Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Nililisha nguruwe miili ya wanawake ili kupoteza ushahidi'
Mfanyakazi katika shamba moja nchini Afrika Kusini ameeleza mahakama jinsi alivyolazimishwa na bosi wake kuwalisha nguruwe miili ya wanawake wawili weusi katika jaribio la kupoteza ushahidi baada ya kupigwa risasi.
Adrian De Wet, 21, alisema aliambiwa atupe miili hiyo ndani ya zizi la nguruwe, akieleza kuwa "nguruwe wanapokuwa na njaa ya kutosha, watakula chochote".
Alikiri kuwafyatulia risasi wanawake hao wawili na bosi wake mmiliki wa shamba Zachariah Johannes Olivier kabla ya kumwamuru kusaidia kutupa miili yao.
Bw Olivier na mwanamume mwingine, William Musora, wanatuhumiwa kwa mauaji baada ya Maria Makgato, 45, na Lucia Ndlovu, 34, kuuawa wakidaiwa kutafuta chakula kwenye shamba karibu na Polokwane katika jimbo la Limpopo kaskazini mwa Afrika Kusini mwaka jana.
Msimamizi wa shamba Bw De Wet pia alishtakiwa kwa mauaji, lakini mashtaka yalitupiliwa mbali na upande wa mashtaka alipogeuka kuwa shahidi wa serikali. Alikuwa akijitetea kuwa alilazimishwa kuitupa miili hiyo kwenye zizi la nguruwe.
Siku ya Alhamisi, Bw De Wet aliambia Mahakama Kuu ya Polokwane kwamba yeye na Bw Olivier, 60, walijihami kwa bunduki zinazotumika kuwinda na kusubiri waliovuka mipaka waingie shambani usiku wa tarehe 17 Agosti 2024.
Alisema baada ya kusubiri kwa dakika 30 walisikia sauti za watu wakizungumza na kuelekea upande wao.
Kisha walifyatua risasi na kusikia mtu akipiga kelele, kabla ya kukagua eneo hilo na kukuta mtu amelala kifudifudi.
Baada ya kutoka eneo hilo na kwenda kulala, walirudi kesho yake asubuhi na kukuta ni mwili wa mwanamke.
Bw De Wet alisema aliombwa na Bw Olivier amsaidie kutupa mwili ndani ya zizi ambapo nguruwe wakubwa wanane takriban kumi walikuwa wakifugwa.
Siku iliyofuata mwili mwingine ulipatikana karibu mita 25 kutoka mahali ambapo wa kwanza ulipopatikana.
Bwana Olivier, De Wet na Musora, 50, wanasemekana kutupa mwili wa pili ndani ya zizi la nguruwe.
Siku ya Jumanne iliyofuata walirudi humo na kukuta nguruwe hao walikuwa wamewauma vipande vikubwa vya nyama wanawake hao.
Picha zilizowasilishwa kama vielelezo mahakamani zinaonyesha kutoweka maeneo ya makalio, uso, mapaja na mabega.
Mwendesha mashtaka wa serikali Wakili George Sekhukhune alimuuliza Bw De Wet lengo la kuweka miili ndani ya zizi hilo lilikuwa nini, na akajibu: "Tulikuwa tukitaka kupoteza ushahidi kwa sababu nguruwe wanapokuwa na njaa ya kutosha, watakula chochote."
De Wet pia alisema Olivier alikatakata bunduki za kuwinda na mashine ya kusagia pembe na kuziteketeza sehemu za mbao za bunduki hiyo.
Kisha walizikata na kuzitupa ndani ya kisima silaha zilizotumika ikiwa ni pamoja na mabaki ya risasi.
Mtoto wa mwathiriwa Bi Makgato alilia mara kwa mara mahakamani, huku Olivier alionekana akifuta machozi De Wet akitoa ushahidi wake.
Kesi hiyo imezua ghadhabu kote nchini Afrika Kusini, na hivyo kuzidisha mvutano kuhusu ubaguzi wa rangi kati ya watu weusi na weupe nchini humo.
Hali hii imeenea sana katika maeneo ya vijijini nchini humo, licha ya kumalizika kwa mfumo wa ubaguzi wa rangi miaka 30 iliyopita.
Mashamba mengi ya kibinafsi yanasalia mikononi mwa wazungu wachache, wakati wafanyakazi wengi wa mashambani ni weusi na wanalipwa vibaya, jambo linalochochea chuki miongoni mwa watu weusi, huku wakulima wengi weupe wakilalamikia viwango vya juu vya uhalifu.
Uchunguzi wa mawakili wa Olivier na Musora utaendelea Jumatano ijayo.