Riek Machar alivyoiweka Sudan Kusini njia panda

- Author, BBC Monitoring
- Nafasi, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Upinzani nchini Sudan Kusini umetoa wito wa "mabadiliko ya utawala" dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir baada ya miezi kadhaa ya kuvunjika kwa makubaliano ya kugawana madaraka mwaka 2018 na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, na kuiweka nchi hiyo katika hatari ya vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe.
Chama cha Sudan People's Liberation Movement/Army - Katika Upinzani (SPLM/A-IO) tarehe 15 Septemba pia kilitangaza serikali ya Kiir kuwa "haramu".
Haya yanajiri baada ya wizara ya sheria kupendekeza Machar afunguliwe mashtaka ya uhaini, mauaji na uhalifu dhidi ya binadamu. Machar amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu Machi. Baadaye Kiir alimvua Machar wadhifa wake kama makamu wa kwanza wa rais.
Serikali inamtuhumu Machar na washirika wake saba, ambao wanakabiliwa na mashtaka sawa na hayo, kwa "kupanga" mapigano mabaya mwezi Machi kati ya jeshi na wanamgambo wa kabila la Nuer wanaofahamika kama Jeshi la White katika mji wa Nasir kaskazini mashariki mwa jimbo la Upper Nile. Takriban wanajeshi 250 waliuawa.
SPLM/A-IO inasema mashtaka hayo "yamechochewa kisiasa" na ukiukaji mkataba wa kugawana mamlaka, ambao ambao unaeleza taratibu za kushughulikia utovu wa nidhamu wa maafisa wakuu.
Wachambuzi wanasema matokeo ya kesi ya Machar yanaweza kuamua sio tu hatima yake, bali pia makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2013-2018.
Tulifikaje hapa?
Wito waThe SPLM/A-IO wa kutaka mabadiliko ya utawala inafuatia miezi kadhaa ya mvutano tangu mapigano ya Machi na hatua zilizofuata za upande mmoja zilizochukuliwa na Kiir ambazo upinzani umesema ni jaribio la kujiimarisha mamlaka.
Mwishoni mwa mwezi Machi, mamlaka za usalama ziliwaweka kizuizini makumi ya washirika wa Machar, akiwemo Waziri wa Kawi Puot Kang Chol na Naibu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Gabriel Duop Lam kutokana na mashambulizi ya Nasir. Chol, ambaye alishtakiwa pamoja na Machar, pia alisimamishwa kazi mnamo 11 Septemba.
SPLM/A-IO imekuwa ikitaka maafisa hao waliozuiliwa kuachiliwa, ikitishia kuchukua hatua za kijeshi.
Kundi hilo lilitangaza kuwa mkataba wa amani ulisambaratika kutokana na kukamatwa kwa watu hao, wakimtuhumu Kiir kwa kuwaondoa wanachama wake kutoka nyadhifa za serikali.
Vikosi vitiifu kwa SPLM/A-IO na jeshi vimekabiliana katika maeneo kadhaa ya nchi tangu kukamatwa kwao.
SPLM/A-IO imejibu vipi?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
SPLM/A-IO ilipinga mashtaka hayo ikiyataja kuwa ya uzushi, kuishutumu SPLM kwa kutumia taasisi za serikali kuwaondoa wapinzani wa kisiasa na kuimarisha utawala wa chama kimoja.
"Mashtaka haya yametungwa… kufuta Mkataba Uliohuishwa wa Amani," alisema Reath Muoch, naibu mwenyekiti wa kamati ya mahusiano ya kigeni ya SPLM-IO.
Msemaji wa SPLM-IO, Pal Mai Deng pia alitangaza kusimamishwa kazi kwa Machar kuwa haramu, akitoa mfano wa Kifungu cha 5.3 cha makubaliano ya amani, ambayo inakabidhi jukumu la uwajibikaji kwa Mahakama ya Mseto ya Sudan Kusini, na sio mahakama za kitaifa.
Kundi lenye nguvu la waasi la National Salvation Front (NAS), ambalo hivi majuzi liliunda muungano na SPLM/A-IO, liliyataja mashtaka hayo kuwa "manyanyaso ya kikabila kwa kisingizio cha kutafuta haki".
Mnamo tarehe 16 Septemba, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na msemaji wa zamani wa rais James Gatdet Dak Lampuar alisema Kiir alikuwa akipanga njama ya "kumuondoa Machar kwa nguvu" ili kumuweka mwandani wake "atakayemhakikishia ulinzi wa urithi wake, mali ... kabla ya kuondoka madarakani".
Je, SPLM/A-IO iliyogawanyika inaweza kupinga utawala wa Kiir?
SPLM/A-IO, iliyodhoofishwa na mapigano ya miezi kadhaa ya mvutando wa ndani, haina uwezo wa kuikabili serikali kikamilifu.
Mnamo Aprili, Waziri wa anayeshughulikia mshikamano wa wa kitaifa Stephen Par Kuol, mwanachama mwandamizi wa SPLM-IO, alijitangaza kuwa mwenyekiti wa muda wa kikundi.
Kuol tangu wakati huo ameunganisha mrengo wake na serikali ya Kiir na anaripotiwa kuungwa mkono na chama tawala cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM) na Muungano wa Upinzani wa Sudan Kusini (SSOA), na anapigiwa upatu kuchukua nafasi ya Machar.
Mamia ya wanajeshi wa upinzani na wanasiasa pia wamejiunga na serikali katika wimbi la uasi tangu kuwekwa kizuizini kwa Machar.
Wakati huo huo, Kiir pia amewafuta kazi maafisa watiifu kwa Machar na nafasi zao kuchukuliwa na viongozi wa upinzani.
Baadhi ya wanachama wa SPLM-IO pia wameikimbia nchi, huku wengine wakielekeza utiifu wao kwa Kiir.
Wachambuzi wanasema kuongezeka kwa upinzani ni onyo kwa washirika wa kimataifa kwamba mpango wa amani hauwezezi kunusurika.
Jamii ya kikanda na kimataifa inasemaje?
Umoja wa Mataifa na Amnesty International wametoa wito wa kuzingatiwa kwa utawala wa sheria kufuatia mashtaka dhidi ya Machar.
"Kesi yoyote ya mahakama inapaswa kuzingatia viwango vya kimataifa vya haki na uwazi, kwa kuheshimu kikamilifu utawala wa sheria na haki za binadamu," msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric alisema tarehe 12 Septemba.
Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa yoyote ambayo imetolewa na Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Igad au Marekani, ambayo imefanya jitihada za pamoja za kupunguza mvutano huo, ikiwa ni pamoja na kutaka Machar aachiliwe.
Mwezi Machi, Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) ilionya kuwa nchi hiyo iko ukingoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na kutaka kujizuia, huku Marekani ikimtaka Kiir kumwachilia Machar na AU ilisisitiza haja ya kuzingatiwa na kutekeleza makubaliano ya amani.
Igad alielezea wasiwasi wake kuhusu kukamatwa kwa Machar na akajitolea kusimamia mazungumzo, huku Kenya ikitoa wito wa kukomeshwa kwa uhasama na kutuma mpatanishi.
AU ilituma wajumbe wa ngazi ya juu mjini Juba tarehe 2 Aprili ili kusuluhisha mzozo huo lakini timu hiyo iliripotiwa kuzuiwa fursa ya kumfikia Machar.
Nini kinaweza kutokea baadaye?
Mashtaka dhidi ya Machar yanaashiria kusambaratika kabisa kwa makubaliano ambayo yamechangia kudumisha amani nchini Sudan Kusini.
Muungano wa hivi majuzi wa kijeshi kati ya NAS na SPLM/A-IO umeongeza uwezekano wa kuzuka upya kwa vita vipya.
Vile vile, kundi la White Army, ambalo lilipigana upande wa majeshi ya Machar katika vita vya wenyewe kwa wenyewe, limekuwa likijipanga kushambulia miji mikubwa inayoshikiliwa na jeshi.
Mivutano ya kikabila kwa mara nyingine inapamba moto - hasa kati ya jamii ya Rais Kiir ya Dinka na Nuer ya Machar - na kufufua kumbukumbu za vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe.
Kushindwa kwa jamii ya kimataifa na kikanda kuingilia kati mzozo huo kunaweza kuhatarisha hali Sudan Kusini kurejea kwenye vita na kutengua mafanikio yoyote yaliyopatikana katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












