Tishio linaloukabili mti wenye faida nchini Uganda

- Author, Njoroge Muigai
- Nafasi, BBC News
- Author, Anne Okumu
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kaskazini magharibi mwa Uganda, ambapo miti ya shea nut ilistawi katika misitu minene, Mustafa Gerima anatembea vijijini, akikusanya jumuiya kulinda kile anachokiona kama hazina inayotoweka.
Mustafa amekuwa ishara ya upinzani dhidi ya kutoweka polepole lakini kwa kasi kwa mti wa shea nut.
Amepewa jina la utani Bwana Shea au Bw Shea na wenyeji kwa sababu ya juhudi zake za kuokoa mti huo ambao una thamani kubwa ya kitamaduni na kiuchumi.
Miaka mingi iliyopita, Mustafa aliondoka Uganda na kuelekea Tanzania kikazi. Aliporudi, alikuta hifadhi ya Msitu wa Mlima Kei, ambayo hapo awali ilikuwa na miti ya shea mwitu, ilikuwa imegeuzwa kuwa tasa na yenye visiki.
"Kuona watu wakikata mti kila mara kumenisababishia maumivu mengi moyoni," Mustafa anasema.
"Jamii yetu imeathiriwa na umaskini. Hivyo wanautazama mti huo kama njia mbadala ya kujipatia kipato nafuu," anasema.
Uharibifu aliouona karibu naye ulimsukuma Mustafa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mti wa shea.
Moja ya kampeni zake ilihusisha kukamilisha matembezi ya siku 19, kilomita 644 kutoka mji mkuu wa Uganda Kampala hadi makao makuu ya Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP) mjini Nairobi, Kenya.
'Dhahabu nyeusi'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mabadiliko ya mti wa shea kutoka "dhahabu ya wanawake" hadi "dhahabu nyeusi" yanaakisi mzozo mkubwa wa kimazingira na kiuchumi nchini Uganda.
Kijadi, wanawake walikusanya njugu za mti wa shea ili kuzalisha siagi ya shea ya Nilotica, yenye thamani duniani kote kwa matumizi yake ya urembo na upishi. Zoezi hili lilikuwa endelevu, lenye kuwezesha, na lililojikita sana katika utamaduni wa wenyeji.
Lakini leo, wakulima wanakabiliwa na mavuno yasiyofanikiwa na ukame wa muda mrefu unaoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
"Miaka thelathini iliyopita, mti wa shea nut ulikuwa na muundo wa uzalishaji wake. Ulichanua maua mwezi Desemba kisha kufikia Aprili, ulikuwa tayari. Lakini sasa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa kuna ukame huu wa muda mrefu. Hivyo unaathiri uzalishaji wa karanga," anasema Mustafa.
Kwa sababu hii, wakulima wengi wanageukia mti kwa chanzo tofauti cha mapato, mkaa. Wanasema mkaa kutoka kwenye mti wa shea nut ni maarufu kwa sababu huwaka kuliko mkaa mwingine.

Profesa John Bosco Okullo, mtaalam mkuu wa kilimo mseto kutoka Chuo Kikuu cha Makerere, amekuwa akisoma miti ya shea kwa zaidi ya miongo miwili.
Kujihusisha kwake na spishi hizo kulianza mwaka wa 1999, wakati alipokuwa sehemu ya mradi wa Umoja wa Ulaya unaolenga kuhifadhi na kutumia mti huo.
"Katika miaka ya 90, jamii zilikuwa zikimiliki na kulinda miti ya shea," anasema.
"Lakini baada ya uvamizi wa ng'ombe na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe yaliyofanywa na Lord's Resistance Army kuwahamisha watu, hisia ya umiliki ilipotea. Watu waliporudi, walizoea kupata faida za muda mfupi kama vile uchomaji mkaa."
Profesa Okullo anasema kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yamezidisha hali hiyo.
"Tija imeshuka miti haitoi maua na kuzaa matunda kama ilivyokuwa hapo awali. Kubadilika kwa misimu ya mvua kumeharibu mzunguko wa asili wa mti wa shea," anasema.
Mti wa shea pia unatishiwa na upanuzi wa haraka wa miji.
"Mengi ya maeneo haya ambayo yalikuwa na miti ya shea sasa yana wilaya mpya, hospitali mpya, shule," anasema Okullo.
"Unakuta miti ya shea inakatwa kwa shughuli za maendeleo. Tunahitaji upandaji wa uhakika. Vinginevyo, ikiwa tunasubiri kuzaliwa upya kwa asili, itakuwa vigumu."
Uhifadhi
Uganda inapoteza takribani ekari 100,000 za misitu kila mwaka, na sehemu kubwa ya hiyo inajumuisha miti ya shea.
Mara baada ya kufunika maeneo makubwa katika "ukanda wa shea" kutoka Magharibi hadi Afrika Mashariki, katika baadhi ya mikoa idadi ya miti ya shea imeshuka kutoka 43% hadi 13%.

Hasara hii imekuwa na athari ya moja kwa moja kwa watu kama Mariam Chandiru, mzalishaji wa siagi ya shea huko Koboko.
"Tungepata pesa nzuri za kuwapeleka watoto wetu shule na kutunza familia zetu. Lakini sasa biashara yangu inaporomoka, ni kikwazo kikubwa," anasema.
"Nilikuwa nauza hadi dumu tano za mafuta ya shea kwa wiki, sasa hivi naweza kujaza jeri mbili tu."
Licha ya mtazamo wa huzuni, kuna msukumo unaokua kuelekea uhifadhi.
"Kwa sasa, kuna taasisi nyingi zisizo za kiserikali zinazohamasisha jamii," Profesa Okullo anasema.
"Watu wanapanda miti mipya na kuilinda ile inayozaa upya kutokana na vishina.
Wengine hata wanatumia mbinu za kuunganisha ili kufupisha msimu, ilikuwa ikichukua miaka 15-20 kabla ya kuzaa, sasa baadhi ya miti inazaa mapema zaidi."
Ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka na kusaidia minyororo endelevu ya ugavi, profesa na wenzake wanakumbatia teknolojia.
"Tunaungana na wenzetu wa sayansi ya kompyuta na fizikia kutumia akili mnemba, Ili tuweze kuchora ramani ya miti ya shea iliyokomaa na tujaribu kutayarisha mavuno," anasema.

Serikali ya Uganda pia imetambua kuathirika kwa mti wa shea nut na mwaka 2023, ilipiga marufuku ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa. Bado, utekelezaji unabaki kuwa kikwazo.
"Kulikuwa na agizo la rais kuacha kukata miti ya shea, lakini imekuwa vigumu kutekeleza," anasema Okullo.
"Mahitaji ya mkaa ni makubwa zaidi mijini, wanaokata miti sio wale wanaotumia mkaa. Tunatakiwa kutoa nishati mbadala kwa miji ili kupunguza mahitaji," anasema.
Huku Koboko, Mustafa Gerima anaendelea na matembezi yake marefu ya kuhamasisha watu, akizungumza na halmashauri za mitaa, kuandaa kampeni za kupanda.
"Hili lazima lisiwe suala la mtu mmoja, lakini lazima lilete juhudi za pamoja, jukumu la pamoja," anasema.
Hatua zake zinazofuata ni pamoja na kuzindua mpango wa ufuatiliaji wa miti mashinani na kushirikiana na shule kujumuisha uhifadhi wa mazingira katika mitaala ya ndani. Anasema dhamira yake si kuokoa mti tu bali kuhifadhi njia ya maisha.
"Tunatakiwa kufikiria kuhusu vizazi vyetu vijavyo. Wakija na kukuta mashina tu, watatufikiriaje?".















