Je, mradi mkubwa zaidi wa bwawa la kuzalisha umeme duniani uko mashakani?

    • Author, Wedaeli Chibelushi & Emery Makumeno
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuna mpango ya kujenga bwawa kubwa, lenye thamani ya mabilioni ya dola kwenye Mto Congo - ambalo litazalisha umeme wa kutosha unaoweza kutumika katika maeneo mengine ya Afrika.

Mradi huo utaitwa Bwawa la Grand Inga. Bwawa hilo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, litazalisha umeme mara mbili ya bwawa la Three Gorges la China. Litakuwa bwawa kubwa zaidi duniani la kuzalisha umeme.

Bwawa la Grand Inga liliwavutia wawekezaji na watengenezaji, lakini miongo kadhaa tangu mradi huo uelezwe, eneo la kutengenezea bwawa hilo bado halijaguswa.

Serikali ya DR Congo inasisitiza kuwa mpango huo bado upo, wakosoaji wanasema ucheleweshaji huo ni kutokana na utawala mbovu wa DR Congo.

Wiki iliyopita, kampuni inayomilikiwa na serikali ya China ya Three Gorges Corporation, ilijiondoa kwenye mradi huo, BBC imeelezwa.

Na kisha kuna gharama kubwa ya ujenzi, ambayo inaripotiwa kuwa ni kama dola za kimarekani bilioni 80 (£63bn), katika mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani.

Ingawa ujenzi haujaanza, lakini kumekuwa na msururu wa mikutano na majadiliano kati ya wahusika katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Takribani watu milioni 600 waliopo Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa hawana uwezo wa kupata umeme, kulingana na Shiŕika la Nishati la Kimataifa.

Majaribio ya kutatua tatizo hili yalianza miongo kadhaa iliyopita. Mwanzoni mwa miaka ya 2000, DR Congo na majirani zake - Afrika Kusini, Angola, Namibia na Botswana - walikuwa na ndoto ya kuwa na gridi ya pamoja ya umeme.

Waliutazama Mto mkubwa wa Congo, wakatambua maji yake yenye nguvu yana uwezo mkubwa wa kufua umeme.

Jumuiya ya kimataifa iliyopewa jina la Westcor - ilitaka kuongeza mabwawa mbali ya yale mawili ambayo tayari yapo kwenye mto huo - Inga 1 na Inga 2.

Kiongozi wa zamani wa DR Congo Mobutu Sese Seko alianzisha ujenzi wa mabwa hayo katika miaka ya 1970 na 1980. Iga 1 na 2 sasa yanafanya kazi kwa takribani 80% ya uwezo wao.

Westcor ilivunjika lakini mpango wa DR Congo wa Grand Inga bado upo, na ni mpango wa kuongeza mabwawa mengine sita ndani ya mto huo.

Mabwawa haya ya ziada yanakisiwa yatazalisha hadi megawati 40,000 za umeme kwa wakati mmoja. Licha ya makadirio ya awali kwamba Inga 3 ingekamilika ifikapo 2018, ujenzi haujaanza.

Mwishoni mwa mwaka jana, benki kuu ya dunia ilitangaza imerejea katika mazungumzo na serikali ya Congo, baada ya kuondoa ufadhili wake kwa Inga 3 mwaka 2016, baada ya "tofauti za kimkakati."

Nayo Benki ya Maendeleo ya Afrika - hivi karibuni imekuwa ikifanya kazi pamoja na Congo ili kuvutia uwekezaji wa kibinafsi kwenye mradi huo.

Mwezi Novemba, Fabrice Lusinde, mkuu wa kampuni ya umeme ya umma ya DR Congo, Snel, alisema, ikiwa ujenzi wa Inga 3 utaanza 2026. Mitambo miwili itaanza kufanya kazi ifikapo 2032. Umeme unaozalishwa na mitambo hii utagharamia ujenzi wa mitambo mengine katika bwawa hilo.

Inga 3 pekee inakadiriwa itazamisha 4,800MW za umeme. Afŕika Kusini, imetia saini mkataba wa maelewano (MoU), ikisema itachukua zaidi ya nusu ya umeme ya megawawiti hizo.

Kampuni ya Nigeria, Natural Oilfield Services, pia imeripotiwa kujisajili kama mnunuzi. Kama Afrika Kusini, Nigeria pia inakabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme. Guinea na Angola pia zinauangalia mradi wa Grand Inga.

Kwanini kuna mkwamo?

"Ni mradi uliopo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo," anasema José Ángel González Tausz, mwenyekiti wa AEE Power, Kampuni ya Uhispania na mhusika katika mradi huo. Tausz anasema bila kuficha. "Hata kama mradi huo ni mojawapo ya mradi bora zaidi duniani – hakuna uhakika."

Kwa miongo kadhaa, DR Congo imekumbwa na ufisadi, ukosefu wa miundombinu na maendeleo duni. Migogoro mashariki mwa nchi pia inagonga vichwa vya habari vya kimataifa - ingawa Inga iko maelfu ya kilomita kutoka katika mapigano.

Wawekezaji pia "wanaogopa" kwa sababu Grand Inga hautoleta faida kwa miongo kadhaa. Nani anajua kitakachotokea Congo katika miaka 30 ijayo."

Bw Tausz - ambaye baba yake alifanya kazi kama mhandisi kwenye Inga 1 mwaka 1972 - anasema ukosefu wa kujitolea kifedha kwa serikali ya Congo kumechangia kuchelewa.

Na kisha kuna suala la ufadhili. Septemba 2023, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo aliwaambia waandishi wa habari, nchi hiyo "bado inakabiliwa na matatizo katika kupata uwekezaji" kwa bwawa hilo.

Kujiondoa kwa kampuni ya Three Gorges ya China kunaongeza matatizo haya. Three Gorges ilikuwa mshirika mkuu, na ilileta pesa na utaalamu katika mradi huo mgumu.

Three Gorges walijiondoa huku wakiwa wamechukizwa na jinsi Rais wa DR Congo Tshisekedi alivyokuwa akishughulikia mradi huo.

Lakini bado hakuna uthibitisho rasmi wa kujiondoa kwao.

Athari kwa Mazingira

Licha ya uwezo mkubwa wa mradi huo, kuna wasiwasi mkubwa kuhusu athari za kimazingira na kijamii za mradi.

Ukosoaji ni kwamba bwawa hilo litazinufaisha nchi za Afrika Kusini na makampuni ya madini ya DR Congo, lakini sio watu wa Congo. 80% ya watu wa Congo hawana huduma ya umeme.

"Inga haitaleta umeme kwa watu," anasema Emmanuel Musuyu, mkuu wa muungano wa vyama vya kiraia vya Congo Corap. Anadai umeme mwingi tayari umeahidiwa kwa nchi ya Afrika Kusini na migodini.

Katika ripoti ya hivi karibuni kuhusu Inga 3, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ilikubali kwamba bwawa hilo "pekee halitoshi kushughulikia changamoto za nishati kwa DRC" lakini ikasema linaweza kuwa "kichocheo" cha mabadiliko ya kitaifa.

Benki ya Dunia imesema inachunguza jinsi gani inaweza kuisaidia serikali ya Congo kuhakikisha Inga "inaleta manufaa mapana kwa upatikanaji wa nishati."

Mashirika ya mazingira na haki za binadamu pia yana wasiwasi kuwa karibu wakaazi 37,000 katika eneo la Inga watahamishwa bila kulipwa fidia. Kulingana na mashirika kama vile International Rivers na Observatori del Deute en la Globalització, maelfu ya watu waliondolewa kwa lazima katika nyumba zao na hawakulipwa fidia wakati wa ujenzi wa Inga I na II.

Pia wanasema mabwawa mawili ya kwanza yaliharibu viumbe hai katika eneo hilo na mabwawa mengine ya ziada yana uwezekano wa kufanya vivyo hivyo.

"Kutakuwa na athari kwa samaki na viumbe wote wa majini, mradi utabadilisha mtiririko wa maji kwenye mito, tunaweza kuona baadhi ya samaki wakitoweka," anasema Bw Msuyu.

Utafiti wa 2018 unasema miradi mingi mikubwa ya umeme wa maji barani Ulaya na Marekani imeleta madhara kwa mazingira.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inatambua kuwa watu wataondoshwa ili kupisha ujenzi wa Inga III, lakini watapewa makazi mapya katika maeneo yenye huduma za kimsingi na kuahidi "fidia" itatolewa.

Pia inaelewa hatari kwa mazingira na kusema tathmini inayolenga kupunguza athari hii itakamilika ndani ya miaka miwili ijayo. Hata hivyo, kulingana na chanzo cha BBC kilicho karibu na mradi huo, serikali bado haijakusanya pesa za kutosha kufadhili tafiti hizo.

Bwawa hilo ni mradi mgumu wa kiuhandisi - ambao unahitaji washikadau wengi kufanya kazi pamoja kwa maelewano.

Kurejea kwa Benki ya Dunia, na kuondoka kwa Three Gorges, ni kielelezo kuwa DR Congo inapata changamoto katika kudumisha umoja huo. Licha ya azma ya DR Congo, ujenzi hauwezi kuanza isipokuwa ufadhili upatikane.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi