Mwanamke anayewaokoa wenzake wanaotuhumiwa kwa uchawi

Monica Paulus at a podium with an illustrated background

Chanzo cha picha, Shali Reddy

Maelezo ya picha, Monica Paulus amejitolea maisha yake kufanya kampeni dhidi ya unyanyasaji unaohusiana na tuhuma za uchawi

"Wananipigia kelele na kusema: 'Umemuua."

Wakati baba yake Monica Paulus alipozirai na kufa kutokana na mshtuka wa moyo, kaka yake alimshtumu kwa kumuua baba yao kupitia uchawi. Alitishiwa kifo cha mateso.

"Nilishtuka sana. Marafiki zangu wote, familia yangu, pia ilinitenga na kunifanya nijihisi kuwa mtu mbaya," anasema. "Waliponishtumu, nilihisi aibu na unyanyapaa."

Alilazimika kutoraka nyumbani kwao na kuishi mafichoni katika mkoa mwingine wa Papua New Guinea, nchi ya kisiwa oliyopo eneo la kusini-magharibi mwa Pasifiki.

Mfano wa watu katika vivuli wakiwa na mienge inayowashwa inayoelekeza kwa mwanamke pekee

Chanzo cha picha, Shali Reddy

Maelezo ya picha, Imani ya kishirikina ni imani iliyoshikiliwa sana na watu wengi nchini Papua New Guinea

'Ni unyama'

Unyanyasaji unaohusiana na tuhuma za uchawi (SARV) umeenea nchini Papua New Guinea. Ingawa hakuna data ya kuaminika inayopatikana kujua unatokea mara ngapi, takwimu za serikali zinasema kumekuwa na takriban matukio 6,000 katika miaka 20 iliyopita.

Hata hivyo makadirio yanaonyesha kuwa idadi hii ni kubwa zaidi, huku maelfu ya waathiriwa - hususan wanawake na wasichana - wakishutumiwa kila mwaka. Mara nyingi hufanyiwa matendo ya kikatili na kingono.

Mara nyingi shutuma hutokana na vifo vya ghafla au magonjwa yasiyoelezeka.

"Tunazungumzia viwango vya juu vya unyanyasaji, baadhi zikiwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa," anasema Stephanie McLennan, meneja mkuu wa mipango ya Asia wa shirika la kutetea haki la Human Rights Watch, ambaye amefanya kazi kwa mapana katika masuala ya vurugu zinazohusiana na uchawi.

"Kuna mashambulizi makali sana ya kundi la watu ambalo linawashikilia wahasiriwa, kuteswa, kuwachomwa kwa fimbo za chuma, kuwavua nguo zao, na mara nyingi kuwaua. Ni ukatili wa ajabu."

Kisa cha Mary Kopari kiligonga vichwa vya habari kimataifa mwaka huu wakati alipouawa kikatili kufuatia kifo cha mtoto wa kiume wa miaka miwili.

Mchoro wa mwanamke na mtoto mbele ya nyumba inayowaka moto iliyozungukwa na mitende.

Chanzo cha picha, Shali Reddy

Maelezo ya picha, Mara tuhuma za uchawi zinapotolewa inaweza kuwa vigumu kuepuka vurugu

Alikuwa akiuza viazi sokoni wakati umati ulipomkamata na kumteketeza akiwa hai. Hakuna aliyekamatwa licha ya tukio hilo kurekodiwa na kuripotiwa na vyombo vya habari vya ndani.

Wanawake wengine kadhaa pia walilengwa lakini walifanikiwa kutorokea msituni, asema Bi McLennan.

Kusulubiwa mitaani

Wakati Monica alipotuhumiwa kwa uchawi, yeye pia alifanikiwa kutoroka.

"Wakati waliponihtumu kwa mauaji kupitia uchawi nilitengwa moja kwa moja. Hawakutaka ushahidi.

"Nilipigwa marufuku kuhudhuria mazishi ya baba yangu, sikuhusishwa kwa vyovyote. Hapo ndipo niligundu akuwa sina nafasi katika familia, jamiiau kabila langu," alikumbuka.

Anaamini kwamba kaka yake alimshutumu kwa uchawi ili aweze kurithi mali peke yake.

Lakini sio shutuma zote zina nia ya kifedha - nyingi zinatokana na imani iliyokita mizizi.

"Uchawi umekita mizizi ndani ya fikira za watu," anaeleza Monica.

Kielelezo cha watu waliojificha msituni

Chanzo cha picha, Shali Reddy

Maelezo ya picha, Watu wanaoshutumiwa kwa uchawi mara nyingi hulazimika kutoka kwa nyumba zao, makabila na jamii zao

"Hata nilipokuwa msichana mdogo kulikuwa na mauaji, lakini yalikubaliwa katika jamii - ingawa mateso waliyopitia hayakuwa mabaya kama sasa."

"Zamani mauaji yalifanywa kimya kimya, sasa wanawake wanachukuliwa mitaani na kusulubishwa. Kwa kweli ni unyama."

Janga la Covid-19

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ongezeko la kesi zilizothibitishwa za Covid-19 huenda zimehusishwa na ongezeko la unyanyasaji unaohusiana na uchawi, kulingana na Human Rights Watch.

"Hakika kumekuwa na wasiwasi mkubwa kwamba Covid ingeongeza mzozo huu - na unyanyasaji wa kijinsia ni changamoto kubwa," anasema Bi McLennan.

Hii ni kwa sababu kukataa chanjo na kutoamini uwepo wa Covid ni suala "kubwa" nchini, Bi McLennan anasema, akimaanisha vifo vinavyosababishwa na Covid vinahusishwa na uchawi.

Lawama za uchawi mara nyingi hufuatana na magonjwa ambayo hayajaelezewa, kwa hivyo janga hilo limesababisha SARV kuenea zaidi.

Chanzo cha picha, Shali Reddy

Maelezo ya picha, Lawama za uchawi mara nyingi hufuatana na magonjwa ambayo hayajaelezewa, kwa hivyo janga hilo limesababisha SARV kuenea zaidi.

Mapema mwaka huu mwanamke mmoja na bintiye waliokolewa na polisi baada ya kushikiliwa na kuteswa, wakishutumiwa kufanya uchawi wakati mumewe alifariki kutokana na maambukizi ya Covid-19. Habari za ndani zinasema wanawake hao, wenye umri wa miaka 45 na 19, wote walivunjika mikono na kuchomwa na chuma cha moto.

Serikali ya nchi hiyo sasa imeunda kamati ya bunge ili kukabiliana na ghasia hizo.

Mwenyekiti wake, Mhe Charles Abel, alisema: "Vurugu ni saratani inayokula Papua New Guinea [na] jamii. Sisi ni nchi ya Kikristo lakini kuua watu kwa jkisingizio cha uchawi sio mwenendo wa Kikristo.

"Watu wanauawa kikatili na hili haliwezi kuvumiliwa. Covid-19 inazidisha hali hii, kwa sababu watu wanaitumia kama kisingizio cha kuwaita watu wachawi. Hili lazima likomeshwe."

Presentational grey line
Colour illustration

Vurugu za uchawi, kwa idadi

  • Matukio 6000 ya vurugu za uchawi, ambayo karibu nusu yalisababisha kifo, yalirekodiwa nchini Papua New Guinea kati ya 2000 na Juni 2020, kulingana na ripoti ya bunge kuhusu unyanyasaji wa kijinsia.
  • Matukio hayahusu jamii za vijijini pekee - ripoti pia ilipata kesi 156 zilizorekodiwa katika wilaya kuu katika kipindi cha miezi 42 iliyopita.
  • Hukumu 19 za makosa ya SARV kwa mwaka, kwa wastani, zilirekodiwa kati ya 2010 na 2020 - zikionyesha ongezeko kidogo kufuatia kufutwa kwa Sheria ya Uchawi ya mwaka 2013, ambayo iliondoa mashtaka ya uchawi kama utetezi katika kesi za mauaji.
  • Uwindaji wa wachawi wa siku hizi haufanyiki Papua NG pekee- nchi nyingine kama vile Saudi Arabia, Gambia na Nepal pia hupitia matukio kama hayo, kulingana na Taasisi ya Kimataifa ya Uhuru wa Kidini.
Presentational grey line

Kuwatetea wahasiriwa

Kufuatia kile alichopitia yeye binafsi, Monica ameamua kuhatarisha maisha yake kuwalinda wengine dhidi ya wawindaji wachawi.

"Nimegundua mabadiliko katitika kipindi ambacho nimekuwa nikifanyia kazi suala hili, lakini sioni mabadiliko yakitokea hivi karibuni - haswa wakati huu wa janga la virusi vya corona," anasema.

Akiwa uhamishoni katika sehemu nyingine ya Papua New Guinea, Monica anasema aliona mwanamke akipigwa mawe hadi kufahadharani.

Mwanamume mmoja alijaribu kumbaka, katika juhudi za kujiokoa akamuuma na kumkata ulimi wake, na kutokana na tukio hilo akamshutumu kuwa mchawi.

"Aliuawa mbele ya maafisa wa serikali ambao waliitazama tu kilichoendelea," anasema. "Wakati huo nilijiambia lazima nichukue hatua."

Monica alianzisha shirika lisilo la kiserikali ambalolinatetea haki za wanawake- Highlands Women Human Rights Defenders Movement, na anakadiria kuwa limeokoa zaidi ya watu 500 katika kipindi cha miaka 15 tangu waanze kuwasaidia waathiriwa wa vurugu za uchawi.

Wafanyakazi wa kujitolea husaidia kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhamisha na kurejesha makazi, kutoa chakula na ushauri wa kisheria ili kuwawajibisha wahusika.

Wakati tuhuma za uchawi zinapotolewa, unyanyapaa huo pia huathiri kwa watoto wa mtuhumiwa.

Chanzo cha picha, Shali Reddy

Maelezo ya picha, Wakati tuhuma za uchawi zinapotolewa, unyanyapaa huo pia huathiri kwa watoto wa mtuhumiwa.

"Kuhamisha watu na kuokoa maisha ni muhimu lakini tunahitaji kupata haki kwa wanawake. Ikiwa jamii zinaona haki basi labda tunaweza kubadilisha mawazo inapokuja suala la shutuma za uchawi," Monica anaongeza.

Tangu aanze kazi hii, nyumba ya Monica imeteketezwa. Sasa ameikimbia nchi kabisa, akiishi kama mkimbizi nchi jirani ya Australia iliyo karibu.

"Ni vigumu sana kuwa mbali na watoto wangu watatu," anasema. "Kama watakuwa salama basi nitakuwa na amani, lakini ninaumia."

'Tunahitaji hatua'

Papua New Guinea ilipiata uchunguzi wa mara kwa mara mbele ya Umoja wa Mataifa (UN) ) mwezi uliopita, ambayo ulihitimisha kuwa serikali yake inapaswa kushughulikia kwa umakini matatizo ya haki za binadamu nchini humo, hasa unyanyasaji wa kijinsia.

Italia na Cyprus zimeishinikiza serikali ya Papua New Guinea kuingilia kati vurugu za uchawi na kutoa wito kwa mamlaka kuongeza juhudi kuzuia matukio hayo.

Gavana Allan Bird, naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia, aliambia BBC kwamba kwa mara ya kwanza "kiwango kikubwa" cha fedha zimetengwa katika bajeti ya serikali ya mwaka 2022 kukabiliana na vurugu za uchawi.

Kwa ufadhili mdogo wa kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, imeachwa kwa mashirika ya kiraia kutoa msaada kwa waathirika wa SARV

Chanzo cha picha, Shali Reddy

Maelezo ya picha, Kwa ufadhili mdogo wa kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia, imeachwa kwa mashirika ya kiraia kutoa msaada kwa waathirika wa SARV

Aliongeza: "Hii inapaswa kuwezesha mashirika yanayohusika na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambazo zimekuwa zikililia msaada kwa miongo kadhaa hatimaye kujibu... [ingawa] bado kibarua ni iwapo tunaweza kukabiliana na changamoto kubwa za utekelezaji."

Kwa sasa shughuli ya kuwalinda wahasiriwa inafanywa na watu wa kujitolea.

"Monica na wanaharakati wengine kwa muda mrefu wamejaza mapengo ambayo serikali inapaswa kuwapatia," anasema Bi McLennan. "Bila wao tungeshuhudia na vifo vingi."

Na Monica hajakata tamaa katika mapambano hayo.

"Tunahitaji hatua kamili kufikia mabadiliko ya kitamaduni," anasema. "Tumeokoa maisha ya watu wachache tu- kulikuwa na wengi ambao hatukuweza kuwaokoa."

Presentational grey line