Kutoka kwenye kutovutia hadi kuwa mali: Jinsi mwani unaonuka unavyotumika katika magari

Wakati safu kubwa ya mwani vamizi ilipoanza kuambaa kwenye fuo za Caribea mnamo 2011, wakaazi wa eneo hilo walipata taharuki.
Hivi karibuni, milima ya sargassum isiyovutia baada ya kubebwa na mikondo kutoka Bahari ya Sargasso inayohusishwa na mabadiliko ya tabia nchi - ilikuwa ikizunguka ukanda wa pwani wenye thamani, ikiwafukuza watalii kwa harufu kali inayojitokeza inapooza.
Jinsi hasa ya kulikabili lilikuwa tatizo la idadi isiyo na kifani kwa visiwa vidogo vinavyotegemea utalii vilivyo na rasilimali chache.
Mnamo 2018, Waziri Mkuu wa Barbados Mia Mottley alitangaza sargassum kuwa dharura ya kitaifa.
Sasa, kikundi cha wanasayansi wa Caribea na wanamazingira wanatumai kubadili hali ya tatizo hili kwa kubadilisha mwani unaosumbua kuwa nishati ya mimea yenye faida kubwa.

Chanzo cha picha, Rufus Gobat
Hivi karibuni walizindua gari la kwanza duniani linaloendeshwa kwa gesi asilia.Kitovu hicho cha ubunifu cha mafuta kilichoundwa katika Chuo Kikuu cha West Indies (UWI) huko Barbados pia hutumia maji machafu kutoka kwenye viwanda vya pombe kali na mbolea inayotokana na kinyesi cha kondoo wa asili wa kisiwa hicho ambao hutoa bakteria muhimu ya anaerobic.
Timu hiyo inasema gari lolote linaweza kubadilishwa ili kutumia gesi kupitia mchakato rahisi na wa bei nafuu wa uwekaji wa saa nne, kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi, kwa gharama ya jumla ya karibu $2,500 (£1,940).
Hapo awali watafiti walichunguza matumizi ya miwa katika kupunguza utegemezi wa nishati ghali, iliyoagizwa kutoka nje ya nchi na kusaidia Caribean kuelekea la kudhibiti uzalishaji wa hewa chafu.
Hata hivyo, licha ya Barbados kuwa mojawapo ya visiwa vichache ambavyo bado vinazalisha miwa, kiasi hicho kilionekana kutotosha kwa malengo makubwa ya timu hiyo, anaeleza mwanzilishi wa mradi huo Dk Legena Henry.

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sargassum kwa upande mwingine, anaelezea kwa masikitiko, ni kitu "hatutawahi kuishiwa".
“Utalii umepitia kipindi kigumu sana kutokana na mwani; hoteli zimekuwa zikitumia mamilioni kukabiliana nao. Imesababisha shida, "Dkt Henry, mtaalam wa nishati mbadala na mhadhiri wa UWI, anaendelea.
Wazo kwamba inaweza kuwa na lengo muhimu lilipendekezwa na mmoja wa wanafunzi wake, Brittney McKenzie, ambaye alikuwa ameona kiasi cha malori yaliyokuwa yakitumwa kusafirisha sargassum kutoka fuo za Barbados.
"Tulikuwa tumetumia wiki tatu tu kutafiti kuhusu miwa. Lakini nilimtazama Brittney usoni na alifurahi sana, sikuweza kumkatisha tamaa,” Dk Henry anakumbuka.
"Tayari tulikuwa na maji taka kutoka viwandani kwa hivyo tuliamua kuweka na sargassum na kuona nini kingetokea."
Brittney alipewa jukumu la kukusanya mwani kutoka kwenye fukwe na kuanzisha vinu vidogo vya kufanyia utafiti wa awali.
"Ndani ya wiki mbili tu tulipata matokeo mazuri," Brittney aliambia BBC. "Ilikuwa inageuka kuwa kitu kikubwa zaidi kuliko tulivyofikiria hapo awali."
Timu hiyo iliwasilisha hati miliki kwenye fomula yao na, mnamo 2019, iliwasilisha mradi wao kwa wawekezaji watarajiwa wakati wa mkutano,kando na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa huko New York.
Baada ya kuguswa huko Barbados, simu ya Dk Henry ilikuwa "ikivuma" na jumbe za pongezi - ikiwa ni pamoja na moja kutoka kwa Wakfu wa Marekani wa Blue Chip uliotoa $100,000 ili kufanikisha kazi hiyo.
Mwanabiolojia Shamika Spencer aliajiriwa kufanya majaribio ya kiasi tofauti cha sargassum na maji taka ili kubaini ni mchanganyiko gani ulitoa gesi ya asilia zaidi.

Anasema alikwepa nafasi ya kushiriki.
"Sargassum imekuwa ikisumbua eneo hilo kwa miaka kadhaa," Bi Spencer, ambaye anatoka Antigua na Barbuda, anaelezea.
"Siku zote nilikuwa nikijiuliza kuhusu mwani huu mpya unaoharibu fukwe huko Antigua, na nilipokuja Barbados kusoma niliona hapa pia."
Mwani huu hautishii utalii tu. Pia huwa tishio kwa afya ya binadamu kupitia madini yanayofahamika kitaalamu kama hydrogen sulphide yanayotolewa baada ya kuoza pamoja na wanyamapori asilia kama vile watoto wa kasa wa baharini walio hatarini kutoweka ambao hunaswa kwenye mikeka minene ya mwani wa ufukweni.
Uchafuzi wa maji na joto linaloongezeka baharini vinatajwa kuwa na sargassum, ni matokeo mengine mabaya ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo Caribean imechangia kidogo lakini mara nyingi hubeba mzigo mkubwa.
Wito wa fidia ya mazingira kutoka kwa viongozi akiwemo kiongozi wa Barbados Mia Mottley na Waziri Mkuu wa Antigua Gaston Browne umeendelea kutolewa katika miaka ya hivi karibuni huku eneo hilo likipambana na viwango vya bahari vinavyoongezeka kila mara na ongezeko la hali mbaya ya Dhoruba.
Huku tukingojea zile zitakazozaa matunda, mradi huu unawakilisha mfano mmoja wa Caribean kuchukua mustakabali wa kimazingira.
"Niligundua ilikuwa muhimu kwamba baada ya kuondoa sargassum kwenye ufuo, haiendi tu kwenye taka," Bi Spencer anaendelea.
“Kwa kuiuza tena kwenye magari unalinda utalii na kuzuia watu kuuvuta. Tunapoongeza mafuta kwenye magari mengi itahitajika kiasi kikubwa sana.
Kutazama mafanikio ya jaribio lililofanywa katika gari aina ya Nissan Leaf linalochajiwa na gesi asilia - kutoka Kituo cha Caribean cha Nishati Mbadala na Ufanisi wa Nishati - kulisisimua sana, anatabasamu Dk Henry.
Mhandisi wa mitambo aliyejifunza MIT alifahamu wazi alikuwa akihatarisha nafasi yake ikiwa mradi huo utashindwa.
Hatukulala usiku mmoja kabla ya tukio la jaribio," anakiri. "Nilikuwa nikifanya kazi muhimu Zaidi katika Maisha yangu"
Dk Henry na mumewe, mtafiti wa data Nigel Henry, waliunda kampuni ya teknolojia ya Rum na Sargassum Inc na wako kwenye mpango wa kubadilisha taswira ya uzalishaji wa nishati katika Caribean.
Wote wawili wanatokana na wazalishaji wakuu wa mafuta Trinidad, walisoma nchini Marekani na walikusudia kunufaisha nchi yao kupitia ujuzi huo.
"Lengo langu ni kusaidia kujenga eneo hili," Dk Henry anasema. "Sasa tunafanya majaribio ya magari manne ili kuonyesha mifano halisi ili kuwashawishi wafadhili kwamba hii inaweza kutekelezeka’’
Anakadiria kuwa itagharimu takribani $2m kuonyesha shughuli za awali za kibiashara na $7.5m kufikia hatua ambapo kampuni inaweza kuuza gesi kwa teksi 300 huko Barbados.
Wafadhili wanaotazamiwa ni pamoja na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa, Umoja wa Ulaya na benki za maendeleo za kimataifa kupitia uwezeshaji kwa mikopo.
Timu inapanga kuongeza wigo wa kazi yake kwa kuanzisha kituo cha gesi asilia ili kuwa mbadala wa kituo chake kidogo kilichopo.
UWI inatarajia kuanzisha ubunifu mwingine wa sargassum pia, kama vile bidhaa za kudhibiti wadudu.
Bi Spencer anasema imekuwa "faraja" kushuhudia matokeo ya utafiti wa timu hii.
"Kushuhudia uwezo halisi kunanitia moyo kuendelea kufanya kazi," anaongeza.

Chanzo cha picha, Tremaine Yearwood
Kuhusu Brittney, miaka mitano baada ya kugundua, anasema bado "anajifinya" mwenyewe.
"Kuona gari likiweza kuwaka ilinisisimua," anatabasamu. "Ningewahimiza wanasayansi wote wachanga kusonga mbele na tafiti zao. Huwezi kujua ni lini unaweza kufanya ugunduzi mkubwa unaofuata."
"Imechukua miaka ya kufanyia kazi, na bidi kubwa kufikia hatua hii.
Dk Henry anakubali. "Ni mfano wa uvumbuzi wa UWI na inaweza kusafirishwa kwa ulimwengu mzima, kwa sababu sio caribbean pekee iliyoathiriwa; sargassum pia huathiri sehemu za Afrika Magharibi, Amerika Kusini na Florida.
“Visiwa hivi vidogo vimeunda teknolojia ambayo inaweza kunufaisha dunia nzima; huu ni ushindi mkubwa kwa Caribean."
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Yusuf Jumah












