Simone Biles: Nilidhalishwa kingono na daktari wa timu

Biles

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Biles alishinda medali nne za dhahabu katika michezo ya Rio Olimpiki mwaka 2016

Mshindi wa medali nne katika michezo ya Olimpiki Simone Biles, amesema kuwa alinyanyaswa kingono na aliyekuwa daktari wa timu ya mazoezi ya viungo ya Marekani Larry Nassar.

Katika taarifa ilionesha hisia nyingi, Biles,nyota wa michezo ya Rio, alisema hangemruhusu Nassar "kuiba furaha na upendo wangu"

Nassar aliyefungwa kwa miaka 60 kwa kupatikana na picha za watoto wakidhalilishwa kingono,pia alikubali kwamba aliwanyanyasa wanamichezo wa mazoezi ya viungo.

Wanaolimpiki watatu kutoka Wamarekani wamemshtumu Nassar kwa kuwadhalilisha kingono akiwa akijifanya ya kuwatibu. Mmoja wapo ni Gabby Douglas aliyeshinda dhahabu pamoja na Biles katika michezo ya timu katika michezo ya Olimpiki Rio

Nassar atahukumiwa mwezi huu baada ya kesi mbili ambazo amekubali mashtaka ya kuwanyanyasa wachezaji wawili wakike wa mazoezi ya viungo

Akiwa na umri wa miaka 54, alifungwa Disemba kwa mashtaka matatu yanayohusu picha za udhalilishaji wa watoto kwenye kompyuta yake.

Mawakili wa Nassar waliambia BBC kuwa hawatatoa majibu kwa taarifa ya Biles.

Shirika la mazoezi ya viungo Marekani limesema kuwa wamejisikia vibaya na wamekasirishwa na vitendo vilivyofanywa na Larry Nassar dhidi ya Simone Biles na wachezaji wengine.

Nani mwengine alijitokeza?

Nassar alifanya kazi katika programu ya mazoezi ya viungo Marekani kutoka mnamo mwaka 1980 hadi mwezi Julai 2015, baada ya bodi ya mamlakia ya michezo kumfuta kazi.

Zaidi ya wanawake 130 wametoa mashtaka dhidi yake wakimshutumu kwa udhalilishaji.

Washindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki Aly Raisman na McKayla Maroney ni miongoni ya wale waliojitokeza.

Kesi ya Nassar ilikuwa katika kashfa iliopelekea rais wa shirika la mazoezi ya viungo Steve Penny kujiuzulu 2016. Penny alishtumiwa na wahanga kwa kushindwa kuripoti mashtaka ya udhalillishaji yaliyopelekwa kwake.

Nassar worked for USA Gymnastics and Michigan State University

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Nassar alifanya kazi na shirika la mazoezi ya viungo na chuo cha Michigan State