Humphrey Polepole anayeripotiwa kutekwa Tanzania ni nani?

Polepole

Chanzo cha picha, THE CITIZEN

    • Author, Florian Kaijage
    • Nafasi, BBC News Swahili
    • Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Humphrey Polepole amekuwa mwanasiasa maarufu kwa takriban miaka 10 kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Malawi mwaka 2022. Baada ya kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu alifanya kazi katika mashirika yasiyo ya kiseikali na kufanya kazi kwa karibu na taasi za vijana ukiwemo Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Alianza kujulikana zaidi kwa umma mwaka 2012 alipoteuliwa na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete kuwa mjumbe wa Tume ya Katiba mpya, iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba na kumaliza kazi yake mwaka 2014.

Mwaka 2016 Rais John Magufuli alimteua Polepole kuwa Mkuu wa wilaya ya Musoma, mkoani Mara, alikohudumu kwa miezi michache kisha kuhamishiwa Ubungo Dar es Salaam kwa nafasi hiyo hiyo ya ukuu wa wilaya na kuhudumu kwa miezi michache pia.

Umaarufu wake uliongezeka alipoteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, nafasi ambayo kimsingi ni ya kuwa msemaji wa chama hicho kinachotawala Tanzania.

Anafahamika kwa kutetea sera na utendaji wa CCM na serikali ya Rais Magufuli, hata pale kulipokuwa na utata mkubwa wa masuala kama vile tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu, utekaji, kuwaweka watuhumiwa mahabusu kwa muda mrefu na wengine kufunguliwa kesi nzito za uhujumu uchumi na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020.

Rais Samia alipoingia madarakani Machi 19, 2021, Polepole hakukaa kwa muda mrefu kwenye nafasi ya usemaj, kwani aliondolewa kisha kuteuliwa kuwa Mbunge kabla ya kuteuliwa balozi nchini Malawi.

Anajulikana pia kwa kauli tata au kuhusu ahadi za CCM na serikali ambazo hazikuwahi kutekelezwa, kama vile ujenzi wa barabara za juu (fly overs) katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa barabara za juu zimejengwa nne pekee katika maeneo ya Ubungo, Tazara, Chang'ombe na makutano ya barabara za Mandela na Kilwa. Maeneo kama vile Mwenge na Morocco Barabara hizo bado hazipo.

Wakati fulani baada ya kuondolewa kwenye usemaji wa CCM aliwahi kunukuliwa kwenye mahojiano akisema CCM kumejaa watu wahuni wanaofanya matendo mabaya kama fitina, zengwe na uchawi, dhidi ya watu 'walionyooka' kama yeye na kudai hawezi kupatwa na uchawi hata shetani anamuogopa.

Tangu alipojiuzulu ubalozi na nyadhifa nyingine za umma barua aliyomwandikia Rais Samia Suluhu Hassan na kutaja sababu za kufanya hivyo, kumetokea masuala kadhaa.

Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Amos Makalla alizungumzia hatua hiyo siku ileile ya Julai 13 na kusema endapo Polepole angethibitisha iwapo barua ile ya kujiuzulu ni ya kwake maudhui ni ya kwake ni utashi wake lakini ambalo lilimfurahisha ni kwamba amemalizia kwa kusema atabaki kuwa mwanachama muadilifu wa CCM.

Polepole

Chanzo cha picha, Citizen

Pamoja na masuala mengine Polepole alikosoa utaratibu uliotumika kumteua Samia na Dkt Emmanuel Nchimbi kuwa wagombea wa urais na Makamu wa rais katika uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Oktoba 29.

"Uchaguzi ule ulikiuka desturi ya CCM inayokifanya chama kuendelea kuwa imara" alisema Polepole.

Haikupita muda, Polepole akaendelea kuporomosha tuhuma moja baada ya nyingine huku akiwataja bayana watu mbalimbali, baadhi yao mashuhuri kwa tuhuma za ufisadi na kujinufaisha na fedha umma kinyume cha taratibu.

Kwa namna ya pekee alikuwa gumzo kwelikweli mtandaoni. Wapo waliompongeza kwa dhati kwa ujasiri wake, pia wapo waliomponda, kumbeza na kumbagaza wakidai hakuwa na hadhi ya kuzungumzia aliyoyaweka hadharani maana alikuwa sehemu ya CCM wakati wa rais Magufuli, na sehemu ya serikali wakati wa Rais Samia. Baadhi ya waliotuhumiwa walijibu pia.

Rais Samia atengua uteuzi wa Polepole, amvua hadhi ya ubalozi

Agosti 5, 2025 Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kupitia Katibu Mkuu wake, Balozi Samwel Shelukindo ilieleza kwamba ilipokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka ikitaarifu kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametengua uteuzi wa Hamphrey Polepole aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba na kumuondolea hadhi ya ubalozi.

Uamuzi huo wa Rais ni chini ya mamlaka aliyonayo chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wizara ya mambo yan je ilieleza pia kuwa Rais Samia, kwa mamlaka aliyonayo chini ya utumishi wa umma, amemuachisha kazi Polepole kwa manufaa ya umma. Kwa mujibu wa barua hiyo, uamuzi huo ulianza tangu Julai 16, 2025.

Pamoja na hatua hiyo Polepole hakunyamaza, aliendelea kutoa tuhuma tofauti zinazowalenga watu binafsi na namna serikali ya Rais Samia inavyoendesha mambo yake.

Polisi yamtaka Polepole kuripoti kwa DCI

Septemba 15, 2025 Polisi Tanzania kupitia kwa msemaji wake David Misime ilitoa taarifa kumtaka H Polepole kuripoti katika ofisi ya Mkurugenzi wa upelelzi wa makosa ya jinai (DCI) na kwamba ilikuwa imefungua jalada la uchunguzi na kuwa uchunguzi ulikuwa ukiendelea kuhusu tuhuma ambazo Polepole alikuwa akizitoa tangu Julai 2025.

Misime alisema tuhuma alizokwisha kuzito na anazoendelea kuzitoa, kulinga nana jinsi alivyozielezea zinaashiria uwepo wa makosa ya kijinai na kwambaba kwa mujibu wa sheria zinahitaji ushahidi wa kuzithibitisha zitakapowasilishwa mahakamani.

Polepole aripotiwa kutekwa Dar es Salaam

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kabla ya Polepole kuripoti kwa DCi Jumatatu ya Octoba 6, 2025 Taanzania iliamka na taarifa za kutekwa kwa Polepole na watu wasiofahamika ambao wanaripotiwa kuvamia nyumbani kwa Polepole usiku, kuvunja milango tofauti na kuondoka naye kwenda sehemu isiyojulikana huku picha zilizoripotiwa kuchukuliwa eneo la tukio zikonesha milango ikiwa imevunjwa na rangi nyukundu inayosadikiwa kuwa damu ikiwa imetapakaa maeneo tofauti sakafuni.

Kaka wa Humphrey Polepole, Augustino Polepole ndiye alitangaza kwa niaba ya família na kwamba walikuwa wameripoti polisi kwa uchunguzi ili kufahamu ndugu yao alipo. Kamanda wa pilisi kanda maalum Dar es Salaam Jumanne Muliro aliiambia BBC kuwa wanafuatilia suala hilo. Msemaji wa polisi David Misime alisema bado wanamgoja Polepole alipoti kwa DCI kama walivyotangaza kwenye wito wao wa Septemba 15.

Mwanasheria wa Polepole, Peter Kibatala alitoa tangazao Oktoba 6 akivitaka vyombo vya dola Tanzania vyenya dhamana ya kuwalinda raia na mali zao kufuatilia na kuutangazia umma kuhusu hali mteja wao na mahali alipo.