Khuda Baksh: Mchawi aliyesoma vitabu akiwa amefunikwa macho

trfgv

Chanzo cha picha, BRITISH PATH

Maelezo ya picha, Aliweza kuandika na kusoma hata akiwa amefumbwa macho

Haishangazi ikiwa mwanaume atapita na baiskeli katikati ya mtaa uliojaa watu. Lakini mtu huyohuyo akipita akiwa amefumba macho na pua zake tu ndio ziko wazi kwa ajili ya kupumua, watu watashangaa.

Mmoja wa waendesha baiskeli wa aina hiyo alikuwa Kuda Baksh au Khuda Baksh. Alizaliwa mwaka 1905 huko Kashmir na akawa maarufu kwa kazi hii ya kuendesha baiskeli kwenye barabara za Uingereza na Ulaya katika miaka ya 1930 na 40.

Alidai aliweza kufanya hivyo kwa sababu aliona bila macho.

Alikuwa akionyesha kazi zake za kichawi kwa jina la 'mtu mwenye macho ya X-ray'. Kwa mtindo wake wa kipekee angeshangaza watu kwa kusoma kifungu kutoka kwenye kitabu huku macho yakiwa hayaoni na kuingiza uzi kwenye sindano.

Khuda Bakhsh amevistaajabisha vizazi vingi kwa uwezo wake. Pia iliripotiwa kuwa ndiye mhusika wa hadithi ya Roald Dahl ya 1977 ''The Wonderful Story of Henry Sugar', ambayo sasa imebadilishwa kuwa filamu na Wes Anderson.

Safari ya Kujifunza Uchawi

thgb

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Jina lake halisi ni Kuda Baksh au Khudah Bukhsh. Alizaliwa katika familia tajiri. Katika mahojiano ya 1952, alisema alivutiwa na uchawi wa mchawi wa Kihindi aliyejulikana kama Profesa Moore.

Siku mbili baada ya kuona uchawi wake, alitoroka nyumbani kwao akiwa na umri wa miaka kumi na tatu.

Alifika Lahore kutoka Kashmir ili kuwa mfuasi wa Moore. Baada ya miaka kadhaa, alisafiri hadi Burma (Myanmar), Ceylon (Sri Lanka) na Bombay (Mumbai) na kujifunza uchawi kutoka kwa wachawi, wasanii wa yoga na wana mazingaombwe.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Pia, alibadilisha jina lake kuwa Profesa KB Duke na kisha akarudisha jina la Khudah Bukhsh. Mwandishi John Zubrzycki ameandika mambo kadhaa katika kitabu chake 'Empire of Enchantment: The Story of Indian Magic.'

Mei 1935, alifika Uingereza, ambapo wachawi kutoka ulimwengu wa Mashariki walikuwa wakihitajika. Watu walitaka kuona kazi yake.

Zubrzycki aliambia BBC - wakati huo India ilionekana kuwa nchi ya uchawi. Yalikuwa ni maoni kutoka kwa maandishi ya watalii, wamishonari, wafanyabiashara na wanahistoria waliotembelea India.

Wachawi wengi wa Kihindi wamefaidika kwa sababu nchi za Magharibi zilipenda mambo ya kichawi. Na Kuda Baksh alikuwa mmoja wao. Ingawa alivaa kama Mwingereza.

Mwanahistoria John Booth, akiandika kuhusu Bakhsh katika kitabu cha The Linking Ring, anamtaja kama, "mtu wa ajabu kutoka bara la India ambaye alikuwa akiendesha baiskeli huko Paris akiwa amefumba macho."

Huko Uingereza, Kuda Baksh alipata umaarufu haraka kwa mchezo wake wa 'X-ray eyes.' Alivutia watu ambao hawakuamini uchawi wake na walipima ukweli wa uwezo wake.

Uchawi wake Wajaribiwa

dfc

Chanzo cha picha, CAITLYN RENEE MILLER

'Mwindaji mizimu' maarufu wa Uingereza Harry Price, pamoja na timu ya madaktari, waliyapima madai ya Kuda Baksh ya maono ya X-ray mnamo Julai 1935.

Zubrzycki anaandika katika kitabu chake Harry Price alifika akiwa na pamba, mkanda wa kufungia, na bandeji nene na nzito.

Kuda Baksh aliposoma kwa mafanikio sehemu ya kitabu baada ya kufunikwa macho na Price, daktari aliyafunika tena macho ya Baksh. Kuda Baksh aliweza kusoma maandishi yaliyoandikwa kwa mkono ambayo yaliwekwa kwenye meza nyuma yake.

Septemba 1935, Price alimpima tena Kuda Baksh, tukio lililomletea umaarufu zaidi nchini Uingereza na sehemu kubwa ya Ulaya.

Kuda Baksh alifanya onyesho la kutembea kwenye moto katika eneo la mashambani la Surrey. Lilikuwa tukio la kwanza la aina hiyo huko England. Alifanya onyesho hilo mbele ya madaktari, wanasaikolojia na waandishi wa habari.

Watahini walimchunguza Kuda Bakhsh kwa kila kipengele na hata kabla na baada ya kupita kwenye moto, walichunguza miguu yake na nyayo zake ili kuona kama alikuwa amevaa kitu chochote cha kudanganya.

Shimo lilichimbwa na kujazwa kuni, mkaa, mafuta ya taa na mabaki ya magazeti na kuchomwa moto. Baada ya saa chache shimo likawa linawaka moto.

Kuda Baksh alitembea na kuvuka shimo la moto - si mara moja bali mara nne. Price ameandika katika kitabu chake 'Confessions of a Ghost Hunter' kwamba hapakuwa na chembe ya malengelenge kwenye miguu yake.

Baada ya siku tisa, mbele ya watu wengine, Kuda Baksh alivuka tena shimo la moto akiwa hana viatu, moto ambao hata chuma kingewaka na kuyeyuka, lakini safari hii pia miguu ya Kuda Baksh ilibaki salama.

Zubrzycki anaandika kitendo hiki kilipelekea akili ya Price kudhani kwamba kulikuwa na uhusiano usiojulikana kati ya nguvu za kimwili na kiakili ambazo zilimlinda kutokana na majeraha.

Mazoezi ya kukazia kitu macho

refdvc

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Khuda Baksh akitembea juu ya moto

Katika mahojiano Baksh alidai, uwezo wake wa ndani wa kuona unamsaidia kuwa na maono ya X-ray. Alipata elimu hii kupitia mazoezi ya yoga - alijifunza akiwa na umri mdogo sana.

Kuangalia sehemu moja kwa muda mrefu, mfano katika mshumaa hadi kila kitu kilichokuwa karibu yake kinapotea na kuweza kuiona kabisa sura ya mtu aliyempenda zaidi. Alikuwa anafanya hivyo.

Baada ya kufanya mazoezi na mishumaa kila usiku kwa miaka kadhaa, Kuda Bakhsh alitambua akiwa na umri wa miaka 24 kwamba kama akifumba macho yake na kukazia sana kitu fulani, "ningeweza kuona kitu nikitakacho."

Alisema alipokuwa na umri wa miaka 28, aliweza kusoma kitabu akiwa amefumba macho.

Mchawi Bill Larson aliandika katika makala kwenye jarida la 'Genie,' maelfu ya watu walikuja kutazama maonyesho yake, huku vyombo vya habari vikiyatangaza 'maajabu ya karne' na 'maajabu ya nane ya dunia.'

Kuona kupitia ukuta

fdcx

Chanzo cha picha, BRITISH PATH

Maelezo ya picha, Dokta akiyafunika macho ya Khuda Baksh kabla ya maonyesho

Kuda Baksh alitambulishwa kwenye kipindi cha kwanza cha televisheni cha Ripley's Believe It or Not. Baadaye alianzisha kipindi chake cha televisheni 'Kuda Baksh: Hindu Yoga.'

Kipindi chake kiliwafanya watu waamini ni kweli ana uwezo wa kusoma bila kuona kwa macho.

Booth aliandika kuhusu moja ya madai ya Bakhsh, ambayo yalitangazwa sana na waandishi wa habari, yalisababisha hofu miongoni mwa waigizaji watatu wa kike ambao walipangwa kutumbuiza katika moja ya maonyesho ya Bakhsh.

Baksh alidai alikuwa akifanya mazoezi ya kuona kupitia kuta za matofali na ndiyo maana wanawake hao waliomba chumba cha kubadilishia nguo mbali na Baksh.

Hatimaye aliondoka London na kuhamia Marekani ambako aliendelea kutumbuiza katika kumbi nyingi ikiwa ni pamoja na klabu maarufu ya Hollywood Magic Castle.

Kuda Baksh aliaga dunia Los Angeles, California 1981. Alitumia siku zake za mwisho kucheza karata na wachawi kwenye Jumba la Uchawi. Booth anaandika alishindwa ikiwa tu hajayafunika macho.