Mzee Joseph Ngala: Sijafaidika na muziki wa bango Mombasa Kenya

Nwanamuziki wa bango mzee Joseph Ngala

Licha ya sifa zake kote Afrika Mashariki, Mzee Joseph Ngala, anayejulikana kwa mdundo wake wa bango anasema hajafaidika ipasavyo kwenye fani ya muziki.

``Sijafaidika kwa muziki kinyume na dhana ya wengi kwamba mimi ni tajiri,'' anasema Mzee Ngala nilipomtembelea kwake nyumbani mtaa wa Frere Town, jijini Mombasa.

``Tungali tunalipisha kiwango chetu cha zamani, hatujaongeza bei maanake tukiongeza wanaotulipa watakimbilia bendi zingine kwa malipo ya chini. Tunaumia sana kwa malipo haya lakini hamna namna itabidi tuendelee hivyo.''

Bendi ya Mzee Ngala ijulikanayo kwa jina la Bango Sounds ina jumla ya watu kumi, na wanagawana chochote wapatacho wanapotumbuiza mashabiki wao.

Bendi hiyo hucheza kwenye sherehe za harusi, baadhi ya hoteli kubwa mjini Mombasa na sehemu zingine nchini Kenya.

Je, Mzee Ngala amewekeza chochote cha kujivunia malipo yake kwenye muziki?

``Hapo sijaweza kabisa kwa sababu mapato yangu yanategemewa na wengi nyumbani, zaidi pesa ninazopata ni za tumbo tu,'' anasema Mzee Ngala ambaye anatimiza miaka 83 Octoba tarehe 14 mwaka huu.

Mzee Ngala na tarumbeta yake

``Kwa hali hii ya kubambanya maisha kweli ni magumu sana lakini muziki nao uko ndani ya damu yangu siwezi kuuwacha.

Nikiacha nitakula nini na malipo ya uzeeni ya shirika la reli nilipokua nafanya kazi ni ya shida shida. Nitazidi kupambana na siku moja maulana atanifungulia njia. Sijafa moyo hata kidogo.''

Mzee Ngala hatahivyo anasema akipata kazi nzuri na mashahara mnono kila mwezi ataachana na muziki, na wazo la kuimba peke yake bado hajalifikiria.

``Kila kitu chategemea mazoea, kuimba peke yangu nikipiga saxa si wazo mbaya lakini sijalifikiria,'' anasema Mzee Ngala ambaye alianza kujishugulisha na muziki mwaka wa 1954 akiwa anafanya kazi na shirika la reli la Kenya.

``Tena kuna gharama hapo za vifaa kama nitaamua kuimba peke yangu na mimi pesa hizo kwa sasa sina kusema kweli. Na isitoshe nguvu zenyewe za kusimama kwa muda mrefu sina. Kama serikali yetu ya Kenya inaweza kunisaidia nitashukuru pia lakini hilo ni kwa hiari yao.''

Miongoni mwa nyimbo zake ambazo zimetia for a for a ni Naitaka Bango, Kadzo na Naona Raha.

Vijana wake, Kilanga na Jimmy Ngala wamefuata nyayo za baba yao, na wote wako na bendi zao mjini Mombasa.