Mahakama ya Marekani yaamuru kwamba mfungwa huyu 'ni sharti ahisi maumivu katika kifo chake '

Russell Bucklew

Chanzo cha picha, Missouri Department of Corrections

Maelezo ya picha, Russell Bucklew asema sindano ya sumu itamsababishia maumivu mengi

Mahakama ya kilele nchini Marekani imeamuru kwamba mfungwa mmoja aliyepatikana na hatia ya mauaji katika jimbo la Missouri hana haki ya kifo kisichokuwa na mateso.

Uamuzi huo unatoa fursa ya kunyongwa kwa Russell Bucklew, ambaye aliomba kunyongwa kwa kutumia gesi badala ya kudungwa sindano ya sumu kutokana ugonjwa usiokuwa wa kawaida.

Bucklew , 50 alihoji kwamba mbinu ya kumuua inayotolewa na jimbo hilo ilipigwa marufuku.

Bucklew alihukumiwa kifo 1996 kwa ubakaji, mauaji na utekaji katika shambulio dhidi ya mpenziwe wa zamani na mpenzi wake mpya pamoja na mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka sita.

Katika ombi lake Bucklew alihoji kwamba hali yake ya kiafya kwa jina cavernous hemangioma-ugonjwa wa kufura kwa mishipa ya damu unaweza kusababisha maumivu iwapo atanyongwa kupitia sindano ya sumu..

Majaji wa mahakam ya kilele

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Majaji wa mahakam ya kilele

Hali hiyo inafanya mishipa ya damu kuwa na uvimbe katika koo, shingo na sura, hali ambayo inaweza kupasuka kwa mishipa hiyo ya damu na kumsababishia maumivu na ukosefu wa hewa.

Kulingana na Bucklew atahisi maumivu mengi iwapo afisa anasimamia tendo la kunyonga watu atatumia mbinu ya serikali ya kumdunga sindano ya sumu.

Lakini majaji wa mahakama hiyo walisema siku ya Jumatatu kuwa jitihada za kisheria zinachukulia mbinu hiyo kuwa ya haki.

Wamesema kuwa ni kwa mfungwa huyo kuthibitisha kwamba mbinu nyengine ya kumnyonga inaweza kupunguza maumivu hayo, lakini hajafanya hivyo.

''Sheria ya nane ya katiba ya Marekani inakataza ukatili ama mbinu isio ya kawaida katika kumtesa mtu wakati wa kumnyonga'' , aliandika jaji Gorsuch ambaye aliteuliwa na jaji Donald Trump .

Aliongezea: kama inavyoeleweka , sheria hiyo ya nane iliruhusu mbinu za kunyonga , kama vile kupitia kitanzi ambacho kina mateso na maumivu, huku ikikataza mateso wakati wa shughuli hiyo.

Katika kisa kimoja jimboni Alabama , mwanamume mmoja wa Kiislamu alikatazwa kuwa na imam wakati alipokuwa akinyongwa , lakini mahakama ikasitisha hukumu kama hiyo baada ya rufaa kukatwa na muumini wa Budha ambaye alitaka mshauri wake wa kidini kuwepo wakati alipokuwa akinyongwa.