Unajua nini kuhusu wazazi na ndugu zake rais Trump?

Chanzo cha picha, Getty Images
Familia ya rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine tena inaangaziwa katika vyombo vya habari , lakini wakati huu wanaomulikwa ni wazazi wake na wala sio watoto wake.
Uchungzi mpya wa gazeti la New York Times unadai kuwa na ushahidi kwamba baba yake Trump alikwepa kulipa ushuru wa mamilioni ya dola kwa ushirikiano na watoto wake watano.
Uchunguzi huo unamlaumu Donald Trump na ndugu zake kwa "Kutumia kampuni bandia kulaghai umma huku wakidanganya kuwa ni zawadi kutoka kwa wazazi''- Madai ambayo ndugu yake mdogo, Robert amekanusha.
Tunafahamu nini kuhusiana na Fred, mke wake Mary Anne na watoto wao watano - akiwemo rais wa Marekani, Donald Trump ambaye ni mtoto wa nne?

Chanzo cha picha, Shutterstock
Fred Trump
Frederick Christ Trump, alizaliwa mjini New York mwaka 1905 na wazazi wahamiaji kutoka nchini Ujerumani, Elizabeth Christ na Frederick Trump.
Baba yake alikuwa mwekezaji katika biashara ya nyumba naye Fred pia akafuata nyayo zake kwa - kuanzisha kampuni kwa jina la mamake kwa sababu alikuwa na umri mdogo.
Alijizolea mali kupitia ujenzi wa nyumba ya gharama nafuu kwa watu wenye kipato cha kadri katika pwani ya Mashariki ya Marekani wakati na baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.
MIradi mingi kati ya yaliokuwepo yalikuwa chini ya mpango wa serikali na wakati mmoja alilazimishwa kufika mbele ya kamati ya uhasibu wa fedha za umma ya Seneti kati ya mwaka 1954, kwa madai kwamba amekuwa akijinufaisha kutokana na kandarasi za serikali.

Miaka ya 1970, alilaumiwa kwa mienendo ya ubaguzi baada ya kuwakataza watu weusi na wale wenye asili ya Puerto Rico kukodisha nyumba zake.
Watetezi wa haki za kiraia waliwasilisha kesi mahakamani dhidi yake, na wakati huo ni Donald Trump ambaye alikuwa akiangaziwa magazetini mara kwa mara akimtetea vikali babake.
Hatimaye kesi hiyo ilitatuliwa bila ya familia hiyo ya Trump kukubali kuwa ilifanya makosa.
Mary Anne Trump
Mary Anne MacLeod alikuwa na miaka 18 alipoutembelea mji wa New York, kwa mara ya kwanza baada ya kusafiri kutoka nyumbani kwao kisiwa cha Uskochi cha Lewis kutafuta kazi ya nyumbani.
Miaka sita baadaye aliolewa na Fred na kuhama nae katika eneo la Queens ambalo ni makaazi ya watu matajiri. Alifanya kazi ya kusaidia watu wasio na uwezo huku akilea watoto wake watano.
Mwaka 1942 akapata uraia wa Marekani.
Mary Anne Trump alifariki mwaka 2000 akiwa na miaka 88 mwaka mmoja na miezi kadhaa baada ya kifo cha mume wake Fred.
Maryanne Trump Barry

Chanzo cha picha, Getty Images
Maryanne Trump Barry ni kifungua mimba wa Frederick Christ Trump na Mary Anne Trump na alikuwa mmoja wa majaji wa wakuu katika jaji mahakama ya rufaa nchini Marekani.
Hata hivyo aliacha kufanya kazi mwezi Februari mwaka 2017 baada ya ndugu yake kuchaguliwa raisi wa Marekani.
Aliteuliwa katika wadhifa huo mwaka 1999 na raisi wa Marekani wakati huo Bill Clinton.
Kabla ya hapo aliteuliwa na Ronald Reagan kama jaji wa jimbo la New Jersey mwaka 1983.
Maryanne ambaye sasa ana mika 81, anasemekana kuwa na uhusiano wa karibu sana na ndugu yake Donald.
Wakati mmoja alielezea jinsi Donald alivyomtembelea hospitali kila siku baada ya kufanyiwa upasuaji.
"Mara moja ingelitosha lakini ilikuwa kama sehemu ya jukumu lake. Hiyo ni ishara ya upendo wake kwangu."
Japo anaonekana kuwa mfuasi wa chama cha Republican, amekuwa akiunga mkono haki ya utoaji mimba na uhamiaji.
Ana mtoto mmoja aliyezaa na mume wake wa kwanza. Mume wake wa pili, John Barry, ambaye pia alikuwa wakili alifariki mwaka 2000.
Fred Trump Jr

Chanzo cha picha, Getty Images
Fred Jr ni wa pili kati ya ndugu wa Donald Trump. Mwanzoni alitarajiwa kuendeleza biashara ya familia lakini baada ya kufanya kazi kwa muda na babake, Fred Jr aliondoka na kuwa rubani.
Ameoa na ana watoto wawili, Fred alionekana mtu aliyekuwa na ufanisi mkubwa maishani lakini kwa mujibu wa taarifa moja iliyochapishwa katika nakala ya mwaka 2016 ya gazeti la New York Times alikabiliwa na tatizo la unywaji pombe kupindukia akiwa na umri kati ya miaka 20 na 30.
"Miaka iliyofuatia haikuwa mizuri kwake. Alitalakiana na mke wake na kuacha kazi ya urubani kwasababu ya unywaji pombe''.
Gazeti hilo pia liliandika kuwa kufikia mwisho wa miaka ya 1970, alirejea nyumbani na kuishi na wazazi wake ambapo alianza tena kufanya kazi katika kampuni ya babake.
Fred alifariki mwaka 1981 akiwa na miaka 43.
Rais Trump aliapa kuwa hatawahi kunywa pombe wala kuvuta sigara kutokana masaibu yaliyompata ndugu yake.
"Alikuwa na athari kubwa katika maisha yangu, kwa sababu mtu hajui anakoenda na ataishia wapi," Bwana Trump alisema.
Elizabeth Trump Grau

Chanzo cha picha, Getty Images
Elizabeth ni wa tatu na ameachana na rais Trump kwa miaka minne, na anaishi maisha ya faragha ukimlinganisha na ndugu zake wengine.
Yeye ni afisa mstaafu katika sekta ya benki na ameolewa na mtayarishaji filamu James Grau.
Robert Trump

Chanzo cha picha, Getty Images
Robert ndiye kitinda mimba wa familia ya Trump na alizaliwa miaka miwili baada ya Donald.
Sawa na ndugu yake ameendeleza taaluma yake na kuwa mmoja wa viongozi wakuu katika kampuni ya familia .
Anasemekana hapendelei umaarufu kama ndugu yake na kwa sasa anaishi New York na anaelekea kustaafu wadhifa wake katika kampuni yao.
Aliripotiwa kujibu madai ya hivi punde ya New York Times akisisitiza kuwa "Vigezo vyote vya ulipaji kodi vimezingatiwa, na kodi zinazohitajika zililipwa''.













