Marcus Rashford: Galasa United, dhahabu Barcelona

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Brendon Mitchell
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Author, Adam Millington
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Marcus Rashford, ambaye amekuwa kama mgeni asiyehitajika Old Trafford tangu mwisho wa mwaka jana, yuko karibu zaidi na ndoto ya kuhamia Nou Camp baada ya makubaliano ya awali kufikiwa.
Hii si habari ya kushangaza sana, kwani Rashford anaripotiwa kuwa na hamu ya muda mrefu ya kujiunga na miamba hao wa Hispania, na mwezi uliopita alitamka wazi kuwa anatamani kucheza pamoja na nyota kinda Lamine Yamal.
Barcelona pia hawajaficha nia yao. Mwezi Mei, mkurugenzi wa michezo Deco alikiri kuwa wanampenda Rashford na kusema kuwa anaweza "kuboresha kikosi".
Hilo ndilo jambo linalozua mjadala kwa sasa, je, Rashford anaweza kweli kutoa mchango mkubwa kwa timu yake mpya?
BBC Sport inaeleza jinsi Rashford alivyojikuta safarini kujiunga na Barcelona na kwa nini wanamtaka.
Tumefikaje hapa?
Kuondoka kwa Rashford Old Trafford kumekuwa kama jambo lililotarajiwa kwa muda mrefu.
Kocha Ruben Amorim alimtema kwenye mechi ya derby dhidi ya Manchester City mnamo 15 Desemba mwaka jana na hajaichezea tena United tangu hapo.
Baadaye Amorim alimkosoa kwa kile alichoita 'hajitumi', akisema kuwa yuko tayari kumpa nafasi kocha wake wa makipa mwenye miaka 63 kuliko mchezaji "asiyejituma kila siku".
Rashford alijiunga na Aston Villa kwa mkopo mwezi Januari, akicheza mechi 17 na kurejea kwenye kikosi cha England, lakini akarudi Old Trafford mwezi uliopita huku hatma yake ikiwa bado haijulikani.
Lakini sintofahamu hiyo ilikuwa zaidi kuhusu ataenda wapi na sio kwaba kama atabaki ama la. Rashford ni miongoni mwa wachezaji watano walioiambia klabu kuwa wanataka kuondoka na kisha wakaambiwa wafanye mazoezi kivyao.
Simon Stone wa BBC Sport anasema:
"Hakuna shaka kwamba Rashford akiwa na motisha, umakini na ari ya kweli angekuwa chaguo la kwanza kwa Amorim. Lakini Rashford wa aina hiyo ameonekana mara moja tu tangu 2021."
"Akiwa Villa kulikuwa na dalili za kurudi kwenye kiwango chake lakini pia kulikuwa na mechi ambazo alionekana kucheza chini ya kiwango."
"Kumuuza mchezaji asiyetakiwa kwenda Barcelona ni jambo la ajabu kwa klabu kama Manchester United, lakini ndivyo hali ilivyo kwa sasa."
Kwa nini Barcelona wanamtaka?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Iwapo United waliomaliza nafasi ya 15 kwenye EPL hawamtaki Rashford kwa nini Barcelona wana nia naye?
Barcelona hawakuwa na shida ya kufunga mabao , waliweka wavuni mabao 102 na kushinda ligi, pamoja na kufunga 43 kwenye Ligi ya Mabingwa wakifika nusu fainali msimu wa 2024-25.
Tatizo lao kubwa lilikuwa safu ya ulinzi, si ushambuliaji.
Lakini bado wanatafuta nyongeza ya washambuliaji.
Andy West, mchambuzi wa soka la Hispania, anasema:
"Barcelona wameweka kipaumbele kusaka mchezaji wa kucheza kushoto kwenye ushambuliaji na kwa muda mrefu walikuwa karibu kumpata chaguo lao kuu, Nico Williams."
"Hata hivyo, Williams alisaini mkataba mpya na Athletic Bilbao. Mpango wa Luis Diaz kutoka Liverpool pia haukufua dafu."
Rashford anavutia zaidi kutikana na unafuu kifedha:
Makubaliano ya awali ni mkopo wenye chaguo la kumnunua jambo linalowapunguzia mzigo kifedha Barca.
"Walitarajia kumuuza kipa Marc-André ter Stegen ili kupata fedha – lakini mpango huo uligonga mwamba baada ya Mjerumani huyo kuhitaji upasuaji wa mgongo," anasema West.
Stone anaongeza:
"Kwa mkopo wenye chaguo la kumnunua, Barcelona hawana cha kupoteza."
"Usisahau, Chelsea walimchukua kwa mkopo Jadon Sancho kwa msimu mmoja, kisha wakamrudisha United licha ya kuwa na wajibu wa kumnunua kwa sababu hakucheza kwa kiwango bora."
Je, Rashford kupata namba kwenye safu hatari ya ushambuliaji Ulaya?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rashford anacheza kama mshambuliaji wa kati na pia upande wa kushoto, uwezo huu wake wa kubadilika ndiyo unawavutia Barca.
Andy West anasema:
"Barcelona wanajua kuwa Robert Lewandowski, anayefikisha miaka 37 mwezi ujao, hawezi kuanza kila mechi."
"Hivyo, uwezo wa Rashford kucheza kama namba 9 unawapa chaguo zaidi."
"Nafasi zake kubwa zitakuwa kucheza kama winga wa kushoto, nafasi iliyo na pengo tangu Neymar alipoondoka miaka nane iliyopita."
"Hivi sasa, Raphinha amebadilishwa kuwa kiungo mshambuliaji, huku Dani Olmo na Ferran Torres wakionyesha uwezo wa kawaida katika upande huo."
Rashford anaweza kujihakikishia namba kwenye safu ya kwanza ya ushambuliaji ya Flick akianza pamoja na Raphinha, Lewandowski na Lamine Yamal."
Je, bado ana kiwango cha kucheza na mastaa wa Barca?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rashford amefunga mabao 138 katika mechi 426 tangu aanze kuchezea United mwaka 2016 akiwa na miaka 18, na ameongeza mabao 17 katika mechi 62 alizochezea England.
Ana uzoefu mkubwa na akiwa na miaka 27, bado anaweza kuwa kwenye kilele cha uwezo wake.
Lakini neno "uwezo" limekuwa likitumika sana kumwelezea Rashford ambaye hajaweza kufunga mabao zaidi ya 20 katika msimu mmoja tangu 2022-23.
Akiwa Villa, licha ya kuonesha mwanga fulani, alifunga mabao mawili pekee kwenye EPL, mojawapo likiwa la penalti.
Stone anasema:
"Barcelona wanajua wanachukua hatari fulani. Na haijulikani wazi mpango wao ni upi, bila shaka si kumnyang'anya nafasi Yamal."
"Walakini, wakimpata akiwa hata karibu na kiwango chake bora, Rashford anaweza kuwa lulu kwenye La Liga na Ligi ya Mabingwa."












