Polyana Viana: Bondia mwanamke amdunda na kumdhibiti mwizi mwanaume

Polyana Viana fighting JJ Aldrich in August 2018

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Polyana Viana (kulia) ameshinda mapambano 10 kati ya 12 aliyopambana

Tahadhari: Kuna picha ya kutisha chini

Mwanaume mmoja amejikuta katika wakati mgumu baada ya kujaribu kumuibia mwanamke mmoja nchini Brazil.

Hata hivyo, mwanamke huyo hakuwa wa kawaida bali bondia wa kimataifa wa mchezo wa mapigo mchanganyiko.

Bi Polyana Viana mwenye miaka 26 alikuwa ameketi nje ya nyumba moja jijini Rio de Janeiro siku ya Jumamosi kabla ya kijana mmoja kumkabili na kujaribu kukwapua simu yake.

Alipoona hali imebadilika na hatari inamnyemelea, bondia huyo alitumia ujuzi wake wa ulingoni kujinasua.

Mwanamke huyo alimvurumishia mvua ya makonde na mateke mwizi huyo na kumuangusha na kumdhibiti vilivyo kabla ya askari kuja kumuokoa.

"Aliniambia: 'Nipe simu yako. Usifanye kitu chochote sababu nina silaha'," Viana aliliambia jarida la MMA Junkie.

"Kisha akauweka mkono wake kwenye bunduki, lakini nikagundua kuwa ni laini sana.

"Nilipoona hivyo nikasimama. Nikamtandika ngumi mbili na teke. Akadondoka chini. Nikampiga kabali ya nguvu. Kisha nikamkalia kwa juu na kumdhibiti, nikamwambia, 'Sasa inabidi tusubiri polisi waje'."

Viana, ana rekodi ya kushinda mapambano 10 na kupigwa mara mbili. Pambano lake la mwisho lilikuwa Agosti mwaka jana ambapo alipigwa na JJ Aldrich.

Split picture of Polyana Viana and the thief

Chanzo cha picha, Getty Images/Dana White Instagram

Maelezo ya picha, Njemba iliyojaribu kuiba ilikiona cha moto baada ya uso wake kuchakazwa.