Je, Arsenal itaipiku Man City na Liverpool na kunyakua taji?

    • Author, Gary Rose
    • Nafasi, BBC

Arsenal imepata ushindi wa sita mfululizo kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, wamefunga mabao 25 katika mechi hizo na wamefungwa mabao matatu pekee - wako kwenye jitihada za kuwania taji na wanaonekana kudhamiria kulinyakua.

The Gunners, walikuwa katika kiwango kama hicho mwaka jana kabla ya kuporomoka, lakini sasa wanaonyesha njaa na ustahimilivu unaoashiria kuwa wamedhamiria kutorudia makosa ya hapo awali.

Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard aliiambia TNT Sports wakati timu yake ikiwa nyuma kwa pointi mbili nyuma ya vinara Liverpool katika nafasi ya tatu:

"Unaona kila wiki jinsi ushindani ulivyo na hapo ndipo tunapotaka kupigania mataji."

Wakati Arsenal wameshinda kila mechi ambayo wamecheza kwenye Ligi ya Premia mwaka 2024, walishindwa na Porto katika mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa katikati ya juma, wakiruhusu bao la dakika za lala salama.

Lakini walijibu kwa ushindi wa mabao wa mabao 4-1 dhidi ya Newcastle siku ya Jumamosi.

Mlinzi wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand anasema, "la msingi ni kuhakikisha hawaruhusu hofu kuwaingia. Lakini hakuna dalili kwamba wana hofu kwa sasa. Ni timu yenye mafanikio na yenye umoja kwa sasa.’’

Odegaard aliongeza: "Mwaka mmoja kabla tulikosa kucheza Ligi ya Mabingwa na tumejerea na nguvu zaidi. Msimu uliopita tulikosa taji na sasa ni wakati wa kuonyesha kwamba tumejifunza."

Arsenal iliyovunja rekodi

Arsenal imekuwa timu ya sita kushinda mechi zao sita za kwanza za Premier League katika msimu.

Idadi ya mabao 25 katika mechi sita ndiyo mabao mengi zaidi ambayo timu yoyote imefunga mwanzo wa msimu kwa mechi sita kwenye Ligi Kuu.

Kwa mara ya kwanza katika historia yao, Arsenal wameanza msimu kwa kushinda mechi sita mfululizo kwenye ligi.

Bukayo Saka amefunga katika mechi tano mfululizo za ligi kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya soka.

Ndiye mchezaji wa kwanza wa Uingereza kufunga katika mechi tano mfululizo za Premier League akiwa na Arsenal tangu Ian Wright (aliyeshinda 7 kati ya Septemba na Novemba 1994).

Saka anaongoza

Matokeo ya kuvutia ya Arsenal 2024 yametokana pia na juhudi Bukayo Saka. Mshambulizi huyo wa kimataifa wa Uingereza alifunga bao la tatu la The Gunners na kufikisha jumla ya mabao 16.

Ilikuwa ni mechi ya tano mfululizo ya Ligi Kuu ya Uingereza kufunga. Pia alishinda magoli mawili mawili katika ushindi wa 6-0 dhidi ya West Ham na ushindi wa 5-0 dhidi ya Burnley.

"Nimefurahishwa na bao jingine leo na muhimu zaidi tumepata ushindi. Ninafanya kazi kwa bidii kila siku na kuonyesha ubora wangu. Ni wazi kuwa niko na wachezaji wenzangu wazuri wanaonipa pasi nzuri, ambazo zinasaidia pia,’’ alisema Saka.

"Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii na tunahitaji tu kuendelea na mtindo huu."

Ushindi huo wa Arsenal uliwasogeza hadi pointi moja nyuma ya mabingwa watetezi Manchester City, ambao wanashika nafasi ya pili, na pointi mbili nyuma ya vinara Liverpool. Huku kukiwa na michezo 12 iliyosalia.

Mwanzo mzuri kwa Arsenal

Mchezaji wa zamani wa the Gunner, Ian Wright anasema, “wako vizuri, wanajifunza kutoka msimu uliopita, wanapaswa kuendelea kufanya wanachofanya. Arsenal wanafunga mabao kushoto, kulia na katikati.”

"Arsenal mwaka huu wako tofauti, na nadhani watafanya kila wawezalo kuwafikia Liverpool na Manchester City. Itakuwa moja ya mbio bora za ubingwa kwa muda mrefu."

Beki wa zamani wa Arsenal, Martin Keown aliongeza, "ni lazima kushinda kila wiki. Zimesalia mechi 12 na lazima ushinde kila mechi - kuna michezo mikubwa inakuja."

Mkufunzi wa Arsenal, Mikel Arteta anasema, “kwa kweli tuna furaha, tunatakiwa kuendelea kufanya mambo mazuri tunayoyafanya.”

"Bado kuna mambo ambayo tunaweza kuyafanya vizuri zaidi, wakati huu wachezaji wakubwa waliokuwa na majera wanarudi uwanjani, hivyo ni faida kwetu.

"Mchezo wetu na Porto tulikuwa sisi bila mpira. Lilikuwa somo kubwa na unajifunza mengi katika nyakati kama hizo."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi