Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Arteta analipa gharama kubwa kwa kutotibu udhaifu wa Arsenal'
- Author, Phil McNulty
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Hatua ya Arsenal ya kutolewa katika raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United kwa mikwaju ya penalti, ilikuwa ni mwendelezo wa kichapo, baada ya kufungwa mabao 2-0 nyumbani na Newcastle United siku ya Jumanne, kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Carabao.
Kwa sasa Arsenal wako nyuma ya vinara wa Ligi Kuu ya England, Liverpool kwa pointi sita wakiwa wamecheza mchezo mmoja zaidi.
Kukosa kununua wachezaji sahihi kumepunguza makali ya Gunners na kuwa kisu butu kisicho na makali, udhaifu ambao uko dhahiri.
Arsenal imekuwa timu bila mshambuliaji anayetambulika kwa muda sasa, na ni jambo ambalo Arteta amekataa kulishughulikia, badala yake alichagua kuimarisha maeneo mengine na kulisahau eneo hilo.
Na sasa, wametoka kwenye Michuano ya FA, wanakabiliwa na pambano huko Wembley kwenye Kombe la Carabao na wanatatizika kuendelea kuifukuzia Liverpool kwenye mbio za ubingwa wa England, kushindwa kwa Arteta na Arsenal kusajili mfungaji ndio tatizo.
Udhaifu wa Arsenal
Soma takwimu za michezo miwili iliyopita ambayo wamefungwa. Walipiga mashuti 23 na matatu pekee ndio yalilenga lango dhidi ya Newcastle, na mashuti 26 huku saba pekee ndio yakilenga lango dhidi ya Manchester United ndani ya dakika 120. Na bao pekee katika michezo yote miwili lilitokana na shuti lililofumuliwa na beki Gabriel.
Udhaifu wa Arsenal ulionekana msimu uliopita, lakini nafasi ya kujaribu kutatua tatizo hilo ilipita bila kutumiwa katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.
Mchezaji wa RB Leipzig, Benjamin Sesko alitajwa kama shabaha ya kununuliwa kwa pauni milioni 55, na Viktor Gyokeres kutoka Sporting lilikuwa jina lingine kwenye mpango huo.
Badala yake, Arteta alianza kuimarisha safu ya ulinzi ya Arsenal kwa kumsajili mchezaji wa kimataifa wa Italia, Riccardo Calafiori kutoka Bologna kwa mkataba wa pauni milioni 42, kisha akamuongeza kiungo wa kati wa Real Sociedad, Mikel Merino, kwa pauni milioni 32.6.
Nyongeza pekee ya mashambulizi katika siku ya mwisho ni ununuzi ni Raheem Sterling, alijiunga na Arsenal kwa mkopo katika dakika za mwisho za dirisha la usajili la majira ya kiangazi. Amecheza mechi 12, akifunga bao moja.
Kai Havertz ametumika kama mshambuliaji lakini hili si jukumu lake la asili. Amekuwa ni nembo ya makosa ya Arsenal, akikosa nafasi za wazi dhidi ya Newcastle na Manchester United. Mjerumani huyo hata alikosa penalti muhimu kwenye mikwaju ya penalti.
Alipiga mashuti matano ndani ya eneo la hatari la Manchester United. Na akakosa bao la wazi dakika za lala salama dhidi ya Newcastle siku ya Jumanne.
Huku hatima ya Arteta ikiwa haijuulikani, kuna jeraha la muda mrefu la Bukayo Saka na mshambuliaji mwenzake Ethan Nwaneri mwenye umri wa miaka 17.
Na kufanya mambo kuwa mabaya zaidi Gabriel Jesus, hajafanya mambo makubwa lakini angalau ndio mchezaji anayemudu maeneo ya kati, alitolewa nje kwa machela katika kipindi cha kwanza dhidi ya Manchester United.
Arteta alieleza jambo baada ya kutolewa katika Kombe la FA: "Kuna shida kuhusu kutoweka mpira wavuni. Mpira lazima uingie wavuni kisha umshinde mpinzani. Huo ndio ukweli."
Mshambulizi wa zamani wa Arsenal na Uingereza Theo Walcott aliiambia BBC Sport: "Kila mtu ameshasema. Arsenal inahitaji mshambuliaji na itakuwa na matokeo tofauti kabisa."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi