Mapromoko ya ardhi Uganda: Kuna hofu huenda idadi ya waliyofariki ikaongezeka

Watu waangalia uharibifu uliosababishwa na maporomoko ya ardhi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu waangalia uharibifu uliosababishwa na maporomoko ya ardhi

Zaidi watu 50 wamepoteza maisha kutokana na maporoko ya ardhi na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha mashariki mwa Uganda.

Mamia ya watu bado hawajulikani walipo huku maafisa katika wilaya ya Bududa wakihofu kuwa idadi ya waliopoteza maisha huenda ikaongezeka.

Walioshuhudia mkasa huo wanasema kuwa mwamba ulidondoka mtoni na kupasua kingo za mto hali iliyosababisha maji yaliyochanganyikana na matope kuanza kusomba watu vijijini.

Mwanamke anaomboleza

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Mwanamke anaomboleza

Serikali imesema vikosi vya uokoaji vimepelekwa katika eneo hilo karibu na mpaka wa Uganda na Kenya lakini miundo mbinu ya barabara na daraja iliyoharibiwa imelemaza shughuli za uokozi.

Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha watu wakitoa miili kutoka ndani ya tope na kuweka kando

Maporomoko mengine ya odongo yalishuhudiwa katika eneo hilo la Bududa yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 300 mwaka 2010.

Bududa inasifika kwa ardhi yenye rutuba ambayo huvutia watu licha ya hatari inayowakabili

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Watu wanaangalia nyumba zilizoharibiwa

Mwanahabari wa kujitegemea Shwahib Ibrahim, ameiambia BBC kuwa baadhi ya wakaazi mpaka sasa hawajui wapendwa wao wako wapi.

Ibrahim pia amesema shirika la msalaba mwekundu limekuwa likiwasaidia waathiriwa wa mkasa huo tangu jana.

Kwa upande wake msemaji wa shirika la Msalaba mwekundu Irene Nakasiita amesema "Maji yalipoanza kuteremka chini ilibeba mawe makubwa ambayo iliharibu nyumba za watu,"

Ramani ya eneo la mlima Elgon

Kufuatia mikasa iliyopita, watu waliiamriwa kuhama eneo hilo lakini wengi wao walirejea kwa kuvutiwa na ardhi yenye rutuba na upendo wa makaazi yao ya asili.