Watu 300 wagundulika na homa ya dengue Tanzania

Mbu
Maelezo ya picha, Homa ya dengue inaambukizwa na virusi vya mbu aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung'aa.

Serikali ya Tanzania imethibitisha uwepo wa ugonjwa wa homa ya dengue nchini humo ambapo watu 307 wamegundulika na virusi vya homa hiyo.

Ugonjwa huo kwa sasa umeripotiwa kwenye mikoa miwili ya Dar es Salaam na Tanga. Watu 252 wamegundulika na virusi hivyo mkoani Dar es Salaam na wengine 52 Tanga.

Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania Faustine Ndugulile Alhamisi amewaambia waandishi wa habari kuwa kutoka Januari hadi Aprili 2 watu 470 waliopimwa ugonjwa huo, 307 waligundulika kuwa na virusi hivyo au walishapata matibabu.

Ndugulile ametahadharisha kuwa si kila homa ni malaria na wananchi wanaaswa kwenda hospitali mara moja wanapokuwa na homa.

"Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana na zinaweza kufanana sana na dalili za malaria, hivyo wananchi wanaaswa kuwa makini wapatapo homa na wawatake watoa huduma kuwapima ugonjwa huo (dengue) vipimo vinapoonesha kuwa hawana malaria."

Homa ya dengue inaambukizwa na virusi vya mbu aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung'aa. Dalili za ugonjwa huo huanza kujitokeza siku tatu mpaka 14 toka mtu alipoambukizwa.

Maelezo ya sauti, Wanasayansi Kenya wamegundua dawa inayoangamiza mbu anayesababisha Malaria.

Madaktari wanatahadharisha dawa zote zenye diclofenac kuwa si salama kwa afya ya mgonjwa wa dengue. Baadhi ya dawa hizo ambazo hupatikana kwa wingi Tanzania kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa nchi hiyo Profesa Mohammed Kambi ni Ibuprofen, Brufen na Diclopar.

Mara ya mwisho kwa ugonjwa huo kuripotiwa kuibuka nchini Tanzaia ilikuwa mwaka 2014 ambapo watu kadhaa walipoteza maisha.

Dalili za homa ya dengue

  • Homa ya ghafla
  • Kuumwa kichwa
  • Uchovu
  • Maumivu ya maungo na misuli
  • Kichefu chefu na kutapika
  • Maumivu ya macho
  • Muwasho na vipele vidogo vidogo

Namna ya kujikinga

  • Kuangamiza mazalia ya mbu
  • Kulala kwenye chandarua chenye dawa
  • Kuvaa nguo ndefu