Dyslexia: Je unapata shida kusoma, kuandika au hata kuyaelewa mambo tofauti maishani?

Iwapo una wasiwasi kuhusu uwezo wa mtoto wako kusoma, na kuandika, na ni wasiwasi ambao umegusiwa na watu walio karibu na mtoto wako kwa saa nyingi mfano waalimu, huenda ana hali inayofahamika kama Dyslexia.
Uwezo mdogo wa kusoma na kuandika ni baadhi ya dalili zinazoangaliwa kwa mtoto au hata mtu mzima ambaye huenda ana hali hiyo ya Dyslexia inayoathiri uwezo wa kujifunza.
na sio kwamba mtoto ana tatizo la kusikia au kuona.
Dyslexia ni tatizo la kawaida la kushindwa kuelewa mafunzo, ambalo huenda pia likasababisha matatizo mengine ya kusoma, kuandika, au kutambua herufi, lakini si ulemavu.
Kwa baadhi ni hali ambayo mtu huzaliwa nayo na ni vigumu hata kwa mzazi kubaini kwamba mtoto wake anatatizo hilo.
Mtu anaweza kuathirika na Dyslexia kwa njia tatu tofauti:
- Hali ya mtu kuona vyema lakini kutoweza kusoma maneno yalioandikwa kwenye vitabu au chati
- Uwezo wa kuelewa mambo yanayowasilishwa kwa matamshi na kutoweza kuandika maneno hayo na kubuni sentensi
- Na kutoweza kusoma , kuandika au hata kuelewa jinsi yanavyowasilishwa.
Miriam Njeri: 'Naona lakini siwezi kusoma wala kuandika vyema'.

Miriam Njeri, Dyslexia yangu ni ya kusoma na kuandika na hata kwa hivi sasa bado kuna maneno magumu siwezi kuyaandika vyema wala kuyasoma.
Nilipokuwa shule ya msingi mwalimu akinipa kitabu cha kusoma, singeweza kusoma lolote na wakati wa mtihani, nilikuwa siwezi kuandika lolote hata jina langu kwenye karatasi hizo za mtihani.
Sasa wakati wa mtihani mimi nilikuwa ninatazama na kuiga alichoandika rafiki yangu, hadi jina lake.
Kazi ya ziada nilikuwa siwezi kufanya, lakini mamangu alikuwa akinisaidia na akinieleza nirudie alichonifundisha sikuweza kurudia kwani wakati wote huwa nimesahau alichonifundisha na hapo nilikuwa na chapwa sana.
Marafiki zangu pia walinichukulia kama mtu asiyeelewa mambo.
Nilipelekwa katika shule ya watu wenye akili punguani nikidhaniwa kwamba mimi ni kama hao na hapo maisha yakabadilika.
Lakini niko na talanta ya kushona shanga na mikeka ya uzi na naamini nitatimiza ndoto zangu maishani.

Neema , kidato cha pili: 'Naona lakini siwezi kusoma'
Mimi nina uwezo wa kuona lakini siwezi kusoma maneno yoyote yaliyoandikwa.
Nikiangalia kitabu naona herufi na rangi tu nyeusi na maneno yote yameshikana lakini mtu akinisomea naweza kujibu swali lolote.
Wakati wa mitihani mimi humuuliza mwalimu kila sentensi ndipo niweze kujibu swali lolote.
Licha kwamba hali hii imenisumbua kwa muda mrefu, naamini nitaweza kusoma maneno muda unavyosogea.
Albert Siye: 'Siwezi kusoma lakini hesabati sio tatizo'
Nilipokuwa shule za kawaida, nilitesaka sana.
Waalimu wangu walinitoa nje ya darasa, wakanichapa wakasema siwezi kufanya lolote au hata kusoma maneno rahisi.
Walimu wakasema sifai kuwa katika shule hiyo na hapo nikapelekwa katika shule ya watu wenye ulemavu.
Shida yangu kuu ilikuwa kujisomea, lakini soma la hesabati nilikuwa nikifanya vyema.
Nilichapwa hadi ukiuangalia mwili wangu ulikuwa umefura na alama za fimbo.
Nilikuwa na chapwa sana hadi nikaanza kutoroka shule.

Geoffrey Karani: 'Siwezi kusoma, kutofautisha maneno na kuyaelewa vyema mambo tofauti'
Maisha yangu ya hapo awali siyataki kuyakumbuka.
Nilipokuwa shuleni hakuna mtu alitaka kuzungumza nami lakini kulikuwa na dada mmoja alinielewa na nilipopewa kazi nilikuwa najificha nampelekea na ananiandikia.
Nilipokuwa shule ya msingi kila mara nilikuwa nambari ya mwisho na nilikuwa naitwa mbele ya wazazi, walimu, na wanafunzi wenzangu na ningezomwa na hata kila mtu kunizungumza.
Mimi nafurahia kusoma katika darasa moja na wenzangu ambao wana hali kama yangu, na sisi sote tunaelewana vyema.
Mimi napenda kuchora picha za farasi na michoro tofauti.
Martin Gichuki: 'Nina Dyslexia lakini nimeweza kusoma hadi chuo kikuu'
Mimi nilikuwa siwezi kutofautisha baina ya herufi 'b' na 'd' na shida ya kuandika vyema hata kuyasoma maneno, lakini niliweza kusoma hesabati tangu nijifahamu nilikuwa napata alama A na niliongoza katika shule ya msingi na hata sekondari lakini katika masomo mengi sikufanya vyema.
Nilijiunga na chuo kikuu na nikapata shahada katika soma la biashara.
Kwa hivyo kila kitu kinawezakana.

Dalili za hali hii Dyslexia
Dalili au ishara zinatofautiana kutoka mtu mmoja na mwingine. Kila mtu anakuwa na udhaifu na uwezo tofauti. Baadhi yake ni:
- Mtoto kuchelewa kuzungumza
- Mtoto kukosa kutofautisha upi mkono wa kulia au kushoto.
- Mtoto anaporuka hatua moja ya kukua mf. Kukosa kutambaa na kuanza kutembea kabla wakati ufaao.
- Mtoto anapoenda shule haelewi anachosoma au kuandika.
- Shida ya kuelewa kila anachoambiwa kufanya.
- Shida ya kutofautisha baina ya herufi tofauti mf. 'B' na 'D'
- Shida ya kuandika maneno au sentensi.
- Kuchukua muda mrefu kutekeleza majukumu ya kusoma au kuandika
Dyslexia hupungua kwa kiwango flani jinsi mtu anavyokuwa. Hali hii huhitaji mtu kupokewa kwa upendo na utaratibu na wala si kupigwa au kukashifiwa.
Mtoto anaweza kuwa na kipaji maalum kinachohitajika kukuzwa vyema.
Marais ambao wameishi na hali hii ya Dyslexia?
John F. Kennedy, kakake Robert George Bush na George W. Bush pia wameishi na hali hii ya dyslexia.
Wafanyibiashara wakuu duniani ambao wameishi na hali hiyo?
- Richard Branson
- John Chambers
- Barbara Corcoran















