Belinda Nyapili: Fahamu namna ya kumsaidia mtu mwenye Sonona na matatizo ya akili

Chanzo cha picha, Belinda
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC Swahili
Sonona ni hali ambayo akili yako inaweza kuuambia mwili wako kuwa umechoka na kufanya mtu kuchanganyikiwa na kuona kuwa hakuna umuhimu wowote wa kubaki duniani.
Mtu anaweza kupata ugonjwa wa sonona au kusononeka baada ya kukosa kazi, kutengana na mwenza wake, kufiwa au kukatishwa tamaa pia huweza kumfanya mtu ajihisi kuwa dunia imesimama na kuona kuwa hakuna kitu chochote kina umuhimu duniani.
Belinda Nyapili ni miongoni mwa watu waliowahi kupita ugonjwa huo wa akili unaojulikana kama sonona, ambao wengine huwa wanauchukulia ugonjwa huo kama ni msongo wa mawazo tu na sio ugonjwa.

Chanzo cha picha, Belinda Nyapili
Belinda alianza kupata tatizo hili la sonona wiki mbili baada ya kumzika mtoto wake wa kwanza ambaye aliugua kwa muda mfupi na kufariki.
Anasema hali ya ugonjwa wake ulianza kwa kujihisi kutotaka kujichanganya na watu, kutoongea, kutokula na kukosa furaha na kikubwa alichokuwa anakifanya ni kunywa pombe.
"Nilifikia ile hali ya kutaka kujiua kabisa, nilikuwa nasikia sauti na nguvu ya kutaka kujiua .Katika kichwa changu nilikuwa nasikia kelele sana na ilinipelekea mpaka kunywa vidonge 60 ili tu nife.Ni kitu ambacho bado kinanishangaza ilikuwaje nilipona maana nilikunywa pombe nyingi pamoja na dawa," Belinda alieleza.
Aidha suala la kujiua ni suala ambalo mwanzoni Belinda anadai alikuwa analiona kuwa watu ambao wanafanya hivyo huwa wana ubinafsi.Hivyo hali hiyo ilimshangaza sana kuwa hata yeye alitaka kujiua wakati akiwa bado ana mtoto mwingine ambaye anamtegemea.

Chanzo cha picha, Belinda Nyapili
"Niliwahi kulazwa katika hospitali ya taifa katika wodi ya wagonjwa wa akili.
Nadhani kupata matibabu kwa kusikiliza ushauri nasaha kutoka kwa madaktari kumeweza kunifanya nipone ingawa hali hiyo huwa inajirudia tu bila kutegemea.
Nafahamu kuwa kuna ueleo mdogo sana katika jamii,wengi wanaokutana na hali kama yangu huwa wanajaribu kutafutiwa tiba katika upande wa kiimani na wengine huwa hata wanakuwa na Imani potofu.
Kuna dada mmoja mbaye nilikuwa naye wakati napata tiba lakini yeye alifanikiwa kujiua kwa sababu alikuwa hana mtu wa karibu wa kumfuatilia kunywa dawa na kupata tiba.
Na mapito yote hayo ambayo nimeyashuhudia katika maisha yangu yameisumkuma kuanzisha asasi ya kuwasaidia wagonjwa wa sonona".

Chanzo cha picha, Belinda Nyapili
Marcus Mwemezi Foundation ni asasi ambayo Belinda aliipa jina la mtoto wake kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya ya akili na kuwakutanisha wagonjwa wa akili na wataalamu wa afya.
"Sonona huwezi kuiona mpaka hatua ya mwisho kabisa ndio unaweza kugundua tatizo.
Ilifikia mpaka hatua ambayo nilikuwa nafungwa minyororo
Thamani ya utu huwa inapotea kutoka kwa jamii na hata jamii haina muda wa kumpa huduma bila kumpa majina".
Belinda aliongeza kusema kuwa kuna changamoto nyingi sana binadamu huwa tunapitia lakini hakuna maumivu makali ambayo mtu anaweza kuyapata kama pale anapopoteza mtoto wake.
Utu ni jambo muhimu ambalo kama litaendelea kuwepo basi litasaidia hata watu ambao wana matatizo ambayo hayaonekani,Belinda alisisitiza.
Watu wenye hatari ya kupata magonjwa ya akili wanaweza kuyaepuka iwapo watapata watu wa kuwasikiliza kwa upendo, kwa kujali na kutoa ushauri pale inapobidi, hata pasipo ushauri ni msaada mkubwa.
Jamii ya watanzania bado inawanyanyapa wagonjwa wa afya ya akili kwa sababu ya kukosa elimu au uelewa kuhusu hali hiyo,watu wengi huwa wanatoa majina kwa wagonjwa wa sonona kwa kuwaita vichaa,chizi,mwendawazimu na majina mengine mengi badala ya kupata matibabu.
Sonona ni nini?
Kila mtu huwa anapata hii hali ya sonona anapokuwa hana furaha,ingawa hali hii huwa inachukua muda mfupi.Ukiwa na sonona akili huwa inavuruga mipango ya shughuli za kila siku na hivyo kusabisha maumivu kwa muhusika na watu wanaomzunguka.
Watu wengi huwa wanapata ugonjwa huu wa sonona lakini huwa hawahutafutii tiba.
Daktari Christopher Peterson kutoka Sanitas hospital,Dar es salaam anasema huwa kuna aina nyingi za sonona lakini katika ukanda wetu wa Afrika sonona inayowapata watu wengi huwa ni ile ambayo inayomfanya mtu kushindwa kufanya kazi,kulala,kula na kufurahia maisha.
Hii huwa inapotokea mara moja huwa inajirudia mara kadhaa.
Sonona nyingine ni ile ambayo huwa inawapata wanawake wanapotoka kujifungua na inakadiriwa kuwa asilimia 10 mpaka 15 ya wanawake huwa inawapata wanawake wanaotoka kujifungua.
Viashiria vya sonona:
•Unajihisi unyonge
•Unajihisi kukata tamaa
•Unajihisi umekosea na huna thamani
•Kuchoka
•Kukosa hamu ya kufanya shughuli yeyote ikiwa pamoja na kufanya mapenzi
•Kukosa nguvu
•Kushindwa kuwa na kumbukumbu na kufanya maamuzi
• kukosa usingizi,kukaa macho usiku kwa muda mrefu
•Kukosa hamu ya kula
•kuwaza kujiua
•kuumwa kichwa
Aidha Daktari Christopher Peterson anasema mtu mwenye Sonoma ana utofauti mkubwa na mtu mwenye kichaa. Sonoma haiwezi kusababishwa na vitu kama madawa ya kulevya
Kuna utofauti mkubwa kati ya kichaa na mtu mwenye sonona.
Mtu mwenye kichaa hawezi kujaribu kujiua huwa anafurahia maisha yake kwa hali ileile aliyokuwa nayo ambayo kila mtu anaona sio maisha wakati sonona mtu anakuwa hana hamu na maisha na anakosa kuiona thamani yake,anapoteza matumaini ya kimaisha kabisa.
Sonona anaweza kupona kwa ushauri nasaha au wa kiimani wakati mgonjwa wa akili ambaye ni kichaa hawezi kupona kwa njia hiyo.












