Huyu ndiye George Foreman bondia mchungaji aliyetajirikia 'jikoni' na kuwapa watoto wake majina yake

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Na Yusuph Mazimu

Gwiji wa ngumi za uzito wa juu George Foreman amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76, kwa mujibu wa taarifa ya familia yake.

Akiwa maarufu kwa jina la Big George kwenye ulingo wa masumbwi, Mmarekani huyu alijenga moja ya taaluma za kipekee na za kudumu zaidi katika mchezo huo, akishinda medali ya dhahabu ya Olimpiki mwaka 1968 na kutwaa taji la dunia mara mbili kwa tofauti ya miaka 21.

Kama walivyo mabondia wengi wenye asili ya Afrika, kama ilivyo kwa Mike Tyson, ni matokeo ya uhalifu. Foreman alizaliwa Marshall, Texas, mnamo Januari 10, 1949, na alikulia pamoja na ndugu zake sita akilelewa na mama yake pekee katika mazingira ya ubaguzi wa rangi na shida kubwa Kusini mwa Marekani.

Aliacha shule na kujiingiza kwenye uhalifu wa mitaani kabla ya hatimaye kupata mwelekeo katika mchezo wa ngumi.

Akiwa na umri wa miaka 16, alijiunga na Mpango maalumu wa serikali ulioitwa Jobs Corps, ambao ulikuwa ukitoa mafunzo ya ufundi stadi na nafasi za kazi kwa waliokuwa na uhitaji.

Akiwa huko alikutana na Doc Broadus, mshauri wa ndondi ambaye alitambua uwezo wake na kuanza kumfundisha. Foreman alionyesha kipaji kwa haraka, akishinda pambano lake la kwanza la ngumi za ridhaa kwa knock out katika raundi ya kwanza.

w

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, George Foreman katika moja ya mapambano yake enzi za uhai wake

Aliendelea kumfundisha na kumsaidia kuelekeza nguvu zake kwenye mchezo huo, na hatimaye kumfanya kushinda medali ya dhahabu kwenye Olimpiki ya 1968, huko Mexico City akiwa na miaka 19 tu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya Olimpiki, akageukia ndondi za kulipwa na kushinda mapambano 37 mfululizo. Mnamo 1973, alimshinda bingwa mtetezi Joe Frazier aliyekuwa hajawahi kushindwa, katika pambano lililofanyika Kingston, Jamaica, akimdondosha chini mara sita katika raundi mbili za kwanza. Foreman alipoteza taji lake la kwanza kwa Muhammad Ali katika pambano lao maarufu Rumble in the Jungle mwaka 1974.

Pambano hilo lililochezwa huko Kinshasa, Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), linabaki kuwa moja ya mapambano maarufu zaidi katika historia ya masumbwi. Hata hivyo, rekodi yake ya masumbwi ya kulipwa ilijumuisha ushindi wa ajabu wa mapambano 76, huku 68 kati yao akiwashinda wapinzani wake kwa knock-out, karibu mara mbili ya idadi ya Ali.

Katika maisha yake yote ya ndondi, alishindwa mara tano pekee.

Alistaafu masumbwi mwaka 1997. Alirejea kwenye ndondi baada ya kusimama kwa muda wa muongo mmoja, na alifanikiwa kurejesha taji la uzito wa juu akiwa na umri wa miaka 45, na kuwa bingwa mzee zaidi wa uzani wa juu zaidi katika historia ya masumbwi.

Maisha baada ya kustaafu ngumi

a

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Foreman alijiingiza zaidi kutangaza majiko ya kubanika nyama na vyakula vingine yaliyompa utajiri mkubwa

Baada ya kupoteza pambano lake la pili la kulipwa, Foreman alistaafu mwaka 1977 na akaamua kuwa mchungaji aliyepewa daraja la kidini katika Kanisa la Lord Jesus Christ huko Texas, ambalo alilianzisha na kulijenga mwenyewe.

Alijiingiza hasa kwenye masuala ya kidini na kijamii. Akahubiri na kutoa neno la kumtukuza Mungu kwa jamii yake.

Familia yake iliandika kwenye Instagram Ijumaa usiku: Alikuwa "Mhubiri mwenye imani kubwa, mume mwaminifu, baba mpendwa, na babu na babu mkubwa mwenye fahari. Aliishi maisha yaliyojaa imani isiyoyumba, unyenyekevu, na kusudi thabiti."

Taarifa hiyo iliongeza: "Mwanaharakati wa kibinadamu, mshindi wa Olimpiki, na bingwa wa dunia wa uzito wa juu mara mbili. Alikuwa mtu mwenye kuheshimika sana - mtu wa nidhamu, msimamo, na mtetezi wa urithi wake, akipambana bila kuchoka kulinda jina lake zuri kwa ajili ya familia yake."

Alikubali jina lake litumike kwenye majiko choma yaliyoitwa George Foreman Grill, uamuzi uliomletea utajiri mkubwa zaidi kuliko hata mapato yake yote ya ndondi. Majiko hayo yalimuingizia karibu dola $200milioni. Yakimlipa karibu $4.5milioni kwa mwezi. Kuna wakati aliitwa mpishi kwa kazi yake ya kuyatangaza majiko hayo.

Nani kurithi utajiri wake?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Freeda Foreman, binti wa Foreman alifuata nyayo za baba yake. Akijiunga na ngumi za kulipwa akicheza mapambano 6 na kupoteza moja tu.

Foreman anatajwa kuwa na utajiri wa zaidi ya dola $300milioni kutokana na vyanzo mbalimbali. Ni utajiri mkubwa unaweza kuiendeleza familia yake kubwa.

Bondia huyu ameoa mara tano katika maisha yake. Foreman alifunga ndoa na Mary Joan Martelly mnamo 1985 na walikaa pamoja kwa karibu miaka 40. Mary, ambaye mara nyingi hujulikana kama Joan, alikuwa mke wake wa tano, kufuatia ndoa za awali na Adrienne Calhoun (1971-1974), Cynthia Lewis (1977-1979), Sharon Goodson (1981-1982), na Andrea Skeete (1982-1985).

Ameacha watoto 12, wakiwemo wakiume watano ambao wote amewapa jina lake moja la George Edward Foreman, mara nyingi akiwatofautisha kwa majina ya utani na kutumia namba (kwa mfano, George Jr., George III ("Mtawa"), George IV ("Gurudumu Kubwa"), George V ("Nyekundu"), na George VI ("Joe").

Mabinti aliwapa majina yasiyoleta mkanganyiko wa utambuzi: Natalia, Leola aliozaa na mke wa kwanza. Wengine ni Michi, Freeda anayedaiwa kujiua mwaka 2019, huku Georgetta Isabella na Courtney akiwaasili.