Bwawa La Ethiopia: Kwanini Misri na Sudan zina wasiwasi?

Misri imeishutumu Ethiopia kwa kuhatarisha mtiririko wa wa maji ya Mto Nile. Kauli hiyo imekuja kufuatia tangazo la Ethiopia kwamba imemaliza kujaza maji kwenye bwawa lake kubwa jipya.

Mradi wa bwawa la Ethiopia

Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (Gerd) liko kaskazini mwa nyanda za juu za Ethiopia, ambapo asilimia 85 ya maji ya Mto Nile hutiririka. Gerd liko maili 19 kusini - mpakani na Sudan na ni mradi mkubwa zaidi wa bwawa la kuzalisha umeme barani Afrika.

Lina urefu wa zaidi ya maili moja na urefu wa mita 145. Bado halijakamilika, lakini tayari limechukua miaka 12 ya ujenzi. Litagharimu dola za kimarekani bilioni 4.2.

Bwawa hilo litaisaidia vipi Ethiopia?

Ethiopia inataka bwawa hilo kuzalisha umeme kwa asilimia 60 ya wakazi wake ambao kwa sasa hawana umeme.

Inatarajiwa litaongeza pato la umeme la Ethiopia mara mbili , liwe chanzo cha biashara, usambazaji wa umeme, umeme kutokatika na kukuza maendeleo.

Linaweza pia kutoa umeme kwa nchi jirani zikiwemo Sudan, Sudan Kusini, Kenya, Djibouti na Eritrea.

Kwa nini Misri na Sudan zina lalamika?

Misri, yenye wakazi wapatao milioni 107, inategemea Mto Nile kwa karibu maji yake yote safi.

Inayahitaji kwa matumizi ya majumbani na kilimo - haswa kwa kukuza pamba, ambayo inahitaji maji mengi.

Maji ya Mto Nile pia hutumika kujaza Ziwa Nasser, hifadhi ya kuzalisha umeme wa Misri, katika bwa lla Aswan.

Sudan, yenye wakazi milioni 48, pia inategemea sana maji kutoka Mto Nile.

Nchi zote mbili zina wasiwasi kuwa bwawa hilo litairuhusu Ethiopia kudhibiti kiwango cha maji wanachopokea. Misri ina wasiwasi ikiwa Ethiopia itahakikisha maji ya kutosha yatatiririka ili kuzalisha umeme hasa wakti wa msimu wa mvua kidogo.

"Mradi wa Ethiopia unatazamwa ni kama kutojali maslahi na haki za nchi mto huo unazopita na usalama wao wa maji," wizara ya mambo ya nje ya Misri ilisema .

Imesema kupunguzwa kwa maji kutoka Mto Nile kwa asilimia 2 kunaweza kusababisha upotevu wa ekari 200,000 za ardhi ya umwagiliaji . Kupungua kwa maji pia kunaweza kuathiri shughuli za usafiri katika mto huo.

Ethiopia ililijaza bwawa hilo kwa muda wa miaka mitatu , ikisema kuwa hoja ya Misri kwamba inapaswa kulijaza miaka 12 hadi 21 haikubaliki.

Ingawa Sudan imeathiriwa na mradi huo katika Mto Nile sawa na Misri, mwitikio wake umetatizwa na migogoro nchini humo.

Je, makubaliano yanaweza kufikiwa?

Bwawa hilo limekuwa chanzo cha kutoelewana kati ya nchi hizo tangu ujenzi wake uanze mwaka 2011.

Mkataba wa 1929 (pamoja na mkataba wa 1959) uliipa Misri na Sudan haki kwa karibu maji yote ya Nile. Pia iliwapa haki ya kupinga miradi kama vile wa Ethiopia ambayo itawanyima sehemu yao ya maji.

Ethiopia ilisema haipaswi kufungwa na mikataba hii ya zamani, na iliamua kuanza kujenga bwawa wakati machipuo ya kiarabu, wakati kukiwa na msukosuko wa kisiasa nchini Misri.

Misri, Sudan na Ethiopia zilitia saini mkataba mpya mwaka 2015, lakini mazungumzo kuhusu jinsi Ethiopia inavyotumia maji ya Mto Nile kujaza bwawa hilo yamevunjika mara kwa mara.

Marekani iliingilia kati mwaka 2019, kujaribu kutafuta makubaliano kati ya Misri na Ethiopia lakini mafanikio yakawa madogo. Mazungumzo yalianza tena wiki tatu kabla ya Ethiopia kutangaza kuwa imemaliza kujaza bwawa.