Kwa nini kuzuia shambulio la Iran ni mafanikio makubwa kwa Israeli?

RFVC

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Picha ya ndege ya kivita ya Israel ya F-15 baada ya misheni ya kuzuia shambulio la Iran

Inaonekana kwamba vita vya chini chini kati ya Israel na Iran vimemalizika, kwa mujibu wa magazeti ya kimataifa, baada ya jibu la moja kwa moja, na la kwanza la Iran dhidi ya Israel.

Gazeti la Haaretz linasema katika uchambuzi uliochapishwa Jumapili na mwandishi Amos Harel anasema Israel kuweza kuzuia shambulio hilo ni mafanikio makubwa.

Katika makala aliyoiita, "Kuzuia shambulio la Iran ni mafanikio makubwa ya Israel, na kulipiza kisasi kunaweza kuhatarisha vita vya kikanda.’’

Harel anaamini jibu la Israel "linaweza kusababisha jibu kutoka kwa Hezbollah na kuziingiza pande nyingi katika vita vya kikanda."

Ndani ya siku chache, dalili zilionekana kwamba Iran inapanga jibu kali lililozinduliwa kutoka katika ardhi yake dhidi ya Israel, na suala hilo halikuhitaji kazi yoyote ya kijasusi.

Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei, alisema hadharani mara tatu kwamba Iran itaishambulia Israel baada ya ubalozi wake mdogo Syria Damascus kushambuliwa.

Iran ilirusha zaidi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya aina mbalimbali 300, bila mafanikio kwani ni idadi ndogo ya makombora ya balestiki ndio yalitua katika maeneo ya wazi, huko Negev kusini mwa Israel, na kumjeruhi msichana mdogo.

Israel ilifaulu kwa asilimia 99 katika kuzuia mashambulizi hayo, na ilinasa sehemu kubwa ya mashambulizi hayo nje ya eneo la Israel, katika anga ya Jordan na Iraq.

Harel pia alizungumzia mpango wa kuunda mwavuli wa ulinzi dhidi ya ndege zisizo na rubani na makombora kwa ushirikiano na nchi za Ulaya na nchi za Kissuni.

Katika kipindi chote cha miezi sita ya vita, viashiria mbalimbali vimejitokeza juu ya uwepo wa mfumo wa ulinzi wa kikanda, ambao Wamarekani waliuita MEAD (Muungano wa Ulinzi wa Anga wa Mashariki ya Kati).”

Hakuna shaka kwamba Baraza la Mawaziri na katika serikali ya Israel linaona sasa ni fursa imekuja ya kubadili hali ya mambo kwa kuharibu safu ya silaha za Hezbollah na makundi mengine ya Iran.

Hata hivyo, Washington inaitaka Israel isijibu, kulingana na ripoti za vyombo vya habari, Rais Joe Biden wa Marekani anajaribu kumtuliza Netanyahu kwa kusema, "ridhika na ushindi ulioupata."

Gazeti la Washington Post

trg

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Iran ilifanya mashambulizi dhidi ya Israel, Aprili 14, 2024
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Gazeti la Washington Post linachambua hatari zinazoweza kujitokeza baada ya shambulio la moja kwa moja la Iran dhidi ya Israel, ambalo ni kujibu shambulio la Israel mwezi huu kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.

Shambulio lililosababisha mauaji ya wanachama wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, akiwemo kamanda mkuu Mohammad Reza Zahedi na Mohammad Hadi Haj Rahimi.”

Israel imefanya mashambulio nchini Syria dhidi ya Iran na washirika wake kwa miaka, na katika kampeni yake ya kijeshi ya miezi sita dhidi ya Hamas huko Gaza, lakini shambulio la Aprili 1 lilikuwa tofauti.

Gazeti linafichua kwamba maafisa wa Marekani wana wasiwasi kuhusu kuzuka kwa vita vya pande nyingi, na wanahofia mgogoro utasababisha mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Marekani walioko Iraq, Syria, au maeneo mengine ya Mashariki ya Kati."

Gazeti hilo pia linasema "maafisa watatu wa Marekani walizungumza kwa sharti la kutotajwa majina kwamba Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin na maafisa wengine wakuu wa ulinzi wanaamini Israel ilipaswa kuwajulisha mapema kuhusu shambulio la ubalozi.

Uwezo wa makombora ya Iran

rgfbv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Mabaki ya kombora la Iran katika ardhi ya Israel

Baada ya jibu la Iran kwa Israel, gazeti la Al-Quds Al-Arabi lilizungumza kuhusu uwezo wa makombora ya Iran, na kubainisha kwamba "makombora ya balistiki ni sehemu muhimu ya silaha za Tehran, na Ujasusi wa Marekani ulisema vivo hivyo."

Gazeti la Al-Quds Al-Arabi, linasema Iran "ilitengeneza droni yenye uwezo mkubwa inayoitwa (Mohajer-10), inayoruka hadi kilomita 2,000 na kukaa juu hadi saa 24, na kubeba hadi kilo 300 za vilipuzi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na maafisa wa Iran, makombora ya balistiki ya Tehran ni "silaha muhimu za kuzuia na kulipiza kisasi dhidi ya Marekani, Israel, na shabaha zingine zinazowezekana za kikanda."

Gazeti hilo linasema, likinukuu vyombo vya habari vya Iran, makombora tisa ya Iran yana uwezo wa kufika Israel, na makombora mashuhuri zaidi kati ya hayo ni "Sejil," ambalo linaweza kuruka kwa kasi ya zaidi ya kilomita 17,000 kwa saa.

Jengine ni "Khaybar" ambalo linaweza kuruka umbali wa kilomita hadi 2,500, na "Haj Qasim" ambalo linaruka hadi kilomita 1,400, na limepewa jina la Kamanda wa Kikosi cha Quds Qassem Soleimani, ambaye aliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani mjini Baghdad miaka minne iliyopita.

Programu ya makombora ya Iran kwa kiasi kikubwa inategemea miundo ya Korea Kaskazini na Urusi na imefaidika na usaidizi wa China."

Kulingana na gazeti hilo makombora ya masafa mafupi na ya kati za Iran ni pamoja na Shahab-1, ambayo yanakadiriwa kufika umbali wa kilomita 300, Zulfiqar kilomita 700, Shahab-3 kilomita 800-1000 km, na Imad-1 linafika kilomita 1,000 na Sejil kilomita 1500-2500.

Gazeti hilo limeongeza kuwa: "Licha ya upinzani kutoka Marekani na Ulaya, Jamhuri ya Kiislamu inasema itaendelea kuendeleza mpango wake wa makombora ya kujihami."