Vita vya kwanza vya ndege zisizo na rubani duniani, sura mpya katika mzozo wa India na Pakistan

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images
Vita vya kwanza vya droni duniani vilizuka kati ya majirani wawili wenye silaha za nyuklia huko Asia Kusini.
Alhamisi iliyopita, India iliishutumu Pakistan kwa kurusha wimbi la ndege zisizo na rubani na makombora katika kambi tatu za kijeshi katika eneo la India na eneo linalodhibitiwa na India la Kashmir, mashtaka ambayo Islamabad ilikanusha haraka.
Pakistan, kwa upande wake, ilidai kuangusha ndege 25 za India, lakini Delhi imekaa kimya rasmi juu ya suala hilo. Wataalamu wanasema mashambulizi ya kulipiza kisasi yanaashiria mwanzo wa awamu mpya na hatari katika uhasama wa muda mrefu wa nchi hizo mbili, ambapo pande hizo mbili zinashambuliana kuvuka mpaka usio na utulivu sio tu kwa vifaru bali pia kupitia silaha zisizo na rubani.
Wakati Marekani na mataifa mengine yenye nguvu duniani yametoa wito wa kujizuia kwa pande zote mbili, eneo hilo liko kwenye ukingo wa mvutano usio na kifani, ambapo ndege zisizo na rubani - zinazohudumu kimya kimya na zisizoonekana - zimefungua ukurasa mpya katika mzozo wa India na Pakistan.
Nchi hizo mbili zilitangaza kusitisha mapigano lakini hivi karibuni zilishutumu kila mmoja kwa kukiuka

Chanzo cha picha, Getty Images
"Mzozo wa India na Pakistan umeingia katika enzi mpya ya vita vya ndege zisizo na rubani, ambapo 'macho yasiyoonekana' na usahihi wa silaha zisizo na rubani zinaweza kuamua kiwango cha mvutano au kujizuia," Jahara Matisik, profesa katika Chuo cha Vita vya Majini cha Marekani, aliiambia BBC.
"Katika anga yenye changamoto za Asia Kusini, yeyote atakayefanikisha ustadi kamili katika vita vya ndege zisizo na rubani hatafuatilia tu uwanja wa vita, bali kuutengeneza upya."
India imesisitiza kuwa shambulio lake la kombora lilikuwa kujibu shambulio baya lililofanywa na makundi ya wanamgambo dhidi ya watalii wa India katika eneo la Pahalgam mwezi uliopita, lakini Islamabad inakanusha kuhusika na shambulio hilo.
Jeshi la Pakistani lilisema siku ya Alhamisi kuwa limeangusha ndege 25 zisizo na rubani za India katika miji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Karachi, Lahore na Rawalpindi.
Ndege hizo zisizo na rubani zilisemekana kuwa aina ya Harpoon zilizotengenezwa na Israel na zilinaswa na kuharibiwa kwa kutumia njia za kiufundi na silaha.
Wakati huo huo, India ilidai kuwa imezima rada kadhaa za Pakistani na mifumo ya ulinzi wa anga, pamoja na Lahore, madai ambayo Islamabad inakanusha.

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Makombora na mabomu yanayoongozwa na teknolojia ya leza, ndege zisizo na rubani zimekuwa sehemu muhimu ya vita vya kisasa, na kuongeza kwa kiasi kikubwa usahihi na ufanisi wa operesheni za kijeshi.
Zana hizi zinaweza kusambaza viwianishi vinavyolengwa kwa mapigo ya anga au, ikiwa vimewekwa, vitambulishe moja kwa moja lengo kwa kutumia leza, hivyo kuruhusu ushiriki wa haraka.
Ndege zisizo na rubani pia zinaweza kutumika kuhadaa adui au kukandamiza mifumo ya ulinzi wa anga.
Kwa kuingia katika maeneo yaliyofunikwa na adui, huwasha mifumo yake ya rada na kuwezesha silaha zingine, kama vile ndege zisizo na rubani au makombora ya kuzuia rada, kuwalenga.
"Ukraine na Urusi zinatumia njia hiyohiyo katika vita vyao," kulingana na Bw. Matysek. "Jukumu hili la pande mbili - kulenga na kufanya uchochezi - limefanya ndege zisizo na rubani kuzidisha nguvu kwa ajili ya kudhoofisha ulinzi wa anga wa adui bila kuhatarisha ndege za abiria."
Wataalamu wanasema ndege za India zisizo na rubani zimelinganishwa zaidi na ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Israeli kama vile IAI Searcher na Heron, pamoja na zana za kivita kama vile Harpy na Harop, ambazo pia ni makombora na yana uwezo wa kufanya upelelezi wa kujitegemea na mashambulizi ya usahihi.
Silaha za Hasa, Harop, wataalam wanasema, zinaashiria mabadiliko kuelekea vita kwa malengo ya kimkakati na ulengaji sahihi sana, mabadiliko ambayo yanaonyesha umuhimu unaoongezeka wa kutengeneza silaha katika vita vya kisasa.
Kulingana na wataalamu, ndege isiyo na rubani ya Heron ni "macho ya India ya angani" kwa ufuatiliaji wa wakati wa amani na operesheni za kijeshi za wakati wa vita.
Droni ya Searcher Mk2 umeundwa kwa ajili ya shughuli za kijeshi za mstari wa mbele na ina uwezo wa kustahimili angani kwa saa 18, ina uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 300 na kuwa juu angani zaididya urefu wa mita 7,000.
Huku wengi wakiwa wanaamini kwamba ndege zisizo na rubani za India bado "zina kikomo," makubaliano ya hivi karibuni ya nchi hiyo yenye thamani ya dola bilioni 4 na Marekani kununua ndege zisizo na rubani 31 za MQ-9B, ambazo zinaweza kuruka kwa saa 40 na kupanda hadi urefu wa futi 40,000, ni hatua kubwa katika uwezo wake.
Kulingana na wataalamu, India pia inaunda mikakati inayohusiana na "vikundi vya ndege zisizo na rubani," matumizi ya idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani ili kuvuruga na kueneza mifumo ya ulinzi wa anga ya adui na kuwezesha kupenya kwa silaha kwa ufanisi zaidi.
Ijaz Haider, mchambuzi wa masuala ya ulinzi kutoka Lahore, aliiambia BBC kwamba ndege zisizo na rubani za Pakistan ni "kubwa na za aina mbalimbali," ikiwa ni pamoja na mifumo ya kiasili na iliyoagizwa kutoka nje.
Anasema hesabu ya sasa inajumuisha "zaidi ya ndege elfu moja," ikiwa ni pamoja na mifano kutoka China, Uturuki na wazalishaji wa ndani. Mifumo mashuhuri ni pamoja na ndege zisizo na rubani za CH-4 za Uchina, zile za Uturuki yz Akinci, na ndege za kiasili za Pakistani, zikiwemo Buraq na Shahpar. Pakistan pia imejiundia silaha zake hatua ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa kijeshi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ijaz Haider anasema Jeshi la Anga la Pakistan limekuwa likianzisha mifumo isiyo na rubani katika operesheni kwa karibu muongo mmoja sasa. Moja ya maeneo makuu ya kuzingatia ni hatua zilizopigwa kwa ndege zisizo na rubani za wingmen drones zilizoundwa kufanya kazi moja kwa moja na ndege za kivita.
Bw. Matisik anaamini: "Msaada wa kiufundi wa Israel, hasa katika utoaji wa ndege zisizo na rubani za Harpoon na Heron, umekuwa na jukumu muhimu katika kuimarisha uwezo wa ndege zisizo na rubani za India, huku utegemezi wa Pakistan kwenye mifumo iliyotengenezwa na Uturuki na China unaonyesha kuendelea kwa mbio za silaha katika eneo hilo."
Wakati mashambulizi ya hivi majuzi ya India na Pakistan ni ishara ya kuongezeka kwa hali ya wasiwasi na ushindani kati ya nchi hizo mbili, wataalamu wanasema migogoro hii ni tofauti sana na vita vya ndege zisizo na rubani katika mzozo wa Russia na Ukraine, vita ambavyo ndege zisizo na rubani zimekuwa kitovu cha operesheni za kijeshi, huku pande zote mbili zikitumia maelfu ya ndege hizo za rubani kwa uchunguzi, kulenga na mashambulizi ya moja kwa moja.
"Kutumia ndege zisizo na rubani badala ya ndege za kivita au makombora mazito kunaweza kupendekeza njia nyepesi katika kukabiliana na jeshi," mchambuzi wa masuala ya ulinzi wa India Manoj Joshi aliambia BBC.
"Kwa kuwa ndege zisizo na rubani zina nguvu ndogo ya uharibifu kuliko ndege zinazoendeshwa na watu, hii inaweza kuonekana kama aina ya kuzuia. Lakini ikiwa hii ni utangulizi wa shambulio kubwa la anga, basi kila kitu kitabadilika kabisa.
Wataalamu wanasema kwamba ingawa ndege zisizo na rubani zimebadilisha uwanja wa vita nchini Ukraine, jukumu lao katika mzozo wa India na Pakistan bado ni mdogo na kwa kiasi kikubwa ni ishara. Nchi zote mbili zinaendelea kutumia vikosi vyao vya anga kurushiana makombora.
"Vita vya ndege zisizo na rubani tunazoshuhudia sasa huenda visidumu kwa muda mrefu na vinaweza kuwa mwanzo tu wa mzozo mkubwa," anasema Manoj Joshi.
End of Pia unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












