Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, chama cha ANC kitaathiriwa na kujiondoa kwa Jacob Zuma?
Licha ya kuwa rais wa zamani aliyehangaishwa na kupelekwa jela, Jacob Zuma anageuka kuwa mwanasiasa asiyetabirika katika kampeni za uchaguzi nchini Afrika Kusini.
Hii inafuatia uamuzi wake wa kukihama chama tawala cha African National Congress (ANC) na kujiunga na chama kipya cha Umkhonto we Sizwe, kumaanisha Spear of the Nation.
Zuma mwenye umri wa miaka 81 anaongoza kampeni zake katika uchaguzi mkuu wa Mei 29, akiwataka watu kukipa kisogo chama cha ANC kinachoongozwa na mrithi wake, Rais Cyril Ramaphosa.
"Zuma hataki mamlaka, lakini kujiinua katika ANC. Anataka kumng'oa Ramaphosa ili apate kiongozi anayekubalika zaidi," mchambuzi wa kisiasa Richard Calland aliambia BBC.
Kura mbili za maoni za hivi punde zaidi zinaonyesha kuwa chama cha Zuma - kinachojulikana kwa kifupi cha MK – kinapata ushawishi mkubwa, kwa kupata karibu asilimia 13 ya kura za kitaifa na asilimia 25 katika ngome ya kisiasa ya rais huyo wa zamani ya KwaZulu-Natal.
Lakini Angelo Fick, mkurugenzi wa utafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Kijamii na Kiuchumi ya Auwal mjini Johannesburg, anaamini kuwa chama hicho kitapata kura chache, hasa katika kura ya bunge la taifa.
"Nitashangaa ikiwa kitapata asilimia 6," aliambia BBC
Ili kuunga mkono maoni yake, alitoa mfano wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) katika uchaguzi wa kwanza kilichoshiriki baada ya kiongozi wa vijana wa ANC aliyefukuzwa Julius Malema kuunda chama hicho.
Bw Malema alichukua sehemu kubwa ya wanachama wa vijana wa ANC kwenda EFF, lakini chama hicho kilipata asilimia 6 tu ya kura za kitaifa mnamo 2014, na asilimia 11 mnamo 2019.
"Chama cha MK ni dhaifu sana kuliko EFF ilivyokuwa 2014," Bw Fick alisema.
Prof Calland alisema Bw Zuma alikuwa ufunguo wa chama kupata kura.
"Ana haiba fulani na mvuto wa watu wengi. Bado ana uaminifu, hasa miongoni mwa watu wa KwaZulu-Natal," aliongeza.
Chama cha MK kinatarajia kushikilia mizani ya madaraka, hasa huku kura za maoni mbalimbali zikionyesha kuwa ANC inaweza kupoteza wingi wake wa moja kwa moja katika bunge la taifa kwa mara ya kwanza tangu kilipochukua mamlaka mwishoni mwa utawala wa wazungu wachache miongo mitatu iliyopita.
"Wakati Zuma alipokuwa katika ANC, KwaZulu-Natal ikawa jimbo kubwa na lenye ushawishi mkubwa zaidi katika chama. Ilisaidia ANC kuvuka mstari wa asilimia 50 katika kila uchaguzi wa kitaifa tangu 2004," aliiambia BBC.
Hapo awali, ANC ilipuuza kuundwa kwa chama cha MK lakini baada ya Bw Zuma kuweka uzito wake nyuma yake mwezi Desemba, chama hicho kilianzisha hatua za kisheria katika mahakama ya uchaguzi kukifutia usajili na kukizuia kushiriki.
Pia inataka Mahakama Kuu kukizuia kutumia jina la MK, ikisema kuwa ANC ina hakimiliki yake.
Vita juu ya jina hilo ni muhimu, kwani MK inarejelea mrengo wa ANC ambao Nelson Mandela alianzisha mnamo 1961 kupigana na mfumo wa ubaguzi wa rangi.
Kwa hivyo, ina ishara kubwa ya kisiasa, na ANC imedhamiria kumzuia Bw Zuma - ambaye alijiunga na mapambano ya kijeshi ya ANC akiwa kijana.
Mzozo mwingine unaendelea kuhusu iwapo Bw Zuma anastahili kuhudumu kama mbunge kwa vile alipatikana na hatia ya kudharau mahakama, na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mwaka wa 2021, kwa kukataa kushirikiana na uchunguzi ulioongozwa na jaji kuhusu ufisadi wakati wa miaka tisa ya urais wake.
Bw Zuma pia anakabiliwa na mashtaka 16 ya ufisadi kuhusu mkataba wa mabilioni ya dola, katika kesi ambayo imeendelea kwa miaka mingi huku rais huyo wa zamani akipinga majaribio ya upande wa mashtaka kumfungulia mashtaka.
Chama cha MK kimemweka Bw Zuma katika orodha ya kwanza ya wagombea ubunge, licha ya kwamba Tume Huru ya Uchaguzi ilisema mwezi Januari kwamba kuhukumiwa kwake kulimuondoa.
Bw Harper alisema alitarajia Bw Zuma kubaki uso wa umma wa kampeni za chama cha MK - hata kama atazuiwa kuwania ubunge.
Binti ya Bw Zuma, Duduzile Zuma-Sambudla, pia ameteuliwa kuwa mgombea ubunge na chama cha MK, na kupendekeza kuwa rais huyo wa zamani anamwona kama mrithi wake wa kisiasa na mlezi wa urithi wake.
Mnamo Desemba, ndiye aliyesoma taarifa kwa niaba ya babake akitangaza kwamba alikuwa ameegemea chama cha MK.
Taarifa hiyo ilimtaja Bw Ramaphosa kama "mshirika" wa "maslahi ya kibepari wazungu".
Ilionyesha chuki kubwa ya kisiasa ambayo Bw Zuma anayo kwa Bw Ramaphosa.
Raia wengi wa Afrika Kusini wanatumai kwamba haitasababisha wimbi jipya la ghasia, huku wanaume hao wawili wakichuana kutafuta kura katika uchaguzi huo.
Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhaririwa na Ambia Hirsi