'Kufa kwa kiu': Athari ya mafuriko yaliyochanganyika na mafuta Sudan Kusini

r

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Maura Ajak & Stephanie Stafford
    • Nafasi, BBC Africa Eye
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Wafugaji wanaochota maji yenye matope katika madimbwi nchini Sudan Kusini wanafahamu vyema hatari wanayokumbana nayo iwapo watayanywa.

"Maji ni machafu kwa sababu eneo hili lina mafuta - lina kemikali," anasema chifu wao, Chilhok Puot.

Nyatabah, ni mwanamke kutoka jamii hii ya wafugaji wa ng'ombe katikati Jimbo la Unity, anasema: "Ukinywa, yanakufanya unatweta na kukohoa. Tunajua ni maji machafu, lakini hatuna mahali pengine popote, tunakufa kwa kiu."

Mhandisi wa zamani wa mafuta, David Bojo Leju, ameiambia BBC, mafuriko katika eneo hilo yanabeba uchafuzi hadi kwenye vyanzo vya maji.

Eneo kubwa la jimbo hilo liko kwenye maji kwa miaka kadhaa baada ya mafuriko ambayo hayajawahi kutokea, na wanasayansi wanasema yamepata nguvu kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Sudan Kusini ndiyo nchi changa zaidi duniani na mojawapo ya nchi maskini zaidi, huku serikali ikitegemea sana mapato ya mafuta.

Pia unaweza kusoma

Kipi kilitokea?

k

Chanzo cha picha, David Bojo Leju

Maelezo ya picha, Aliyekuwa mhandisi wa mafuta wa GPOC David Bojo Leju alipiga picha kadhaa baada ya kumwagika kwa mafuta na uchafuzi mwingine katika eneo la Roriak.

Jimbo la Unity, jimbo kubwa linalozalisha mafuta, daima hukumbwa na mafuriko ya msimu. Lakini mwaka 2019, mvua kubwa ilileta mafuriko ambayo yaliharibu vijiji, nyasi na misitu. Kisha mwaka baada ya mwaka, mvua kubwa hutokea na maji hutuama.

Mwaka 2022, theluthi mbili ya Jimbo la Unity ilifunikwa na maji, kulingana na Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) - hata sasa, karibu 40% ya jimbo hilo liko chini ya maji.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bojo Leju alifanya kazi kwa miaka minane katika kampuni ya Greater Pioneer Operating Company (GPOC), ubia kati ya makampuni ya mafuta ya Malaysia, India na China - huku serikali ya Sudan Kusini ikimiliki 5%.

Baada ya bomba kubwa kupasuka miaka mitano iliyopita, alianza kupiga picha madimbwi ya maji yenye mafuta na rundo la udongo mweusi katika Jimbo la Unity, ikiwa ni pamoja na maeneo ya karibu na Roriak, ambako wafugaji wanaishi.

Anasema umwagikaji wa mafuta kutoka katika visima vya mafuta na mabomba lilikuwa ni jambo la mara kwa mara, na alihusika katika kusafirisha udongo uliochafuliwa mbali na barabara, ili usionekane.

Alijaribu kuelezea wasiwasi wake kwa wasimamizi wa kampuni, lakini anasema kilichofanyika ni kidogo sana na "hakukuwa na mpango wa kuusafisha udongo huo."

Bojo Leju pia anasema maji yanayotolewa kutoka ardhini wakati mafuta yanapotolewa, mara nyingi yana hidrokaboni na vichafuzi vingine - hayakusafishwa vizuri

Kulikuwa na ripoti za kiwango cha juu cha mafuta, juu ya viwango vya kimataifa, katika maji yaliyotolewa "kila siku katika mkutano wetu wa asubuhi", anasema, "na maji haya yanaingizwa tena kwenye mazingira."

"Swali ni wapi maji yanakwenda?" Anasema. “Yanakwenda mpaka mtoni, hadi kwenye vyanzo vya maji ambapo watu wanakunywa, hadi katika madimbwi ambako watu huvua samaki."

Bojo Leju anaeleza kuwa "baadhi ya kemikali za mafuta zilishuka hadi kwenye maji ya ardhini, ambayo hutiririka hadi kwenye visima vya kunywa.

“Wakati mvua kubwa ilipoanza mwaka 2019, kuta zilichimbwa karibu na mafuta yaliyomwagika lakini hayakutosha kuhimili wingi wa maji," anaongeza.

Athari kwa watu na mifugo

l
Maelezo ya picha, Kuta huzuia maji ya mafuriko kuingia kwenye kambi ambayo inahifadhi takriban watu 140,000 waliokimbia makazi

Huko Roriak, hakuna taarifa kuhusu ubora wa maji ambayo wafugaji wanakunywa, lakini wanahofia uchafuzi wa mazingira unafanya ng'ombe wao kuugua.

Wanasema ndama huzaliwa bila vichwa au bila viungo.

Waziri wa Kilimo wa Jimbo la Unity anasema vifo vya zaidi ya ng'ombe 100,000 katika miaka miwili iliyopita ni kutokana na mafuriko pamoja na uchafu wa mafuta.

Katika msitu ulio karibu na Roriak, kikundi cha wanaume na wanawake wanakata miti ili kutengeneza mkaa.

Wametembea kwa muda wa saa nane kwenye barabara za vumbi na maji ya mafuriko hadi kufika msituni. Wanasema maji yaliyopo hapa ni machafu.

Hata ukiyachemsha "husababisha kuhara na maumivu ya tumbo," anasema mwanamke mmoja, Nyakal.

Mwingine, Nyeda, anafuta machozi, akisema anahitaji mkaa huo ili auze, na anahangaikia watoto wake saba, aliowaacha na mama yake kwa muda wa wiki moja.

Nyeda anaishi karibu na mji mkuu wa jimbo hilo, Bentiu, katika kibanda cha mianzi kwenye kambi inayohifadhi watu 140,000 ambao wamekimbia vita au mafuriko. Kambi hiyo imezungukwa na maji ya mafuriko na inalindwa tu mifereji.

Maji salama ni haba. Nyeda hutumia maji kutoka kwenye kisima kuosha na kupikia, lakini inahitaji pesa kununua maji ya kunywa.

Madhara kwa binaadamu

O
Maelezo ya picha, Wanawake wanaotengeneza mkaa katika eneo la Roriak wanasema huchemsha maji kabla ya kuyanywa lakini bado si salama

Wataalamu wa afya na wanasiasa katika eneo hilo wameambia BBC, kuwa wanaamini uchafuzi wa mazingira na ukosefu wa maji safi unaathiri afya ya umma.

Katika hospitali moja huko Bentiu, mama mmoja amejifungua. Pua na mdomo wa mtoto wake mchanga vimeunganika.

"Hawana maji safi," anasema Dk Samuel Puot, mmoja wa madaktari wanaomhudumia mtoto. "Wanakunywa kutoka kwenye mto ambao maji na mafuta yamechanganyika."

Anasema kuna matukio mengi ya watoto wanaozaliwa na matatizo, kama vile kutokuwa na miguu na kuwa na kichwa kidogo, huko Bentiu na pia Ruweng, eneo linalozalisha mafuta kaskazini mwa Jimbo la Unity.

Mara nyingi hufa ndani ya siku au miezi, anasema.

Upimaji unaweza kutoa jawabu kuhusu sababu za matatizo haya, lakini hospitali haina vifaa.

Wataalmu wa afya

K
Maelezo ya picha, Familia ya mtoto huyu aliyezaliwa katika hospitali ya Bentiu inaishi katika eneo ambalo maji yamechafuliwa na mafuta, daktari aliambia BBC.

“Inawezekana uchafuzi unaohusiana na mafuta unaweza kuchangia kuongezeka kwa hatari ya kuzaliwa na kasoro," anasema Dk Nicole Deziel, mtaalamu wa afya ya mazingira katika Chuo Kikuu cha Yale.

Uchafuzi wa mazingira ni sababu ya matatizo ya kuzaliwa, pamoja na maumbile, matatizo ya uzazi, maambukizi na lishe, anasema.

Baadhi ya kemikali zinazotolewa wakati wa uzalishaji wa mafuta zinaweza kuathiri maendeleo ya kichanga tumboni, anasema Dk Deziel.

"Ripoti zisizo za kawaida zinaweza kutumika kama viashiria vya matatizo yatokanayo na mazingira," anasema, lakini anasisitiza bila kukusanya data kwa utaratibu, kuonyesha ushahidi wa uhusiano huo itakuwa ngumu kujenga hitimisho.

Mwaka 2014 na 2017, shirika lisilo la kiserikali la Sign of Hope lenye makao yake nchini Ujerumani lilifanya tafiti karibu na maeneo ya uchimbaji mafuta katika Jimbo la Unity.

Walipata kiwango kikubwa cha chumvi na kiwango cha juu vya metali nzito katika maji karibu na visima vya mafuta, pamoja na viwango vya juu vya kemikali ya risasi na bariamu katika sampuli za nywele za binadamu.

Watafiti walihitimisha kuwa viashiria hivi ni vya uchafuzi wa mazingira kutokana na uzalishaji wa mafuta.

Serikali imeagiza ukaguzi wa kimazingira, lakini matokeo bado hayajawekwa wazi zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Nchi hiyo ilianzishwa mwaka 2011 baada ya kupata uhuru kutoka kwa Sudan. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano vilizuka mwaka 2013. Ni taifa linalokabiliwa na migogoro na linategemea sana mapato ya mafuta.

Moyo wa serikali

OK
Maelezo ya picha, David Bojo Leju amepewa hifadhi nchini Sweden baada ya kupokea vitisho nchini Sudan Kusini

"Kuzungumzia mafuta ni kama kugusa moyo wa serikali," anasema Bojo Leju akiwa nchini Sweden, ambako amepewa hifadhi.

2020 alifuatwa na mawakili wa Sudan Kusini ambao walitaka kuishtaki serikali kuhusu uchafuzi wa mafuta.

Alikubali kutoa ushahidi. Lakini anasema maafisa wa usalama walimzuia, kumpiga kichwani na bastola na kumlazimisha kutia saini hati ya kubatilisha ushahidi wake.

Alikimbia nchi hivi karibuni. Na mawakili hao hawakufuatilia tena kesi yao.

BBC iliutaka muungano wa mafuta wa GPOC na ofisi ya rais wa Sudan Kusini kutoa kauli kuhusu madai ya ripoti hii, lakini hawakujibu.

Wanasayansi hawana uhakika kama mafuriko katika Jimbo la Unity yatapungua.

Dk Chris Funk, mkurugenzi wa Kituo cha Hali ya Hewa katika Chuo Kikuu cha Carolina, Santa Barbara, anasema mwaka 2019 kulikuwa na viwango vya juu ya joto katika eneo la magharibi la Bahari ya Hindi.

Anasema kuna "uhusiano mkubwa" kati ya halijoto hii ya bahari na mvua kali za 2019 huko Afrika Mashariki.

Joto nchini Sudan Kusini limeongezeka na linatarajiwa kupanda zaidi, anaongeza. Hii inamaanisha kuwa mvua kubwa zaidi italeta hali mbaya zaidi.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla