Nancy Pelosi: Marekani haitaitelekeza Taiwan

Chanzo cha picha, Getty Images
Spika wa Marekani Nancy Pelosi amekutana na Rais wa Taiwan Tsai Ing-wen katika ziara ambayo imelaaniwa vikali na China.
Bi Pelosi, mwanasiasa mkongwe zaidi wa Marekani kuzuru Taiwan katika kipindi cha miaka 25, amesema ujumbe wake umekuja kuweka "dhahiri" kwamba Marekani "haitakitelekeza" kisiwa hicho.
Uchina hapo awali ilisema Marekani "italipa gharama" za ziara ya Bi Pelosi.
Taiwan inajitawala, lakini China inaiona kama jimbo lililojitenga ambalo huenda likajiunga na nchi hiyo.
"Miaka arobaini na tatu iliyopita, Marekani ilitoa ahadi ya kusimama na Taiwan daima,’’ leo wajumbe wetu walikuja Taiwan ili kuweka wazi wazi kwamba hatutaacha ahadi yetu kwa Taiwan," Bi Pelosi alisema, akimaanisha Sheria ya Mahusiano ya Taiwan.

Chanzo cha picha, Getty Images
Taiwan imekuwa kitovu kingine tena huku kukiwa na mvutano mkali na maneno makali kati ya Washington na Beijing katika miaka ya hivi karibuni, huku Marekani ikishikilia mkazo wa kidiplomasia kuhusu suala hilo.
Marekani inatii sera ya "China Moja" - msingi wa uhusiano wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili ambayo inatambua serikali moja tu ya China - na ina uhusiano rasmi na Beijing na sio Taiwan. Lakini pia inadumisha uhusiano "usio rasmi" na kisiwa hicho. Hiyo ni pamoja na kuuza silaha kwa ajili ya Taiwan kujilinda.
Ziara ya Bi Pelosi inatazamwa na Beijing kama ishara nyingine ya kuunga mkono Taiwan.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini, Ikulu ya White House imekuwa ikipinga ziara hiyo, na Rais Joe Biden alikuwa amesema jeshi liliitathmini na kuona kama "si wazo zuri".
Katika mkutano wake na Bi Tsai katika ofisi ya rais, Bi Pelosi aliitaja Taiwan kuwa "msukumo kwa watu wote wanaopenda uhuru", akisema: "Ulimwengu unakabiliwa na chaguo kati ya demokrasia na uhuru. Uamuzi wa Marekani kuhifadhi demokrasia hapa Taiwan bado ni kipaumbele."
Bi Tsai vile vile alisifu ushirikiano kati ya maeneo yote mawili, akisema Taiwan imesalia "mshirika wa kuaminika na wa kutegemewa wa Marekani".
Aliongeza kuwa Taiwan "inakabiliwa na vitisho vya kijeshi vilivyoimarishwa kwa makusudi", akiongeza kuwa "haitarudi nyuma na kwamba Taiwan itafanya chochote itakachoweza kuimarisha uwezo wake wa kujilinda".
Bi Pelosi anatarajiwa kukutana na kundi la wanaharakati wa haki za binadamu baadaye siku ya Jumatano.
Hapo awali alikutana na Naibu Spika wa Bunge la Taiwan Tsai Chi-Chang.
Wakati ndege yake ilipotua Jumanne usiku, vyombo vya habari vya serikali ya China viliripoti kwamba ndege zake za kijeshi zilikuwa zikivuka mlango wa bahari wa Taiwan. Taiwan ilikanusha ripoti hizo wakati huo, lakini baadaye ilisema kuwa zaidi ya ndege 20 za kijeshi za China ziliingia katika eneo lake la ulinzi wa anga siku ya Jumanne.
Ndani ya saa moja baada ya Bi Pelosi kuwasili, China ilitangaza kwamba Jeshi la Ukombozi la Watu litafanya mfululizo wa mazoezi ya kijeshi ya angani na baharini karibu na Taiwan baadaye wiki hii , ili kuonya meli na ndege kutoingia katika baadhi ya maeneo.
Hatua hii inafuatia mvutano unaoongezeka ambapo ndege za kivita za China zilikuwa tayari zimetoka hadi kwenye mstari wa kati, mgawanyiko usio rasmi unaotenganisha China na Taiwan katika bahari kati yao.
Hatari inayoonekana ni kwamba ni ngumu kurudi nyuma.
Sasa kwa vile Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi ameweza kuzuru Taiwan - afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kufanya hivyo katika miaka 25 je, wengine hawatataka kufanya hivyo katika siku zijazo?
Sasa kwa kuwa China imefanya mazoezi makubwa ya kijeshi karibu sana na Taiwan, kwa nini isifanye hivyo tena?
Si muda mrefu uliopita, mpango wa Beijing na Taiwan ulihusisha kujiunga.
Lakini, mbinu chini ya Rais wa Uchina Xi Jinping imekuwa ya kivita zaidi, na shinikizo zaidi linatumika kwa Taipei.
'Hatutatishika'
Changamoto kubwa labda kwa utulivu wa kikanda ni kwamba msimamo wa umma wa kila mtu juu ya Taiwan ni wa kuchekesha, na unaonekana kuwa mgumu kudumisha kila uchao.
China inaifanya Taiwan kuwa kama sehemu yae neo lake kwa sasa, ingawa kisiwa hicho kinakusanya kodi yake, kura katika serikali yake, kutoa hati zake za kusafiria na ina jeshi lake.
Marekani inafanya kama haichukulii Taiwan kuwa ni nchi huru, ingawa inaiuzia silaha za hali ya juu na, mara kwa mara, mwanasiasa wa ngazi ya juu hutembelea kile kinachoonekana kama safari rasmi.
Ingawa ziara ya Bi Pelosi imekuwa mada ya uvumi mkubwa wa kimataifa kwa siku nyingi, ilikuwa imegubikwa na usiri hadi dakika ya mwisho.
Alipoanza ziara ya Asia siku ya Jumapili, hakutajwa Taiwan katika ratiba yake rasmi, ambayo ilijumuisha Singapore, Malaysia, Korea Kusini na Japan.
Lakini baada ya Bi Pelosi kutua, Bw Kirby wa Ikulu ya Marekani aliambia CNN ziara hii ilikuwa sawa na safari za awali za maafisa wengine, akiongeza kuwa "Marekani haitatishwa na vitisho".
Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi alitoa taarifa akionyesha wazi kutoridhishwa kwa nchi yake na ziara ya Bi Pelosi.
Bw Wang aliiita kama "uchokozi za wazi za kisiasa", akiongeza kuwa "inakiuka sana kanuni ya China moja na inadhuru uhuru wa China".
"Marekani inapaswa kuacha kuzuia kujiungana tena kwa China. Taiwan ni sehemu isiyoweza kutengwa ya China".
China pia ilizindua vizuizi kadhaa siku ya Jumatano, kusimamisha usafirishaji wa mchanga kwenda Taiwan na kusimamisha uagizaji wa baadhi ya matunda na samaki kutoka Taiwan.
Beijing pia inatoa shinikizo la kimataifa kwa mataifa mengine kukubali kanuni yake ya "China Moja" , kwamba kuna serikali moja tu ya China, iliyopo Beijing. Ni mataifa 15 pekee duniani ambayo yana uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Taiwan.














