Petroli yasafirishwa kwa chupa kutoka Dar es Salaam hadi Mafia

Mafuta hupimwa kwa chupa kisiwani Mafia kisha kuuzwa kwa bei ya juu kuliko maeneo ya karibu kama Dar es salaam Tanzania.
Maelezo ya picha, Mafuta hupimwa kwa chupa kisiwani Mafia kisha kuuzwa kwa bei ya juu kuliko maeneo ya karibu kama Dar es salaam Tanzania.

Kisiwani Mafia Tanzania, Mafuta ya petrol na dizeli huuzwa kwa reja reja katika vibanda, huku kukiwa hakuna sheli ya mafuta kwa ajili ya mahitaji ya matumizi ya watu wenye vyombo vya usafiri kisiwani humo.

Mafuta hayo hupimwa kwa chupa kisha kuuzwa kwa bei ya juu kuliko maeneo ya karibu kama Dar es salaam.

Wauzaji wanasema sababu kuu ya hali hiyo ni kutokua na usafiri wa kuaminika wa kuingia na kutoka kisiwani humo.

Wauzaji hufunga safari kutoka Mafia hadi maeneo ya karibu kama Dar es salaam na pwani kisha hununua mafuta katika sheli za mafuta kama watu wengine wenye magari wanavyofanya, wao huweka kwenye mapipa na kusafirisha kwa mashua hadi kisiwani mafia.

Wauzaji hufunga safari kwa mashua kutoka Mafia hadi maeneo ya karibu kama Dar es salaam kununua mafuta
Maelezo ya picha, Wauzaji hufunga safari kwa mashua kutoka Mafia hadi maeneo ya karibu kama Dar es salaam kununua mafuta

Kwa kawaida hununua mafuta kama petrol kwa dola moja ya marekani kwa lita moja kisha huongeza pesa kidogo kwa wanunuzi yanapofika mafia.

Mashua hizo huweza kuchukua siku kadhaa kutokana na hali ya upepo wa bahari na wauzaji wa mafuta hayo wanasema kuna uwezekano wa mapipa kupasuka katika mashua hizo hivyo hupata hasara.

Katika vibanda katika eneo hilo wauzaji wengi wamekua wakiogopa kuzungumza kutokana na kutojua hatma ya kazi yao, ingawa wamekua msaada mkubwa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri.

Mmoja wa wauzaji, Abdalah Mohamed anasema kuwa gharama wanayonunua mafuta na kuuza, wanapata faida kidogo sana kutokana na gharama ya usafirishaji huo wa mafuta.

Vibanda vya kuuza mafuta kama hivi vimekuwa msaada mkubwa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri
Maelezo ya picha, Vibanda vya kuuza mafuta kama hivi vimekuwa msaada mkubwa kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri

''tunayavusha katika bahari na bahari kuna wakati inakua inachafuka, vitu vinapinduka lakini sasa ndio kazi hiyo'' Anasema bwana Abdallah

Wategemeaji wa mafuta kuendesha kazi zao, kama wamiliki wa taxi na bajaji, wanasema mafuta huchukua muda mrefu kufika hivyo biashara zao huweza kuathirika.

Bakari ismail ni dereva wa Tax anasema kuwa amewahi kusimamisha Bashara yake kutokana uhaba wa mafuta.

''Nimewahi kupaki gari wa muda wa siku nne, wateja wananipigia simu nawaambia kuwa sina mafuta hadi nilivyopata mafuta nikaendelea na biashara''

Maelezo ya sauti, Visiwa vya Zanzibar ambavyo havina shule za sekondari

Serikali imewezaje kuruhusu mafuta kuuzwa kwa namna hii?

Mkuu wa wilaya ya Mafia, Shaibu Nnondoma anasema kuwa wameruhusu wauzaji hawa wa mafuta katika vibanda kutokana na usafiri wa mashua hauwezi kuleta mafuta kwa wingi, hivyo wafanya biashara hawa wamekua na umuhimu mkubwa katika upatikanaji wa mafuta kisiwani hapa.

''Wafanyabiashara wadogo wadogo wananua kwa bei ya kawaida na wanakuja kuuza hapa, tumewaruhusu wauze kwa bei ya soko itakavyowaruhusu kwasababu akiuza bei ndogo sana hawezi kupata faida na wanasaidia sana wakazi wa hapa''amesema Nnondoma.

Hata hivyo hapo awali walikua wanauza karibu na makazi ya watu , lakini uongozi wa kisiwa hiki uliwahamishia mbali na makazi ya watu.