Nyongeza ya tozo ya uagizaji maziwa itawaathiri Watanzania vipi?

Mkazi wa Zanzibar akinywa chai yamaziwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Serikali ya Tanzania imeongeza tozo ya kuingiza maziwa na bidhaa zake kwa zaidi ya asilimia 1,200, hatua ambayo imezua mjadala kuhusu hatima ya sekta ya maziwa nchini humo.

Hatua hiyo imezua mtafaruku kiasi cha wadau katika sekta hiyo kukutana kuijadili.

Tozo hiyo ambayo ipo katika kanuni zilizotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipitishwa mwezi Agosti lakini ikaanza kutekelezwa tarehe 1 Oktoba.

Awali, waagizaji walikuwa wanalipa Sh150 kwa kilo moja ya maziwa iliyoingizwa Tanzania lakini sasa ada hiyo imepanda hadi Sh2,000, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 1,233.

Baadhi wanahisi kwamba hatua hiyo inalenga kuzuia maziwa yanayoagizwa kutoka nje, hasa Kenya na Afrika Kusini.

"Hizi si kanuni bali ni marufuku kamili ya kuingiza maziwa nchini. Haiwezekani tozo ikapanda kwa kiasi hicho. Bidhaa zetu hazitauzika tena," alisema mkurugenzi wa kampuni ya Woodland Dairy nchini, Kariras Alando, akiongea na gazeti la Mwananchi. Kampuni hiyo ina makao makuu yake nchini Afrika Kusini na huuza maziwa aina ya First Choice.

Serikali ya Tanzania hata hivyo imesema ongezeko la tozo hiyo ni la kawaida na wala halina lengo la kumuonea mtu.

Tozo itakuwa na athari zozote kwa Watanzania?

Mchambuzi wa masuala ya kiuchumi, Lenny Kasoga, ameambia BBC kwamba iwapo hatua hizo zimechukuliwa kuimarisha soko la ndani nan chi ambazo maziwa yalikuwa yanatoka hazitachukua hatua za kulipiza kisasi kama inavyofanyika kwa Marekani na Uchina, basi itakuwa na manufaa.

"Wazalishaji watazalisha kwa wingi zaidi na maziwa yakauzwa. Watanufaika na soko la ndani bila ushindani wa nje. Lakini kwa upande mwingine ushindani hufaa, unapopata mshindani unaweza ukajitahidi kuboresha zaidi ubora wa bidhaa zako, kusudi upate hata soko la nje," anasema.

Uzalishaji wa maziwa Tanzania hupungua sana wakati wa kiangazi

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uzalishaji wa maziwa Tanzania hupungua sana wakati wa kiangazi

Bw Kasoga anasema kuna wasiwasi pia kwamba huenda taifa likawa halijajiandaa vya kutosha kukidhi mahitaji ya soko la maziwa.

"Huko vijijini hali bado ni duni, wale walio na ng'ombe ndio wanaotumia maziwa...sasa hivi kauli mbiu ni viwanda na kuongeza pato tufike katika pato la kati. Je, mmejipanga? Unapokurupuka na haujajipanga, matokeo yako ni kwamba wanaoumia ni wananchi."

"Kuna wanaosema tumekomaa kiasi kwamba tujitegemee kwa kuzalisha ndani na kutozana kodi gani, mwananchi wa kawaida huwa hajali. Unapokuja wa wachumi ndipo kunatokea maswali, maamuzi yaliyochukuliwa yamemlenga nani, yatamfadi nani na kwa kipindi gani?"

Mmoja wa wadau wa sekta ya maziwa Tanzania, Samuel Makubo alisema hili ni pigo si kwa waagizaji pekee.

"Uzalishaji nchini haukidhi mahitaji. Viwanda vya maziwa vitashindwa kuagiza malighafi na vikilazimisha, basi bidhaa zao zitauzwa kwa bei kubwa," anasema.

Mmaasai akinywa maziwa

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mujibu wake, viwanda vya kusindika maziwa Tanzania vinahitaji lita 700,000 lakini huzalisha asilimia 40 ya uwezo uliopo kutokana na uhaba wa malighafi.

Kwa waagizaji wa maziwa kukiwa kilio, wasindikaji wa ndani wanashangilia kwamba wamepewa fursa kubwa wanayotakiwa kuitumia vyema.

"Tunaipongeza Serikali kwa uamuzi huu. Itaongeza motisha kwa wafugaji na kuvutia wawekezaji zaidi. Naamini watajitokeza wazalishaji wa maziwa ya unga," Fuad Jaffer, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Asas mjini Iringa aliambia gazeti la Mwananchi.

Tanzania ni nchi ya tisa duniani na ya tatu Afrika kwa wingi wa ng'ombe lakini inazalisha kiasi kidogo cha maziwa kutokana na mifugo mingi kutunzwa kienyeji hali inayochangia matumizi yake nchini kuwa chini ya viwango vya kimataifa

Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likipendekeza unywaji wa walau lita 200 kwa mwaka, takwimu zinaonyesha kuwa kila Mtanzania hunywa wastani wa lita 45 tofauti na Wakenya wanaokunywa lita 145.

Kwa hatua hiyo, wateja waliokuwa wananunua kopo la lita moja kwa Sh3,200 sasa hivi bei itapanda kwa zaidi ya asilimia 75 hivyo kutakiwa kulipa takriban Sh6,000 kwa kiasi hicho hicho.

Unywaji wa maziwa Tanzania

Kiwango cha unywaji wa maziwa Tanzania bado kiko chini ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Shirika la Chakula Duniani (FAO) linapendekeza lita 200 zinywewe kwa mtu mmoja kwa mwaka lakini nchini Tanzania kiwango hicho kwa sasa ni wastani wa lita 6 hadi 45 kwa mtu mmoja kwa mwaka.

Nchini Kenya, kiwango hicho ni kati ya lita 19 maeneo ya mashambani hadi lita 125 maeneo ya mijini.

Takwimu za Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) zinaonyesha Kenya ina ng'ombe wa maziwa 5 milioni ikiizidi Tanzania kwa zaidi ya ng'ombe 4 milioni.

Changamoto zinazoikumba Tanzania

Tanzania ni nchi yenye nafasi nzuri ya kuzalisha maziwa kwa wingi lakini bado haijaweza kutumia nafasi hiyo kikamilifu, kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia yam waka 2008 iliyolinganisha sekta ya maziwa India, Uganda na Tanzania.

Wakati Uganda inakisiwa kujitosheleza kwa maziwa, kiasi kikubwa cha maziwa yaliyo katika soko rasmi nchini Tanzania huagizwa kutoka nje.

Mwanamke akikama ng'ombe eneo la Loita Hills karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Nchini Tanzania, ingawa uzalishaji wa maziwa unaongezeka, na sekta isiyo rasmi ni kubwa zaidi, lakini baadhi ya changamoto zilizopo ni kushindwa kwa sekta kukabiliana na tatizo la kuyumba kwa kiwango cha uzalishaji kutoka msimu mmoja hadi mwingine, uhaba wa takwimu ambazo ni muhimu katika kuweka mipango na kuendesha sehemu mbalimbali za mtiririko wa thamani.

Kadhalika, kuna tatizo la uwezo mdogo na uchache wa vikundi vya wafugaji, wasindikaji, wafanya biashara viwe vya ushirika au umoja, na mtandao mbovu wa barabara vijijini.

Maziwa huzalishwa kwa wingi wakati wa masika, lakini kiasi kikubwa (asilimia 20 hadi 50) huharibika kutokana na kukosa soko. Wakati wa kiangazi kiwango cha uzalishaji hushuka na kushindwa kukidhi mahitaji ya soko.

Ukuaji wa sekta ya maziwa Tanzania pia unakwamishwa na wingi wa sheria na kanuni ambazo huongeza gharama za kuendesha biashara na pia mfumo wa kodi ambao unamwongezea mlaji mzigo wa bei ya bidhaa za maziwa yaliyosindikwa na sekta rasmi. Yote haya yanapunguza motisha kwa mwekezaji wa sekta binafsi