China ''yatuma ndege 27 za kivita katika anga ya Taiwan'' baada ya Pelosi kuondoka

TH

Chanzo cha picha, AFP

China imeanza mazoezi yake makubwa zaidi ya kijeshi katika bahari karibu na Taiwan kufuatia ziara ya mwanasiasa wa Marekani Nancy Pelosi.

Mazoezi ya moto ya moja kwa moja yalianza saa 12:00 kwa saa za ndani (04:00 GMT) na katika maeneo kadhaa yalipaswa kufanyika ndani ya maili 12 kutoka kisiwa hicho.

Taiwan ilisema China inajaribu kubadilisha hali ilivyo katika eneo hilo.

Bi Pelosi alifanya ziara fupi lakini yenye utata nchini Taiwan, ambayo China inachukulia kama jimbo lililojitenga.

Mazoezi hayo ni jibu kuu la Beijing, ingawa pia imezuia biashara fulani na kisiwa hicho.

Mazoezi hayo yanatarajiwa kufanyika katika njia za maji zenye shughuli nyingi na yatajumuisha ufyatuaji wa risasi za masafa marefu, Beijing inasema.

Taiwan inasema ni sawa na kuzuiwa kwa bahari na angani huku Marekani ikisema kuwa mazoezi hayo hayakuwajibiki na yanaweza kusogea nje ya udhibiti.

Ndege za China aina ya J-10

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ndege za China aina ya J-10

Ndege katika eneo la Taiwan

Taiwan imesema kwamba China imetuma ndege 27 za kivita katika eneo lake la ulinzi wa anga na 22 kati yao zimevuka mstari wa kati unaotenganisha kisiwa hicho kinachojiendesha na China, huku kukiwa na mvutano unaoongezeka katika eneo hilo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Na China imeelezea hasira yake juu ya ziara ya Spika wa Bunge Nancy Pelosi nchini Taiwan, ziara ya afisa wa ngazi ya juu wa Marekani katika kisiwa hicho kwa miaka 25, kwa kutangaza mfululizo wa mazoezi ya kijeshi ambayo itafanya karibu na Taiwan.

Wizara ya mambo ya nje ya China ilimwita balozi wa Marekani mjini Beijing na kusitisha uagizaji wa bidhaa nyingi za kilimo kutoka Taiwan.

Beijing inaichukulia Taiwan kama eneo la Uchina, lakini Taiwan inakataa madai ya China na kuapa kujitetea.

Katika ongezeko la hivi karibuni la mvutano katika kisiwa cha Taiwan, Taiwan ilisema kuwa imetuma ndege na kusambaza mifumo ya makombora "kufuatilia" shughuli za jeshi la China katika eneo lake la ulinzi wa anga.

Katika miaka ya hivi karibuni, Taiwan imekuwa ikilalamika kuhusu safari za mara kwa mara za jeshi la anga la China karibu na kisiwa hicho, hasa katika sehemu ya kusini-magharibi ya eneo la ulinzi wa anga la Taiwan.

Wizara ya Ulinzi ya Taiwan ilisema ujumbe wa hivi punde zaidi wa China ni pamoja na ndege 16 za kivita aina ya Sukhoi-30 na aina nyingine 11.

Chanzo kinachofahamu mipango ya usalama ya Taiwan kiliiambia Reuters kwamba ndege 22 ambazo zilivuka mstari wa kati hazikuruka ndani ya eneo lisilo rasmi lisilomilikiwa na upande wowote.

Kawaida, ndege kutoka pande zote mbili hazivuka mstari wa kati.

Taiwan ilisema mapema Jumatano kwamba baadhi ya mazoezi ya kijeshi yaliyopangwa ya China yatafanyika ndani ya eneo la ulinzi wa anga na baharini la maili 12 la Taiwan, hatua ambayo haijawahi kufanywa ambayo afisa mkuu wa jeshi la Taiwan alielezea kama "kiwango cha kizuizi cha majini na anga cha Taiwan."

Pelosi akiondoka Taiwan mapema siku ya Jumatano

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Pelosi akiondoka Taiwan mapema siku ya Jumatano

Pelosi alisema mwishoni mwa ziara yake nchini Taiwan kwamba China haiwezi kuzuia viongozi wa dunia kuzuru kisiwa hicho.

"Inasikitisha kwamba Taiwan ilizuiwa kushiriki katika mikutano ya kimataifa, ambayo hivi karibuni zaidi ilikuwa Shirika la Afya Ulimwenguni, kutokana na pingamizi la Chama cha Kikomunisti cha China," Pelosi alisema katika taarifa yake.

"Wakati wao (Wachina) wanaweza kuzuia Taiwan kutuma viongozi wake kwenye vikao vya kimataifa, hawawezi kuzuia viongozi wa dunia au mtu yeyote kusafiri hadi Taiwan kuonyesha heshima kwa demokrasia yake inayoendelea, kuangazia mafanikio yake mengi, na kuthibitisha tena dhamira yetu ya kuendelea ushirikiano, "aliongeza.

Je jamii ya kimataifa inasemaje?

Waandamanaji wanaoiunga mkono China wakiikatakata bendera ya Marekani Hongkong

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Waandamanaji wanaoiunga mkono China wakiikatakata bendera ya Marekani Hongkong

Katika maoni ya kimataifa, mawaziri wa mambo ya nje wa Kundi la nchi saba kuu walielezea wasiwasi wao juu ya "vitendo vya vitisho" vya China kuhusu Mlango wa-Bahari ya Taiwan.

Katika taarifa rasmi, wameonya kwamba hatua za China "zinahatarisha ongezeko la mzozo usio wa lazima" na kuitaka Beijing kutotafuta "kubadilisha hali iliyopo kwa nguvu" katika eneo hilo.

Pelosi aliondoka Taiwan mapema Jumatano, baada ya ziara ambayo China iliona kama "ya uchochezi."

Katika ziara hiyo, alisema, wajumbe wa Marekani "walikuja kusema bila shaka kwamba hatutaacha ahadi yetu kwa Taiwan na kwamba tunajivunia urafiki wetu wa kudumu."

Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen alisisitiza Jumatano kwamba nchi yake "haitarudi nyuma" kutokana na tishio kutoka kwa China.

Wakati wa mkutano na Tsai huko Taipei, Pelosi alisema alikuja katika eneo hilo "kwa amani", akisisitiza wakati huo huo kwamba Marekani haitaacha ahadi zake kwa kisiwa hicho cha kidemokrasia, ambacho kinaishi chini ya tishio la mara kwa mara la uvamizi wa Wachina.

Mazoezi makali ya kijeshi

Nchini Marekani, msemaji wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Kirby alisema kuwa ziara ya Pelosi inaendana na sera ya Marekani, ambayo ni kusisitiza umoja wa China (China moja) na hakuna haja ya kugeuza (ziara ya Pelosi) kuwa mgogoro.

Vyombo vya habari vya serikali ya China vilithibitisha mapema kwamba jeshi litafanya mazoezi ya moto kwa siku tatu, kuanzia Jumatano, na meli zote na ndege za kiraia kuingia katika maeneo ya mazoezi.

Uchina pia ilisimamisha uagizaji bidhaa kutoka kwa wazalishaji 35 wa biskuti na keki wa Taiwan, katika onyo kabla ya ziara ya Pelosi.

Biskuti na keki ni bidhaa muhimu za biashara kati ya Taiwan na Uchina, ikiwa ni pamoja na Hong Kong.

China

Takriban theluthi mbili ya mauzo ya nje kutoka Taiwan mwaka 2021 yalikuwa biskuti na keki, zenye thamani ya jumla ya dola milioni 646, vyombo vya habari vya Taiwan viliripoti.

Mnamo 2020, thamani ilifikia $ 660 milioni na iliwakilisha asilimia 37 ya jumla ya mauzo ya nje.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya kampuni 100 nchini Taiwan zitalazimika kuacha kufanya biashara na Uchina baada ya adhabu kuanza kutekelezwa.

Kisiwa cha Tawian
Maelezo ya picha, Kisiwa cha Tawian

Sera ya "China moja" ni ipi?

Tangu mwaka 1979, Marekani imekubali kutambua sera ya "China moja".

Hii ina maana kwamba Marekani inatambua msimamo wa China, na kwamba kuna serikali moja tu ya China.

Chini ya sera hii, Marekani ina uhusiano rasmi na China, si Taiwan.

Lakini Marekani bado inakiunga mkono kisiwa hicho na imeahidi kukisaidia kujilinda, ikiwa ni pamoja na kukipatia silaha.

Sera ya "China moja" ni msingi mkuu wa uhusiano kati ya China na Marekani.

Chama tawala cha Kikomunisti nchini China kinatishia kutumia nguvu ikiwa Taiwan itajitangazia uhuru wake rasmi