Je, Wahouthi wanaitumbukiza Marekani na washirika wake kwenye vita wasivyoweza kushinda?

cx

Chanzo cha picha, US DEPARTMENT OF DEFENSE

    • Author, Céline Guerret & Kate Forbes
    • Nafasi, BBC

Hakuna ushindi rahisi kwa muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani, Uingereza, Australia, Bahrain, Canada na Uholanzi, ambao unalenga kuharibu uwezo wa kijeshi wa Wahouthi huko Yemen ili kulinda meli katika Bahari ya Shamu.

Kundi la Houthi linaloungwa mkono kifedha na kijeshi na Iran, limefanya mashambulizi zaidi ya thelathini dhidi ya meli za kimataifa na kibiashara katika Bahari ya Shamu tangu katikati ya mwezi wa Novemba, na hakuna dalili ya kumalizika kwa mashambulizi hayo.

Kwa upande wa Marekani, maafisa wa ulinzi pia wanaonekana kuwa imara na wamedhamiria kutekeleza malengo ya muungano huo, kama walivyosema katika mkutano na waandishi wa habari Januari 23:

"Tuko tayari kuchukua hatua zaidi za kupunguza vitisho au kujibu mashambulizi, na kuhakikisha utulivu na usalama wa eneo la Bahari ya Shamu na njia za biashara ya Kimataifa".

Mashambulizi ya Wahouthi yalivuruga usafiri wa meli duniani na kuzidisha hofu kwamba madhara ya vita kati ya Israel na Hamas yatavuruga Mashariki ya Kati.

Je, Marekani inaweza kushinda kundi ambalo muungano wa nchi kadhaa unaoongozwa na Ufalme wa Saudi Arabia umeendesha vita - bila mafanikio - kwa karibu muongo mmoja?

Nchi jirani ya Saudi Arabia hivi karibuni imenyamaza kimya juu ya kile kinachotokea katika Bahari ya Shamu, kwani mazungumzo ya amani yanaendelea kati yake na Houthis.

Kabla ya mashambulio ya hivi karibuni, yaliyofanywa na Marekani na Uingereza kwenye maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Wahouthi, juhudi za kidiplomasia za kimataifa zilijaribu kutuliza hali ya mambo katika eneo hilo, lakini Wahouthi walikata.

Mjumbe maalumu wa Marekani kwa Yemen, Tim Lenderking, alisema: "Inasikitisha kwamba suala hilo limefikia kiwango hiki."

Unaweza pia kusoma

Je, vikosi vya Houthi vina uwezo gani?

fdvc

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Mpiganaji wa Houthi akiwa amebeba mizinga kwenye lori wakati wa maandamano ya kulaani mashambulizi yanayoongozwa na Marekani dhidi ya Ansar Allah na kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Iran inalipa kundi la Houthi silaha na kulisaidia kifedha. Lakini Wahouthi hawako chini ya udhibiti wa moja kwa moja wa Tehran.

Kundi la Houthi limeonyesha linaweza kukabiliana na jeshi la muungano wa Saudi Arabia. Limebadilika kutoka kundi dogo hadi kuwa kikosi cha kikubwa kilichofunzwa chenye vifaa vya kisasa, ikiwa ni pamoja na helikopta, makombora na ndege zisizo na rubani.

Ingawa Wahouthi waliweza kupambana na Saudia, kukabiliana na Marekani na washirika wa kimataifa ni suala tofauti kabisa. Nguvu zao, mkakati, na uzoefu wao pamoja ni mkubwa zaidi kuliko ule wa Wasaudi.

"Tuna nguvu nyingi, na tunapaswa kuzitumia kwa kiasi fulani kwa hekima," Stephen Cook, anasema afisa katika Kituo cha Eni Enrico Mattei cha Mafunzo ya Mashariki ya Kati na Afrika katika Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Marekani, alisema. "

Vitakuwa vita vya muda mrefu?

C

Chanzo cha picha, UK/REUTERS

Maelezo ya picha, Meli ya Uingereza "HMS Diamond" yarusha makombora baada ya kuongezeka kwa mashambulizi ya Houthi kwenye njia ya kimataifa ya meli.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Inawezekana operesheni hii itakuwa kubwa.'' Anasema Afisa wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Marekani James J. Foggo, ambaye pia aliwahi kuwa kamanda wa zamani wa Vikosi vya Wanamaji vya Marekani barani Ulaya na Afrika.

''Ni swali ambalo utawala wa Marekani haujaweza kulisema hadharani. Lakini nina uhakika wanalizungumzia."

Foggo anakumbuka mashambulizi ya 1980 na 1988 katika Ghuba ya Uajemi, ambapo Marekani ilishambulia Jeshi la Wanamaji la Iran, baada ya Wairani kushambulia meli za meli.

Admiral Foggo pia anakumbuka shambulio dhidi ya meli ya kivita ya Marekani, nchini Yemen mnamo Oktoba 2000, na kusababisha kifo cha mabaharia kumi na saba wa Marekani.

Ingawa shambulio hilo lilihusishwa na Al-Qaeda, hakukuwa na jibu la kijeshi dhidi ya shirika hilo wakati huo. Alijiuliza: "Ni nini kilitokea mwaka mmoja baadaye? Mashambulizi ya Septemba 11 yalitokea Marekani, na kuthibitisha kwamba hatua za kijeshi zilipaswa kuchukuliwa."

Stephen Cook anasema: “Uhuru wa usafiri wa majini ni jambo la msingi sana kwa Marekani, na kuruhusu kikundi kama hiki kupata mamlaka kama hiyo katika eneo hili ni hatari sana.”

Ni vita visivyokuwa na mshindi?

V C

Chanzo cha picha, SUEZ CANAL AUTHORITY OFISI / EPA

Maelezo ya picha, Meli ya kubeba mizigo ya Zophia inayomilikiwa na Ugiriki huko Ismailia, Misri Januari 22 inafanyiwa ukarabati baada ya uharibifu uliosababishwa na shambulio la kombora la Houthi.

Mkakati wa Rais wa Marekani Joe Biden kuhusu Yemen unalenga kuwadhoofisha wanamgambo wa Houthi, lakini haitaki kujaribu kulishinda kundi hilo au kukabiliana na Iran moja kwa moja, kulingana na wataalamu.

Mkakati huu - una mchanganyiko wa mashambulizi machache ya kijeshi na vikwazo - inaonekana kulenga kuwaadhibu Wahouthi, huku ikijaribu kupunguza hatari ya mzozo mpana zaidi katika Mashariki ya Kati.

"Sidhani kama misheni hii inalenga kuwaangamiza Wahouthi, au kurudisha serikali ya Yemen madarakani," anasema Brian Carter wa Taasisi ya American Enterprise.

Anaongeza: "Ninaamini operesheni hii inalenga kudhoofisha uwezo wa jeshi la Wahouthi na kuwazuia kushambulia meli za kimataifa katika Bahari ya Shamu. Kudhoofisha mifumo ya kijeshi sio kazi isiyoweza kushindwa. Ni lengo la kijeshi linaloweza kufikiwa."

Mjumbe maalum wa Marekani nchini Yemen, Tim Lenderking, alithibitisha kwamba "suala hilo ni kuvuruga tu uwezo wa Wahouthi wa kushambulia meli."

Pentagon inasema imeharibu zaidi ya vituo 25 vya kurushia makombora tangu Marekani ilipoanza kushambulia maeneo ya kijeshi ya Wahouthi nchini Yemen mnamo Januari 11.

Pentagon inaongeza kuwa ilipiga pia droni, rada za pwani, na vifaa vya uchunguzi wa anga vya Wahouthi, pamoja na maeneo ya kuhifadhi silaha.

Je, mzozo huo utawapa Wahouthi umaarufu zaidi?

X

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Waasi wa Houthi waliandamana kulaani mashambulio ya anga yanayoongozwa na Marekani na kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Tim Lenderking anasema Wahouthi wanaweza kutaka kujihusisha na vita hivi kama njia ya kuwaonyesha watu wa Yemen kwamba wanasimama sio tu na watu wa Palestina, lakini pia dhidi ya Magharibi.

Frank Gardner, mwandishi wa usalama wa BBC, anasema Wahouthi sasa wanajulikana sana katika ulimwengu wa Kiarabu, kwa sababu wanaunga mkono Hamas kama sehemu ya "mhimili wa upinzani" unaoungwa mkono na Iran dhidi ya Israel.

Ujasusi wa Magharibi hivi karibuni ulikadiria kuwa angalau asilimia 30 ya makombora ya Wahouthi yaliharibiwa. Hata hivyo, Wahouthi huenda wakaendeleza mashambulizi yao dhidi ya meli wanazoshuku kuwa na uhusiano na Israel, Marekani, au Uingereza.

Hisham Al-Omeisy, mshauri mkuu wa Yemen katika Taasisi ya Amani ya Ulaya, anasema watu wengi wanaweza wasitambue kwamba Wahouthi wana malengo yao wenyewe, kando na kuunga mkono Gaza.

"Itakuwa ni kutoona mbali bila kuzingatia athari za kijamii na kisiasa na za ndani ambazo zinaimarisha na kuchochea hisia za upinzani dhidi ya Marekani na Uingereza.''