FW de Klerk: Rais wa mwisho mweupe wa Afrika Kusini

FW de Klerk alikuwa kiongozi mkuu katika kipindi cha mpito cha Afrika Kusini kutoka taifa la ubaguzi wa rangi hadi demokrasia kamili.

Ingawa wimbi la historia pengine lingefanya mabadiliko hayo kutoepukika, ni De Klerk aliyeongeza kasi ya mageuzi.

Kimsingi, mhafidhina kwa asili, rais wa mwisho wa taifa lililotengwa alikuja kuamini kwamba ubaguzi wa rangi haukuwa endelevu.

Kukomesha kwake marufuku dhidi ya chama cha African National Congress na kuachiliwa kwa Nelson Mandela zilikuwa hatua zilizochochea hatua ya kuwa na utawala wa wengi.

Frederik Willem de Klerk alizaliwa tarehe 18 Machi 1936 huko Johannesburg, katika safu ya wanasiasa wa Kiafrikana. Baba yake, Jan, alikuwa waziri .

Alienda Chuo Kikuu cha Potchefstroom, kinachojulikana kwa uhafidhina, na wakati alipochukua shahada yake ya sheria, ubaguzi wa rangi ulikuwa umeimarishwa. Baada ya miaka 11 kama wakili alishinda kiti salama cha ubunge kwa chama tawala cha National Party mnamo 1972.

Msururu wa nyadhifa za uwaziri, wa mwisho katika elimu, ulimpeleka hadi juu ya chama chake. Wakati huo alikuwa muumini thabiti wa ubaguzi wa rangi na usanifu wake wa kisheria: maeneo tofauti ya makazi, shule na taasisi za vikundi tofauti vya rangi.

Hata hivyo, De Klerk alikuwa mtu wa nje wakati alipokuwa kiongozi wa chama Februari 1989, baada ya Rais PW Botha kuugua kiharusi.

Miezi sita baadaye, baada ya mzozo mkali na Botha, alichukua nafasi ya rais.

Botha, mhafidhina mara nyingi alizungumza juu ya hitaji la mageuzi, lakini alikuwa amepinga wito wa kuondolewa kwa marufuku ya vikundi vya kupinga ubaguzi wa rangi, na serikali yake ilijibu kwa nguvu maandamano yaliyoikumba nchi mwishoni mwa miaka ya 1980.

Vidonda vya kale

De Klerk baadaye alionyesha kwamba alikuwa tayari kukanyaga mahali ambapo Botha hajawahi kuthubutu. Alitoa mwito hadharani kwa Afrika Kusini isiyo na ubaguzi wa rangi na mwishoni mwa 1989 alimwachilia huru Walter Sisulu na wafungwa wengine wa kisiasa kama hatua ya awali kabla ya mageuzi yake makubwa zaidi.

Tarehe 2 Februari 1990, Rais De Klerk aliondoa marufuku kwa African National Congress na kumwachilia Nelson Mandela siku tisa baadaye.

Ni lazima ilionekana kwa De Klerk, alipokuwa akimwangalia Mandela akielekea kwenye uhuru, kwamba siku zake za kuwa madarakani zilikuwa chache.

Muda uliosalia wa muhula wake madarakani ulitawaliwa na mazungumzo ambayo hatimaye yangesababisha utawala wa wengi.

Lakini mazungumzo kuhusu katiba mpya yalifungua majeraha ya zamani. Kulikuwa na vurugu za kutisha kati ya ANC na wapinzani wake katika Inkatha Freedom Party.

Mnamo Aprili, De Klerk alitangaza kwamba vikosi vya usalama vitarudishwa kwenye vitongoji. Alisisitiza nia ya serikali yake "hatimaye kufunga vitabu vya zamani na kuanza katika ukurasa mpya".

Wale wanaong'ang'ania mapambano ya silaha na kusisitiza kuendelea kutawaliwa "lazima watambue kwamba tuna nia ya kuijenga Afrika Kusini mpya bila ukatili na bila machafuko. Vurugu na mapambano ya silaha yamepotezwa".

Mwandishi wa wasifu wa Mandela aliyeidhinishwa, mwandishi wa habari Anthony Sampson, baadaye alipendekeza kuwa De Klerk aliungana na vikosi vya usalama katika jaribio la kugawanya vikundi viwili vikuu vya kupinga ubaguzi wa rangi. Ilikuwa ni shutuma aliyoitoa Mandela mwenyewe katika kitabu chake, Long Walk to Freedom.

Kasi ya mabadiliko

Sampson pia alidai De Klerk aliruhusu mawaziri kuunga mkono kwa siri mashirika yanayounga mkono ubaguzi wa rangi ambayo kwa pamoja yalijulikana kama Kikosi cha Tatu.

De Klerk alikanusha vikali madai hayo, akisema hana mamlaka juu ya wale wanaochukua hatua za vurugu dhidi ya hatua ya demokrasia lakini baadaye alikiri katika mahojiano ya 2004 kwamba vikosi vya usalama vilifanya shughuli za siri. Pia alishutumu ANC kwa kuwahifadhi watu wenye itikadi kali wenye nia ya kuvuruga mchakato wa amani.

Pia walioghadhabishwa walikuwa ni watu weupe wenye msimamo mkali - waliokasirishwa na matarajio ya serikali ya watu weusi. De Klerk alihisi tishio hilo na kuwazidi ujanja kwa kutoa kura ya maoni ya "wazungu pekee" mwaka 1992, ambapo wengi wa wapiga kura weupe waliidhinisha mageuzi zaidi.

Kasi ya mabadiliko sasa ilionekana kutozuilika na mitazamo ya ulimwengu kwa Afrika Kusini ilikuwa ikibadilika. Mnamo 1993, De Klerk alitunukiwa kwa pamoja Tuzo ya Amani ya Nobel na Nelson Mandela, mtu ambaye angechukua nafasi yake kama rais.

Aliwahi kuwa naibu rais baada ya kura za kwanza watu wa rangi zote mwaka 1994 na alistaafu siasa mwaka 1997 akisema: "Ninajiuzulu kwa sababu nina hakika kwamba ni kwa manufaa ya chama na nchi."

Ijapokuwa uhusiano kati ya De Klerk na Mandela mara nyingi ulijaa mizozo mikali, rais huyo mpya alimtaja mtu aliyemrithi kuwa mtu mwadilifu sana.

'Idadi ya kutokamilika'

Mnamo 1998, De Klerk na mkewe Marike walitalikiana baada ya miaka 38 alipogunduliwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa mfanyabiashara wa meli, ambaye baadaye alimuoa.

Matendo yake yalilaaniwa vikali na Waafrikana wa Calvin, mojawapo ya sehemu za kihafidhina za jamii ya wazungu wa Afrika Kusini.

Miaka mitatu baadaye, Marike aliuawa wakati wa wizi. Mlinzi wa usalama mwenye umri wa miaka 21 alipatikana na hatia baadaye na kuhukumiwa kifungo cha maisha kwa mauaji hayo.

De Klerk hakuacha siasa. Alianzisha Wakfu wa FW de Klerk ili kukuza shughuli za amani katika nchi zenye jamii nyingi na alisafiri duniani kote kama mtetezi wa demokrasia.

Mnamo 2004 alijiondoa katika Chama Kipya cha Kitaifa kwa sababu ya mpango wa kuunganishwa na ANC. Alidai kuwa ameridhishwa kwa mapana na mabadiliko ya Afrika Kusini lakini alikiri kulikuwa na "kasoro kadhaa".

Nelson Mandela alipofariki mwaka 2013, De Klerk alitoa heshima kwa rais wa kwanza mweusi wa nchi hiyo. "Alikuwa muunganishi mkuu na mtu wa pekee sana katika suala hili, zaidi ya yote aliyofanya. Msisitizo huu wa upatanisho ulikuwa urithi wake mkubwa."

Mnamo 2015 aliingia kwenye mzozo katika Chuo Kikuu cha Oxford, akikosoa matakwa ya wanaharakati kwamba sanamu ya Cecil Rhodes katika Chuo cha Oriel inapaswa kuondolewa. "Wanafunzi," alisema, "siku zote wamekuwa wamejaa sauti na hasira isiyoashiria chochote."

FW de Klerk alibaki mwaminifu kwa urithi wake wa Kiafrikana. Baadhi ya wafanyakazi wenzake wa zamani walilalamika kuwa alikuwa mtu mbinafsi, akichukua fursa kwa sababu aliona mabadiliko hayangeepukika .

Lakini, bila kujali nia zake, jukumu lake katika kipindi cha mpito cha amani kwa utawala wa wengi nchini Afrika Kusini kinahakikisha nafasi yake katika vitabu vya historia vya Karne ya 20.