Afrika Mashariki
Mwaka 2013-Tuzo ya MCSK linalotolewa kwa msanii ambaye nyimbo zake zilichezwa zaidi katika vituo vya redio na kupendwa nchini Kenya.
Mwaka 2014-Tuzo ya muziki ya Kilimanjaroya Afrika mashariki-Wimbo bora- Kipepeo
Mwaka 2014- Tuzo ya AFRIMMA (Dallas Texas)-Aliteuliwa kama mwanamuziki bora wa kiume Afrika
Mnamo mwaka 2013 Jaguar alianza kurekodi katika Studio kuu Switch Studios iliyoanzishwa na mmoja wa wazalishaji wa muziki wake wa muda mrefu, Philip Makanda zamani akiwa katika Ogopa Deejays.
Miongoni mwa nyimbo nyingine zilizompatia umaarufu ni Kioo na One centimeter, na kufanya ushirikiano wa kimziki( Kolabo) na wasanii maarufu wa muziki badarani Afrika kama Iyanya kutoka Nigeria, na Mafikizolo kutoka Afrika Kusini katika singo "Going Nowhere"
Siasa
Tarehe 9 Agosti 2017 Jaguar alichaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Starehe mjini Nairobi kupitia tiketi ya chama tawala cha Jubilee baada ya kuwashinda washindani wenzake Steve Mbogo, Boniface Mwangi na Mwaniki Kwenya.
Jaguar ni kipenzi cha wengi nchini Kenya na ni mwanasiasa ambaye amekuwa na mvuto hasa kwa wafuasi wake ambao wengi wao ni vijana na wanawake.
Mvuto wake umekuwa ukishuhudiwa kila mara anapojitokeza kukutana na wafuasi na wananchi kwa mikutana katika jimbo lake la Starehe ambapo umati mkubwa hujitokeza kumsikiliza na kumshangilia.














