Mjadala kuhusu viwanda vya sekta ya afya wapamba moto Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC Swahili
Ajenda ya kukuza uchumi wa viwanda nchini Tanzania inazidi kushika kasi na hivi sasa wataalamu katika sekta afya nchini humo wameanza kutilia mkazo uanzishwaji wa viwanda vya kuzalisha dawa ili kuendana na mipango ya nchi katika kujenga uchumi wa watu wa kipato cha kati.
Takribani asilimia themanini ya dawa zinazotumika nchini Tanzania zinazalishwa nje ya nchi na kusalia asilimia ishirini peke yake ambayo hutengenezwa nchini humo.
Kiwango hicho kidogo cha uzalishaji kinatokana na viwanda vya dawa kuwa vichache katika nchi hiyo huku kiwanda kimoja tu kikiwa kimeidhinishwa kwa kiwango cha kimataifa.
Hali hii imewasukuma wataalamu wa afya kuanzisha jitihada maalum za uanzishwaji wa viwanda vipya vya dawa. Lakini, bado swala hilo linahitaji mjadala mpana.
Dkt Omary Chillo, Rais wa Kongamano la kila mwaka la Afya nchini Tanzania (Tanzania Health Summit), amesema ukuaji wa viwanda katika sekta ya afya unaweza kuisaidia sekta ya afya kuacha utegemezi kwa kiwango kikubwa.
Dkt Chillo, ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(Muhas) ni miongoni wa wataalamu watakao jumuika jijini Dar es Salaam, November 13 ili kujadili namna bora ya kuanzishwa kwa viwanda hivyo na jinsi ya kukuza sekta ya afya katika uchumi wa viwanda kwa ujumla.
Mpaka sasa, viwanda vya dawa nchini Tanzania havizidi sita. Hii ni kwa mujibu wa ripoti mbalimbali nchini humo. Na vinne kati ya hivyo, ndio vyenye uwezo wa kutengeneza dawa za binadamu ambazo ni za maumivu, kikohozi na malaria.
"Inasikitisha kuwa 80% ya dawa Tanzania tunanunua nje hata maji yale yanayohitajika hospitalini ambayo ni rahisi kutengeneza tunanunua pia,"Dkt Chillo aliiambia BBC.
Viwanda vingi vya dawa vilivyopo Tanzania ni vya muda mrefu; vingine ni vya tangu miaka ya 1980. Kunahitajika juhudi za makusudi kuanzisha viwanda vipya ili kukidhi mahitaji ya sasa, alishauri Dkt Chillo.
Ripoti ya makadirio ya watu nchini Tanzania inaonyesha kuwa kwa upande wa bara nchi hiyo ina watu 52.6 milioni na Zanzibar watu 1.6milioni. Hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya sita barani Afrika kwa ongezeko kubwa la watu ikitanguliwa na Nigeria, Ethiopia, DRC na Misri.
Ongezeko la watu limekuwa kwa kasi na lakini si katika miundombinu hususani katika sekta ya afya, anabainisha Dkt.Chillo.
Lakini anakiri kwamba, uanzishwaji wa viwanda vya dawa na vingine vya afya kwa ujumla si rahisi. Inabidi vianze hatua kwa hatua kwa kuunganisha nguvu baina ya sekta binafsi na serikali katika kuongeza uwekezaji wa rasiliamali watu, yaani watendaji,kufanya utafiti na kujenga viwanda.
Aidha viwanda vya afya vinatajwa kuwa tofauti na viwanda vingine kutokana na utaalamu unaohitajika pamoja na teknolojia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Taarifa kutoka Tanzania zinaonyesha kwamba nchi hiyo inalenga kuanzisha kiwanda cha kutengeneza maji ya hospitalini kwasababu maji ni rahisi kupatikana na formula zake na vilevile kutengeneza bidhaa za nyingine za hospitalini zinazotokana na pamba. Kilimo cha pamba hufanyika nchini humo.
"Tuna wanafunzi ambao wana ujuzi wa nadharia lakini sio vitendo, hivyo ni muhimu kwa serikali kuwajengea uwezo ili baada ya miaka kumi labda ndio tunaweza kusema tuna wataalamu wa kutengeneza dawa,"Dkt Chillo alisisitiza.
Kutenga eneo kuratibu shughuli za viwanda
Tanzania imeweza kupata eneo moja(One-stop centre) ambayo inaweza kusaidia katika kuratibu shughuli zote za uwekezaji wa viwanda, ambapo inaweza kuwezesha,kurahisisha na kuhakikisha sera ya viwanda inafanikiwa katika mikakati hii.
Dkt.Chakou Halfani, daktari bingwa wa saratani na mwenyekiti wa Kongamano la afya Tanzania, anasema kongamano ambalo lilifanyika hivi karibuni likiwajumuisha wadau wa afya na mamlaka husika liliangalia maendeleo ya viwanda na kutoka na makubaliano kuwa kati ya mwaka 2020 mpaka 2025,Tanzania tayari iwe imeanza kuwa na viwanda vya dawa.

Dkt.Chakou alieleza pia kuwa sasa ni wakati muafaka kwa Tanzania kuweka mkazo kwa dawa zote za sayansi na za miti shamba.
Tanzania tayari ina muamko katika viwanda vya dawa za miti shamba na kuna watanzania wengi ambao wanaamini katika dawa za miti shamba na tunaweza kuwekeza zikawa katika kiwango kizuri kama ilivyo dawa za China ambazo zinauzwa nchini, alisema Dkt Halfani.
Kuna dawa za miti shamba ambazo tunazinunua kutoka nje ya nchi na Tanzania ina dawa zake za asili lakini hatufaidiki katika hilo, aliongeza kusema.
"Teknolojia ni gharama hivyo kuna uhitaji wa kuwepo kwa uwekezaji Kinachohitajika katika dawa ni uwepo wa taarifa kamili na zinazo jitosheleza,''Dkt. Halfani aliiambia BBC.
Kwa dawa za sayansi wataalamu wanasema kwamba wana uwezo wa kutengeneza za hapa nchini na hata nje ya nchi ingawa kuna haja ya kutazama upya jinsi ya kufanya biashara na masoko nje ya nchi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Watanzania wamekuwa na desturi ya kuamini kuwa dawa kutoka nchi fulani huwa ndio nzuri jambo ambalo sio sahihi, alisema, akiongeza kuwa, "Dawa zote ni sawa, isipokuwa viwanda vinatofautiana katika ubora kwa kiasi fulani kutokana na nchi husika."
Kwa mfano dawa iliyotengenezwa Uingereza inaweza kuwa ghali kutokana na usafirishaji au teknolojia iliyotumika lakini dawa ikabaki kuwa ni ileile katika utendaji.
"Hata daktari akimuandikia mgonjwa anapaswa kueleza dawa iliyotengenezwa kufanya kazi lakini sio jina la kampuni, yaani brand name.
Dkt Halfani alitoa mfano wa paracetamol ambazo zote ni sawa katika ufanyaji kazi wake sema zina tofautiana majina na ubora kutokana na teknolojia iliyotumika na daktari hatakiwi kuandika jina la kampuni ya dawa bali aseme jina la sayansi, yaani generic name.
Rais wa nchi hiyo Dkt John Magufuli alinukuliwa na vyombo vya habari nchini humo akisisitiza kwa ni muda muafaka kuepuka aibu ya kununua dawa nchi za jirani wakati nchi hiyo ina wataalamu na mali ghafi nyingi za kuanzia ili kutengeneza dawa na vitendanishi.













