Rahaf al-Qunun: Mwanamke wa Saudia aliyeukana Uislamu apewa hadhi ya ukimbizi

Rahaf Mohammed al-Qunun talks to Thai Immigration Police Chief Surachet Hakparn at the Suvarnabhumi international airport near Bangkok

Chanzo cha picha, EPA/THAI IMMIGRATION BUREAU

Maelezo ya picha, Rahaf Mohammed al-Qunun, akiwa uwanja wa ndege wa Bangkok anasema "nataka kuwa huru" mbali na Saudi Arabia
Muda wa kusoma: Dakika 3

Mwanamke raia wa Saudi Arabia aliyeikimbia familia yake na kisha kujifungia hotelini jijini Bangkok amepewa hadhi ya ukimbizi na Umoja wa Mataifa.

Rahaf Mohammed al-Qunun, 18, aligoma kupanda ndege kutoka Bangkok kwenda Kuwait ambapo familia yake ilikuwa inamsubiria siku ya Jumatatu wiki hii. Alijifungia kwenye chumba cha hoteli kwenye uwanja wa ndege.

Bi Rahaf amesema ana hofu kuwa familia yake itamuua baada ya kuukana Uislamu.

Serikali ya Australia imesema Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wakimbizi (UNHCR) limewapa taarifa rasmi ili ikiwezekana wampe hifadhi.

Awali maafisa uhamiaji wa Thailand walitaka kumrejesha mwanamke huyo nchini Kuwait. Bi Rahaf akalazimika kuanzisha kampeni kwa kutumia mitandao ya kijamii ambayo iliibua hisia kimataifa.

Katika taarifa fupi, idara ya Mambo ya Ndani ya Australia imesema "itaishughulika kesi hiyo kwa njia ya kawaida".

"Serikali (ya Australia) haitalizungumzia tena suala hili kwa sasa," taarifa hiyo imesema.

Hadhi ya ukimbizi kwa kawaida hutolewa na serikali za nchi, kwa mujibu wa tovuti ya UNHCR shirika hilo linaweza kutoa hadhi hiyo pale serikali hizo "zitakaposhindwa ama kugoma kufanya hivyo. UNHCR imesema haiwezi kuzungumzia kesi za mtu mmoja mmoja."

Baada ya bi Rahaf kupata hadhi hiyo, nchi nyengine inapaswa kukubali kumpatia hifadhi.

Screen grab from a video released to AFPTV via the Twitter account of Rahaf Mohammed al-Qunun

Chanzo cha picha, AFP

Maafisa nchini Australia tayari wamedokeza kuwa ombi lake la hifadhi litakubaliwa.

"Kama atabainika kuwa kweli ni mkimbizi, basi tutalipa uzito stahiki suala lake na kumpatia viza ya kibinaadamu," Waziri wa Afya Greg Hunt amekiambia kituo cha runinga cha ABC kabla ya maamuzi ya UNHCR kuwekwa wazi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Astralia Marise Payne anatarajiwa kuwasili Thailand kesho Alhamisi, hata hivyo ziara hiyo ilipangwa kabla ya mkasa huo.

Kwa nini ameomba hifadhi ?

Kuukana Uislamu ni kosa linaloadhibiwa kwa kifo nchini Saudi Arabia. Baba wa Rahaf ni gavana wa al-Sulaimi, mji uliopo kwenye jimbo la Hail.

"Maisha yangu yapo hatarini," ameliambia shirika la habari la Reuters. "Familia yangu inatishia kuniua kwa mabo madogo tu."

Msemaji wa familia yake ameiambia BBC kuwa hawataki kulizungumzia suala hilo na kwa sasa wanajali usalama wa ndugu yao.

Baba na kaka wa bi Rahaf tayari wameshawasili nchini Thailand lakini amegoma kukutana nao.

Makundi ya wanaharakati za haki za binaadamu kama Human Rights Watch (HRW) wameeleza wasiwasi wao mkubwa kwa usalama wa mwanamke huyo.

Phil Robertson, Naibu Mkurugenzi wa HRW kwa bara la Asia ameiambia Reuters: "Amesema wazi kabisa kuwa amekumbana na manyanyaso ya kimwili na kiakili. Amesema amefikia uamuzi wa kuukana Uisilamu. Na nilijua mara baada ya kusema hivyo basi yupo kwenye hatari kubwa."

Jumatatu asubuhi alituma tena ujumbe wa twita akiomba hifadhi katika nchi za Uingereza,, Canada, Marekani na Australia.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Presentational white space

Mkasa mzima umetokeaje?

Bi Rahaf anasema alikuwa safarini na familia yake nchini Kuwait alipoamua kutoroka Januari 4.

Alikuwa njiani akielekea Australia, lakini ilimpasa kubadili ndege jijini Bangkok.

Kwa sababu hakuwa na viza ya kuingia Thailand, polisi walimnyima ruhusa ya kuingia nchini humo na wakaanza utaratibu wa kumrejesha kupitia ndege ya Kuwait Airways aliyotua nayo.

Mwanadiplomasia wa Saudia anadaiwa kumpora pasipoti yake alipowasili Thailand. Hata hivyo, ubalozi wa nchi hiyo jijini Bangkok umekanusha kuhusika kwa namna yoyote kwenye mkasa huo. Bi Rahaf amesema amerejeshewa pasi hiyo jana Jumanne.

Bangkok airport

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Awali polisi katika uwanjwa wa ndege wa Bankok walimnyima Bi Rahaf ruhusa ya kuingia nchini humo na wakaanza utaratibu wa kumrejesha kupitia ndege ya Kuwait Airways aliyotua nayo.

Alianza kurusha mbashara mkasa wake wote na pia kuwapa rafiki zake nywila (password) yake ya mtandao wa Twitter ili wamsaidie kupaza sauti.

Wanaharakati wakawaunga mkono, japo baadhi ya watumiaji wa mtandao nchini mwake walilaani matendo yake.

Picha ya video ilipakiwa mtandaoni ikionesha ni kwa namna gani alipambana kuzuia kurejeshwa kwa familia yake. Alijifungia ndani ya chumba cha hoteli na kuweka meza mlangoni ili kuzuia watu kuingia.

Ameiambia BBC kuwa "Nimeweka tukio angu katika mitandao ya kijamii na baba yangu ameghadhibika kweli sababu nimefanya hivyo... Siwezi kusoma na kufanya kazi nchini mwangu, hivyo nataka kuwa huru, kusoma na kufanya kazi vile nitakavyo."

Bi Rahaf kwa sasa amewekwa kwenye nyumba ambayo inalindwa na maafisa wa Thailand toka Jumatatu usiku pale aliporuhusiwa kutoka uwanja wa ndege na ameshahojiwa na maafisa wa Umoja wa Mataifa juu ya madai kuwa maisha yake yatakuwa hatarini kama atarejeshwa kwenye mikono ya familia yake.

Kisa hiki kinafanana na kingine kilichotokea mwezi Aprili mwaka 2017 ambapo mwanamke mwingine raia wa Saudi Arabia alizuiliwa katika uwanja wa ndege alipokuwa safarini kuelekea nchini Australia.

Dina Ali Lasloom, 24, alikuwa akitoka Kuwait kupitia nchini Ufilipino lakini alikamatwa na familia yake katika uwanja wa ndege wa Manila na kurudishwa Saudia.

Alitumia simu ya mtalii mmoja wa Canada kutuma ujumbe wa video kwenye mtando wa Twitter, akisema familia yake itamuua.

Hatima yake baada ya kuwasili nchini Saudi Arabia haijulikani mpaka sasa.