Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matokeo ya uchaguzi wa Marekani 2020: Wasifu wa Donald Trump, tajiri anayepigania kusalia Ikulu ya White House
Donald Trump, Rais wa Marekani, kwa sasa yupo katika mpambano mkali wa kuzuia kuwa rais wa kwanza wa taifa hilo kwa takriban miongo mitatu kuongoza kwa kipindi kimoja tu cha miaka minne.
Kwa saa kadhaa sasa toka matokeo ya uchaguzi yaanze kutangazwa, amekuwa nyuma ya mshindani wake Joe Biden. Hata hivyo mbio za ushindi bado hazijafikia kikomo, na msamiati wa kushindwa ni adimu kabisa katika kamusi ya Trump.
Amekuwa mtu anayeangazia sana ushindi katika maisha yake na alikuwa tangu mwanzo amesema ni lazima afanikiwe katika kupata tuzo kuu duniani na hata kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani.
Trump ni tajiri anayemiliki majumba mengi na mahoteli, na hata kabla ya kushinda urais miaka minne ilopita alikuwa maarufu kwa kuendesha kipindi cha maisha ya uhalisia kwenye runinga.
Kwa wafuasi wake, yeye ndiye anayeweza kuleta ufanisi kwa Marekani.
Kwao, huyu ni tajiri shupavu anayeweza kusuluhisha matatizo yote ya nchi ambayo wanahisi yameshusha hadhi ya Marekani duniani.
Wengi wao ni raia wa Marekani wafanyikazi hasa wenye asili ya Kizungu na walio na maisha ya kadri.
Lakini kwa wakosoaji wake, Trump anaonekana ni mbaguzi na mfitini, mfidhuli mkubwa ambaye hakustahili toka awali kuwa kiongozi wa taifa lenye nguvu zaidi duniani.
Je, urais wake umekuwaje?
Trump, akiwa mgeni kabisa kwenye ulimwengu wa siasa alistaajabisha dunia Novemba 2016 kwa kumuangusha mwanasiasa mkongwe Hillary Clinton.
Alipata kura za wajumbe 278, Bi Clinton akiwa na 218. Mshindi alihitajika kupata kura 270 za wajumbe.
Kinyume na matarajio ya wengi, ndoto ya kisiasa ya Trump ikatimia. Lakini miaka minne ya urais wa Trump imeendaje mpaka sasa?
Kama ilivyokuwa kwenye kampeni yake ya awali, urais wake pia umejaa mambo ambayo baadhi wameyatafsiri kama ni viroja.
Mwezi wake wa kwanza madarakani, Januari 2017, Trump alitia saini amri yake ya kwanza, kuzuia wasafiri kuingia Marekani kutoka mataifa saba ambayo mengi ni ya wenye raia wengi Waislamu. Japo uamuzi huo umetafsiriwa na wengi kama ni wa kibaguzi, Mahakama ya juu zaidi ya Marekani ilitoa hukumu ya kumuunga mkono Trump.
Baada ya hapo, akaishangaza Marekani kwa kumtimua kazi Mkurugenzi wa Shirika la Ukachero la FBI James Comey. Kufutwa kazi kwa Comey kulitafsiriwa ni kama sehemu ya njama ya kuficha ukweli kuwa Urusi ilisaidia Trump kuingia madarakani. Hata hivyo uchunguzi rasmi wa tuhuma hizo ulionesha kuwa hakukuwa na njama yoyote ya kijinai baina ya kampeni ya Trump na Urusi.
Baada ya hapo zikaja tuhuma kwamba Trump ameishinikiza serikali ya nchi moja kuchunguza tuhuma ambazo zingeweza kumpaka matope mpinzani wake Joe Biden. Tuhuma hizo zikafanya Trump apigiwe kura ya kutokuwa na imani na Bunge la Congress ambalo lina wajumbe wengi wa Democrats, hata hivyo, Bunge la Senate lenye wajumbe wengi kutoka chama chake cha Republican wakamsafisha na kusalia madarakani.
Licha ya yote, Bwana Trump ameweza kusalia na umaarufu wake na ushawishi katika maeneo ambayo walimchagua toka awali, hilo ni kutokana na kutekeleza ahadi za kampeni ambazo alizitoa. Bila shaka, jambo alofanya Trump ambalo litaendelea kudumu nchini humo na kuathiri juu ya mustakabali wa sera za nchi hiyo ni uteuzi wake wa majaji watatu wa mrengo wa kihafidhina katika Mahakama ya Juu Zaidi ya nchi hiyo.
Uchaguzi wa mwaka huu umetawaliwa na janga la virusi vya corona na katika suala hilo, Trump amekosolewa vikali namna alivyolishughulikia. Marekani inaongoza duniani kwa idadi ya maambukizi na vifo. Kampeni yake ilibidi isimame kwa muda baada ya yeye mwenyewe kuambukizwa virusi hivyo.
Kwa sasa, kura zimeshamalizwa kupigwa, na mchakato wa kuzihesabu unaendelea ili kuona kama Wamarekani wamemrejesha katika Ikulu ya White House kwa miaka mingine ama wamemtoa na kumpa nafasi hasimu wake Joe Biden.
Failia ya Trump
Donald Trump ameo mara tatu, Ivana na Marla Maples, mke wa kwanza na wa pili mtawalia ambao wote ametalikiana nao. Mke wake wa sasa ni Bi Melania.
Bwana Trump ana watoto watoto watano, watatu wa kiume Donald Trump Jr, Eric, Barron na watoto wawili wa kike Ivanka na Tiffany.
Rais huyo wa 45 wa Marekani alizaliwa Juni 14 mwaka wa 1946, mjini New York, akiwa mtoto wa tano kati ya watoto sita.
Babake Fred alikuwa tajiri aliyemilki majumba na babu zake Trump walikua wahamiaji kutoka Ujerumani.
Mamake Mary alikuwa mzaliwa wa Scotland.
Tangu utotoni, Trump alikuwa mtundu na wazazi wake walimpeleka shule ya msingi iliyofadhiliwa na jeshi mjini New York.
Baadaye alifuzu kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania, kitivo cha elimu ya biashara mwaka wa 1968.
Alifanya kazi katika kampuni ya babake ambaye aliendesha biashara ya kuuza nyumba kwa raia wa kipato cha kadiri, viungani mwa New York.
Hata hivyo Donald Trump alikuwa na ndoto ya kufanya biashara nje ya makaazi ya Queens na Brooklyn.
Aliwekeza katika biashara kubwa ya ujenzi na kuweza kujenga mojawapo ya mijengo ya kifahari zaidi nchini Marekani. Alifanikiwa kutokana na sera ya kiuchumi iliyowekwa na utawala wa Reagan miaka wa 1980.
Kuna tofauti kuhusu utajiri hasa wa Trump. Aliwahi kuambia tume ya uchaguzi kwamba anao utajiri wa kima cha dola bilioni 10. Hata hivyo jarida la Forbes limenadi kwamba utajiri wa Trump haufikii juu ya bola bilioni 4.5.
Lakini unapotembea barabara kuu za Manhattan, kampuni ya Trump imeweka mabawa yake kwa majumba ya kifahari yaliyofuatana.
Yapo mahoteli, viwanja vya mchezo wa gofu, makazi ya kifahari, majumba ya kamari kutoka Carlifonia hadi Mumbai nembo yake ikiwa ni Trump.
Ameandika Riwaya kadhaa kuhusu biashara, huku umaarufu wake uking'aa zaidi katika makala yanayoelezea maisha halisi, "The Apprentice," katika runinga ya NBC. Hata hivyo alitupwa nje ya makala hayo baada ya kutoa kauli zilizowakera raia wa Mexico.