Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingia DRC kukabiliana na Ebola

Wahudumu wa afya wakiwa kazini

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linafanya ziara ya dharura kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufuatia mapigano makali nchini humo ambayo yametatiza jitihada za kudhibiti kuzuka kwa virusi vya Ebola.

Baraza hilo lenye wanachama 15 pia imeonya kuenea kwa Ebola kwa nchi za jirani na kuifanya kuwa vigumu zaidi kudhibiti.

Ugonjwa huo umeua watu zaidi ya mia moja tangu Agosti 1.

Mapigano makali kati ya makundi yaliyojihami katika mji wa Beni Mashariki mwa nchi yamewalynga pia wahudumu wa afya wa Umoja wa Mataifa na kupunguza kasi ya vita kuzuia kuenea kwa Ebola nchini DRC.

Maelezo ya sauti, Kampeini ya chanjo dhidi ya ugonjwa hatari wa ebola kuendelea DRC

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Dr Tedros Adhanom ameiambia BBC kwamba wanachama wa baraza hilo wataelekea DRC Ijumaa ili kutathmini matatizo ambayo wahudumu wa Umoja wa Mataifa wanakabiliwa nayo katika kutoa msaada katika maeneo yaliyoathirika.

Maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa
Maelezo ya picha, Maeneo ya kutolea huduma kwa wagonjwa

Awali, alionya kwamba mapigano kati ya makundi yenye silaha katika eneo la Beni mashariki mwa nchi yaliwalazimu wafanyakazi wa afya kupunguza kasi ya matibabu ya wale walioathirika.

Mpaka sasa, watu mia na sita wamekufa tangu mwanzo wa kuzuka kwaz homa hiyo mapema Agosti.

Maelfu ya watu wamepewa chanjo katika maeneo yaliyoathiriwa katika jitihada za kukomesha kuzuka, lakini usaidizi umezuiliwa na vurugu ambayo pia inawalenga wafanyakazi wa misaada.

Lakini mkuu wa WHO anasema wengine wengi hawajapata chanjo kwa sababu ya kukosa imani na wafanyakazi wa afya.

Wahudumu wa afya wakijiandaa kwenda sehemu zenye mlipuko wa ebola

Baraza la usalama pia limeonya kwamba homa hiyo inaweza i kuenea katika taifa jirani la Uganda baada ya kugunduliwa kwa kesi kadhaa katika eneo la mpakani.

WHO imekubaliana na tathmini hiyo.

Mlipuko huu wa hivi karibuni, ulioanza katika mji wa Kaskazini Kivu wa Mangina, ni wa 10 kuathiri DRC tangu 1976.