Sahau kuhusu Mwakinyo haya ni mapambano 5 ya ngumi duniani yaliyomalizika 'kiajabu'

Na Yusuph Mazimu, BBC Swahili

Usiku wa kuamkia Jana bondia namba moja Tanzania Hassan Mwakinyo amepoteza moja ya mapambano muhimu dhidi ya Muingereza Liam Smith, kwenye uzito wa Super welterweight.

Pambano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa M& S Bank Arena katika jiji la Liverpool, Uingereza lilimalizika kiajabu katika raundi ya nne baada ya Mwakinyo kupiga goti mara mbili wakati akiwa hashambuliwi, na kusababisha refa kumaliza pambano.

Wengi wameshangazwa, na hawakujua nini kimemkuta Mwakinyo aliyeonekana kulimudu vyema pambano hilo mpaka kufikia wakati huo.

Mpizani wake Smith baada ya pambano hilo hakuonekana kushangilia akisema hajafurahishwa, akisema mpinzani wake amekimbia ulingoni na zaidi amesikitishwa na alichokifanya Mwakinyo.

"Sijui nini kimetokea, nadhani amesalimu amri, sijafurahishwa, sijawapa mashabiki umaliziaji mzuri lakini kilichotokea kiko nje ya uwezo wangu, najua wengi hawapendi kusikia, lakini nipeni mapambano ya maana (sio haya)" alisema Smith.

Mwakinyo alionekana kutema kinga meno (mouythshied) ambayo kisheria ni lazima bondia avae wakatiwote wa pambano. Lakini muamuzi akigundua imetemwa kwa makusudi alama hukatwa kwa bondia aliyetema.

Katika ukumbi huo mkubwa walijazana mabondia wengi wakubwa wa zamani wa uzani huo ambao wengi wamemkosoa Mwakinyo kukimbia Pambano.

Lakini Mwakinyo huku akilia kwa uchungu kwa kilichotokea wakati akizungumza na mwandishi wa BBC, Salim Kikeke amewaomba msamaha watanzania,

“Najua imeumiza Watanzania wengi lakini na mie pia imeniumiza sana kwasababu sipendi kupoteza kabisa katika maisha yangu, ipo nje ya uwezo wangu naombeni mnisamehe sana ambao nimewaumiza lakini Promota ameahidi pambano litarudiwa”.

Sababu anayoitaja Mwakinyo ni kwamba, begi lake lilisahaulika katika uwanja wa ndege wa Amsterdam wakati akitokea Marekani kwenda Uingereza, hivyo alilazimika kutumia viatu vingine ambavyo vilikuwa vinamfinya na kumsababishia maumivu ya kifundo cha mguu (enka). Sababu ambayo sio wote wamekubaliana nayo.

Kupitia mtandao wake wa twitter Mwakinyo amesema pambano lake na Smith litarudiwa mwezi Januari mwakani.

Lakini hili ni pambano moja tu lililoisha ‘kimajaabu’ na kushangaza lakini yako mengi aliyowahi kumalizika kwa mshangao, matano kati yao ni haya; 

5: Bernard Hopkins vs Robert Allen

Lilikuwa pambano la ngumi kati ya Bernard Hopkins na Robert Allen lililofanyika Agosti 28, 1998.

Pambano hili lilikuwa lakushikana sana tangu raundi za mwanzo. Muamuzi wa pambano hili Mills Lane, alikuwa akiiingilia kati mara kwa mara kuwaachanisha mabondia hao wasishikane.

Lakini walipozidi kushikana, alijikuta akiwaachanisha kwa kuwasukuma kwa nguvu kitendo kilichomfanya mmoja wa mabondia Hopkins kudondoka nje ya ulingo kabisa na kuteguka ‘enka’, alianza kulia na kulalamika kuumia na hapo ukawa mwisho wa pambano hilo ambalo halikuwa na mshindi.

4: Evander Holyfield v Mike Tyson

Hili ni pambano maarufu zaidi, kwa sababu liliwahusisha pia mabondia maarufu zaidi wa uzito wa juu katika kizazi chao.

Linafahamika kama ‘The Bite fight’, kwa sababu ya kitendo cha Tyson kumng’ata sikio Evander mara mbili katika raundi ya tatu, na muamuzi kuamua kumaliza pambano.

Ilikuwa June 28, 1997 pambano la kuwania mkanda wa ubingwa wa dunia wa WBA.

3: Adolpho Washington vs Virgil Hill

Lilikuwa pambano kati ya Adolpho Washington na bingwa wa dunia wa WBA uzito wa Light Heavyweight Virgil Hill lililofanyika mwaka1993. Katika raundi ya 11 Washington akakutana na kisa cha kushangazwa alipojigonga kwenye kamera za Televisheni zilizokuwa zikichukua matukio ya pambano hilo na kushindwa kuendelea, na hivyo Hill kutetea mkanda wake.

Ilikuwa wakati wa mapumziko kwenye raundi hiyo ya 11, ili kuingia raundi ya 12, wakati watu wa kamera wakisogeza kamera yao karibu na yeye kama ilivyo kawaida wakati wa mapambano ya ngumi bahati mbaya alijigonga na kuumia jichoni.

2: Lennox Lewis vs Oliver McCall II

Lilikuwa pambano la pili lililopigwa Februari 7, 1997 kuwania ubingwa wa dunia wa mkanda wa WBC katika ukumbi wa Las Vegas Hill, Marekani. Lilikuwa moja ya mapambano ya ngumi ya uzito wa juu yaliyomalizika kwa kushangaza na kupewa jina la "Payback or Playback".

Lilipewa jina hilo kwa sababu ya Oliver McCall kuingia ulingoni na kuanzia raundi ya nne akaamua kutorusha ngumi kabisa. Mpaka raundi ya tatu alirusha ngumi 26. Baada ya raundi ya tatu alikataa kurudi kwenye kona yake, akagoma kusikiliza maelekeo ya mwalimu wake George Benton na ilipoanza raundi ya nne, ndipo alipoamua kuzunguka ulingoni na kutopigana.

Alionekana kama amesusa, hataki kupigana, alikuwa akiangalia pembeni, hamuangalii mpinzani wake, akirushiwa konde anakinga tu anarudi nyuma na kutembea tu ulingoni.

Watu wakaanza kurusha maneno ‘rudisha pesa ama jibu mapigo' na hapo ndipo jina la "Payback or Playback" liliboibuka.

Kumalizika kwa raundi ya nne, muamuzi akawa anampeleka kwenye kona yake kujua nini kimetokea, McCall alikuwa akilia tu. Muamuzi na watu wa kona yake wakamuuliza kama anataka kuendelea, alikubali kuendelea, lakini ilipoanza raundi ya tano, aliendelea na mtindo ule ule wa kutembea na kutopigana.

Lewis aliendelea kumrushia makonde tu, muamuzi aliamua kumaliza pambano, kwa sababu halikuwa pambano la ngumi, bali pambano na mrusha ngumi na mkinga ngumi.

Kabla ya pambano hilo McCall alikamatwa kwa kushitakiwa kwa kosa la kuharibu mali na kukataa kukamatwa. Ilionekana anapitia masahibu mengi. Siku chache baada ya pambano hilo ikagundulika alikuwa na msongo wa mawazo na kupelekwa Hospitali kwa matibabu.

1: Steve McCarthy vs Tony Wilson

Hili ni pambano lililoisha kimaajabu. McCarthy alionenekana kufanya vyema katika pambano hili ambapo katika raundi ya tatu alifanikiwa kumuangusha Wlison.

Wakati pambano likiendelea katika dakika za mwisho kabisa, Wilson akiwa anashambuliwa kwenye kamba, mama yake aliyeitwa Minna Wilson aliyekuwa na umri wa miaka 62 (uchungu wa mama), hakupenda kushuhudia mwanae akichapwa.

Akavua kiatu (skuna) kilichokuwa na kisigino krefu akapanda ulingoni na kuanza kumshambulia McCarthy kwa kiatu. Kukazuga zogo na kumfanya McCarthy kuondoka ulingoni akiamini ameshinda kwa kuwa mama yake na mpinzani wake ameleta vurugu.

Lakini muamuzi Andrian Morgan alimwambia arudi wamalizie pambano, McCarthy aligoma na kwa mshangao wa wengi akampa ushindi Wilson. Kukazuka vurugu ukumbini huku mama yake Wilson akiburutwa nje kwa kuvutwa nywele na watu wa usalama.

McCarthy alikuja kushonwa nyuzi nne kwa majeraha ya kupingwa na kiatu.