Ongezeko la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi zaathiri ulinzi wa Ukraine na kuziharibu familia

Muda wa kusoma: Dakika 4

Maria Troyanivska alirejea nyumbani kwake mapema usiku ambao ndege isiyo na rubani ya Urusi ilishambulia chumba chake.

"Ilishambulia kupitia dirishani, hadi ndani ya chumba chake," mama yake Viktoria aliambia BBC.

Baada ya mlipuko huo, yeye na mumewe Volodymyr walikimbilia chumba kingine cha binti yao na kukuta kinateketea kwa moto.

"Tulijaribu kuzima, lakini kila kitu kilikuwa kinateketea," anasema huku akitokwa na machozi. "Ilikuwa vigumu kwetu kupumua - ikatulazimu kuondoka."

Ndege isiyo na rubani ya Shahed ya Urusi ilimuua mtoto wa miaka 14 kitandani mwake, katika chumba chake katika kitongoji cha Kyiv, mwezi uliopita.

"Alikufa papo hapo, na kisha kuteketea kwa moto," mama yake alisema.

"Ilitubidi kumzika kwenye jeneza lililofungwa. Haikuwezekana kunusuru maisha yake”

Urusi imezidisha kwa kiasi kikubwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Ukraine.

Zaidi ya 2,000 yalitekelezwa mnamo Oktoba, kulingana na wafanyikazi wa Ukraine ikiwa ni idadi iliyoreodiwa katika vita hivyo.

Ripoti hiyo hiyo inasema Urusi ilirusha ndege zisizo na rubani 1,410 mnamo Septemba, na 818 mnamo Agosti - ikilinganishwa na karibu 1,100 kwa kipindi chote cha miezi mitatu kabla ya hapo.

Ni sehemu ya kujiimarisha kwa vikosi vya Urusi.

Wavamizi wanasonga mbele kwenye mstari wa mbele. Wanajeshi wa Korea Kaskazini wamejiunga na vita kwa upande wa Moscow.

Na kwa kuchaguliwa kwa Donald Trump kwa muhula wa pili kama rais wa Marekani, vikosi vya Ukraine vilivyopungua na kudhoofishwa kwa vita vinakabiliwa na uungwaji mkono usio na uhakika kutoka kwa wafadhili hao wa kijeshi.

Ndege nyingi zisizo na rubani za Urusi zinazoshambulia Ukraine ni Shahed zilizobuniwa na Iran: zinazoendeshwa na propela, zenye umbo la kipekee la bawa na kichwa kwenye sehemu ya mbele.

Urusi pia inarusha ndege bandia zisizo na rubani,bila vilipuzi vyovyote, ili kuwachanganya vitengo vya ulinzi wa anga vya Ukraine na kuvilazimisha kupoteza risasi.

Ikilinganishwa na makombora ni rahisi kutengeneza, ni rahisi kurusha, na inatumiwa ili kudhoofisha ari ya Ukraine.

Unaweza pia kusoma

Kila usiku, raia wa Ukraine huingia kulala kwa kupokea viashiria kwenye simu zao, huku ndege zisizo na rubani zikizunguka nchi nzima, zikiwasha ving'ora.

Na kila asubuhi, wanaamka na kusikia habari za shambulizi jingine. Tangu mwanzoni mwa Novemba, ndege zisizo na rubani zimeshambulia Kyiv, Kharkiv, Odesa, Mykolaiv na Zaporizhzhia.

Siku ya Jumapili, Urusi ilirusha ndege 145 zisizo na rubani nchini Ukrainekwa mujibu wa Rais Volodymyr Zelensky - idadi iliyorekodiwa kwa siku moja tangu kuanza kwa uvamizi kamili.

Kyiv ilisema siku hiyo iliweza kuangusha ndege 62 zisizo na rubani, na kwamba nyingine 67 "zilitoweka" - ikimaanisha kuwa ziliangushwa kwa mashambulizi, au kutoweka kwenye za rada.

Ulinzi wa anga wa Ukraine wanajitahidi kukabiliana na idadi inayoongezeka.

‘’Hadi sasa tumekuwa tukiingilia mfumo wao wa mashambulizi ya anga’’anaeleza Sgt Mykhailo Shamanov, msemaji wa uongozi wa jeshi la jiji la Kyiv.

Huku akisema Urusi inajaribu kushambulia mitambo ya kijeshi, "lengo kuu ni kuwatisha raia".

Wanajua kuwa Urusi itaendeleza mashambulizi,alieleza ndio maana serikali yake inaomba mara kadhaa ulinzi wa anga kutoka kwa washirika wa magharibi.

Ndio sababu hasa Ukraine inashauku ya kuona hatua za rais Mteule wa Marekani Donald Trump mara atakapoanza kazi.

Hata kama ulinzi wa anga utakuwa na ufanisi,ndege zisizo na rubani au makombora yataanguka kwenye jiji hilo.Husababisha moto,uharibifu na bahati mbaya wakatimwingine waathirika,alieleza

"Kila usiku tunabahatisha – inaposhambulia,inaposhambuliwa inapoangukia na yatakayotokea baada ya hapo.

Vitaliy na watu wake hawana nafasi maalum - silaha zao za kuwaangusha wapiganaji hubebwa nyuma ya lori, na kuwaruhusu kutekeleza kwa haraka.

Tunajaribu kufuatilia, kusonga mbele, kuikabili ndege isiyo na rubani, n ahata kuiteketeza," alisema.

Ni wazi kwamba kazi inazidi kuwa ngumu.

"Nusu mwaka uliopita, ilikuwa ndege 50 zisizokuwa na rubani kwa mwezi.

Sasa idadi imepanda 100, kila usiku," alisema.

Siku zao pia zinaongezeka pia. Wakati Warusi wakitumia zaidi makombora kushambulia Ukraine, kamanda wa kitengo alisema, tahadhari hizo za anga zingechukua saa sita. "Sasa, ni karibu saa 12 au 13," alisema.

Vitaliy anajiamini mbele ya jeshi lake akitangaza kwamba watamudu mashambulizi yote kutoka kwa Urusi ikiwa watapata silaha kutoka kwa washirika wao mataifa ya magharibi.

‘’Wanajeshi wetu wanaweza kupambana na ndege 250 zisizo na rubani kwa usiku mmoja tu ‘’alieleza

Hata hivyo ulinzi wa anga unaweza kufanya kwa ufanisi Zaidi.Waukraine wataendelea kuteseka hadi pale Urusi itakapositisha uvamizi wake na mashambulizi ya anga katika miji.

Viktoria anasema maisha yao sasa yamegawanyika kabla na baada ya kifo cha binti yao. Wanakaa na rafiki baada ya kuharibiwa kwa ghorofa yao; alisema wanalala kwenye korido usiku ili kujikinga na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani.

"Bila shaka inachosha," alisema. "Lakini inaonekana kwa upande wangu inawafanya watu kuwa na hasira zaidi, inakera na kuwakasirisha. Kwa sababu watu kwa kweli hawawezi kuelewa, hasa hivi karibuni, mashambulizi yale ambayo yamekumba nyumba zilizokuwa na amani.”

"Sielewi hata kidogo kwa nini vita hivi vilianza na kwa nini," babake Maria, Volodymyr, aliiambia BBC. “Ina maana gani? Sio kwa mtazamo wa kiuchumi, wala kibinadamu, hata kieneo - watu wanakufa tu."

"Ni 'malengo ya watu wasio na akili’’

Imetafsiriwa na Martha Saranga