Eid al-Fitr ni lini na tarehe yake inaamuliwa vipi?
Na Ahmen Khawaja, BBC

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwisho wa mwezi mtukufu wa Kiislamu wa Ramadhani huadhimishwa na sikukuu muhimu ya kidini inayojulikana kama Eid al-Fitr, ambapo familia hukutana pamoja wakiwa wamevaa nguo zao nzuri zaidi kufanya karamu. Lakini kwa tukio kubwa kama hili la kimataifa, kufahamu ni lini litatokea ni jambo gumu ajabu - kama Ahmen Khawaja anavyoelezea.
Nguvu ya Mwezi
Wakati mwisho wa Ramadhani unakaribia, Waislamu wengi karibu bilioni 1.9 duniani watakuwa na matumaini ya uwepo wa anga safi ili kuona ishara inayowaambia mwezi umeandama na kuwa ni wakati wa kuanza kwa sherehe.
Uislamu unafuata kalenda ya mwezi, kulingana na awamu za mwezi. Ramadhani huanza katika mwezi wake wa tisa.
Kila mwaka, kila mwezi wa kalenda ya mwandamo hutokea karibu siku 11 nyuma ukilinganisha na ilivyotokea mwaka uliopita.
Kufuata kalenda ya mwezi ni muhimu sana kwa Waislamu na ina athari kubwa juu ya jinsi watu wanavyopitia Ramadhani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Waislamu hufunga wakati wa Ramadhani, kujiepusha na chakula na vinywaji kuanzia alfajiri hadi machweo. Lau miezi ya Kiislamu ingeliegemezwa kwenye kalenda ya jua, ambapo misimu iliwekwa, basi watu wanaoishi katika sehemu fulani za dunia wangekuwa na Ramadhani katika majira ya joto, yenye vipindi virefu vya mchana, na katika sehemu nyingine ingekuwa majira ya baridi na mchana mfupi.
Kwa kufuata kalenda ya mwezi, kila Mwislamu hupata uzoefu wa kufunga katika misimu tofauti (na hivyo ana muda mrefu au mfupi wa kila siku wa kufunga) katika kipindi cha miaka 33 ya maisha yao.
Utata
Sikukuu ya Eid al-Fitr huangukia siku ya kwanza ya mwezi wa kumi wa Shawwal, lakini ndani ya Uislamu kuna mjadala juu ya wakati huu hasa.
Ingawa wengine hufuata kalenda iliyowekwa ya mwezi na wengine hutumia uchunguzi wa unajimu kutangaza kuonekana kwa Mwezi mpya, Waislamu wengi huadhimisha mwezi mpya baada ya Mwezi mpevu kuonekana angani.
Hii kwa kawaida hufanywa na maafisa kutoka kwa mamlaka ya Kiislamu, badala ya watu binafsi kuangalia angani wenyewe.
Eid itakuwa lini mwaka huu?
Kwa wale wanaoamua Eid kuanzia kuonekana kwa mwezi, inatarajiwa kuanza Ijumaa tarehe 21 Aprili au Jumamosi Aprili 22, kulingana na mahali ulipo duniani.
Waislamu bado watahitaji kusubiri hadi usiku kabla ya Eid kuthibitisha hili kwani miezi ya mwandamo inaweza kuwa na urefu wa siku 29 au 30, kulingana na wakati mpevu wa kwanza wa Mwezi unaweza kuonekana angani usiku.
Watafutaji wa Mwezi wa Karibu wataanza kuchanganua anga baada ya jua kutua, wakitafuta mwezi mpevu katika siku ya 29 ya mwezi popote walipo duniani.
Ikiwa wataona Mwezi mpya, sherehe za Eid zitafanyika siku inayofuata.
Ikiwa sivyo, basi siku moja zaidi ya kufunga itafanyika, kukamilisha mwezi wa siku 30.
Kulingana na HM Nautical Almanac Office ya Uingereza, Mwezi mpya unapaswa 'kuonekana kwa urahisi' kuanzia Ijumaa, 21 Aprili, kumaanisha siku ya kwanza ya Eid itakuwa siku inayofuata, Jumamosi, 22 Aprili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tarehe za Eid hazifanani kote ulimwenguni, ingawa kwa kawaida huwa ndani ya siku moja au mbili baada ya nyingine.
Kwa mfano, mamlaka nchini Saudi Arabia - taifa linalotawaliwa na Wasunni ambalo lilikuwa chimbuko la Uislamu - hutangaza kuanza na mwisho wa Ramadhani kutegemea shuhuda za watu wanaotazama mwezi kwa macho.
Waislamu katika nchi nyingine nyingi wamekuwa wakiiga mfano huo.
Lakini Iran, ambayo ina Waislamu wengi wa Shia, inatii tangazo la serikali ambalo linategemea kuutazama Mwezi kwa macho.
Na Iraq, ambayo ina Waislamu wengi wa madhehebu ya Shia na wachache wa Sunni, inatumia mchanganyiko wa mawili hayo - Shia hufuata tangazo la kiongozi mashuhuri Ayatollah Ali al-Sistani, huku Wasunni walio wachache wakiwafuata maulama wao wenyewe.
Uturuki, wakati huo huo - nchi ambayo sio ya kidini - hutumia hesabu za unajimu kuamua mwanzo na mwisho wa Ramadhani.
Na huko Ulaya, Waislamu wengi husubiri matangazo ya viongozi wa jumuiya zao - ingawa hii inaweza kutegemea kuutazama mwezi katika nchi nyingine za Kiislamu.














