Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Lowassa: Magufuli aliniomba nirudi CCM
Mjumbe wa kamati kuu ya chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Edward Lowassa amefichua kuwa Rais John Magufuli alimuomba arejee chama tawala cha CCM wakati wa mazungumzo yao juma lililopita.
Katika taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, Lowassa ameeleza: "Ujumbe wa Rais Magufuli ulikuwa kunishawishi kutaka nirejee CCM, suala ambalo sikukubaliana nalo na nilimueleza Rais ya kwamba uamuzi wangu wa kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA haukuwa wa kubahatisha".
Wiki iliopita, kiongozi huyo wa upinzani nchini Tanzania, ambaye pia ni Waziri mkuu wa zamani, alikutana na Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli Ikulu na kumsifu sana kwa kazi anayoifanya.
Ni hatua ambayo iliwashangaza wengi kwani si kawaida kwa kiongozi huyo kumsifu Rais Magufuli kwani kwa muda amekuwa akikosoa utawala wake.
Bw Lowassa aliwania urais kupitia chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 lakini akashindwa na Dkt Magufuli aliyewania kupitia Chama cha Mapinduzi.