Kwa Picha: Magufuli akutana na marais wa zamani, na Edward Lowassa

Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli amekutana na marais wa zamani pamoja na viongozi wengine wa zamani walioshikilia nyadhifa mbalimbali serikali.

Rais huyo aliwapa mwaliko wa kukutana naye ikulu, ambapo mkutano ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es salaam.

Picha zilizotolewa na ikulu hata hivyo zinaonesha Bw Kikwete hakuhudhuria mkutano huo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kukutana na viongozi hao wakuu wastaafu na taarifa ya ikulu imesema lengo lilikuwa "kupokea ushauri na maoni yao juu ya uendeshaji wa Serikali na mustakabali wa Taifa".

Ni miaka miwili na nusu sasa tangu serikali ya Awamu ya Tano yake Rais Magufuli ilipoingia madarakani.

Bw Lowassa aliwania urais mwaka 2015 dhidi ya Dkt Magufuli lakini akamaliza akiwa wa pili.

Miongoni mwa waliofika kulikuwa na rais wa zamani Benjamin Mkapa.

Rais Magufuli ametumia fursa hiyo pia kuwaeleza viongozi hao juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali yake ambapo ni pamoja na uongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambao amesema umeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 800 hadi kufikia Shilingi Trilioni 1.3 kwa mwezi.

Aidha, kuna kuanza ujenzi wa reli ya kisasa kuanzia Dar es Salaam hadi Dodoma utakaogharimu Shilingi Trilioni 7.26, kujenga mradi wa umeme katika mto Rufiji (Stieglers' Gorge) utakaozalisha Megawati 2,100 za umeme, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo na kuongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Unaweza kusoma pia: