Wanaanga wawili wanaojiandaa kurejea duniani baada ya miezi 9 kukwama angani ni akina nani?

Chanzo cha picha, Fish trap
Sunita "Suni" Williams na Barry "Butch" Wilmore walianza safari yao ya anga mnamo Juni 2024, wakipanda chombo cha angani cha majaribio kilichoundwa na Boeing, wakiwa wanatarajia kukaa kwenye Stesheni ya Anga ya Kimataifa (ISS) kwa siku nane.
Chombo hicho cha anga, kinachojulikana kama Starliner, kilitengenezwa na Boeing kwa ajili ya NASA, na safari hiyo ilikuwa ni ya kwanza kwao wakiwa na wafanyakazi wa anga.
Lakini matatizo yalijitokeza haraka. Kulikuwa na matatizo na vichochezi (thrusters) vinavyosukuma chombo, pamoja na uvujaji wa gesi ya heliamu inayotumika kuweka mafuta kwenye mfumo wa kusukuma.
Wakati NASA ilipokuwa ikichanganua matatizo ya kiufundi, kurudi kwa wanaanga hao kulicheleweshwa tena na tena. kuwa walikuwa "wamekwama" kwenye stesheni ya anga kwa karibu miezi tisa.
Lakini, ingawa hali hii ni ya kushangaza, siyo hali kama ile ya Robinson Crusoe. Wanapata rasilimali zote za msaada kutoka NASA, na Williams na Wilmore ni wana anga wawili waliobobea, wakiwa na saa nyingi za safari za anga, wanadai kuwa wamefundishwa "kutegemea yasiyotarajiwa."
Wamejitolea kwa shauku kufanya utafiti wa kisayansi na kudumisha ISS kwa njia ambayo wanaanga wote wanaoishi humo huchangia.
Wanaanga hawa ni kina anani?
Sunita "Suni" Williams, mwenye umri wa miaka 58, ni mtoto wa baba Mhindi na mama Mslovenia. Alikamilisha masomo yake katika Chuo cha Naval cha Marekani na kupata shahada ya Sayansi mwaka 1987, kisha alifanya shahada ya uzamili katika Usimamizi wa Uhandisi katika Taasisi ya Teknolojia ya Florida.
Alichaguliwa kuwa mwana anga na NASA mwaka 1998 na ni mzoefu wa misheni mbili za anga kabla ya kukaa kwake sasa kwenye Stesheni ya Anga ya Kimataifa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pia amefanya kazi Moscow na Shirika la Anga la Urusi, Roscosmos, kwenye masuala ya mchango wa Urusi kwenye stesheni ya anga.
Ameongeza maarifa yake kwa kufanya kazi katika idara ya roboti. Williams alikaa angani kwa jumla ya siku 322 katika misheni mbili zake za awali.
Amefanya matembezi tisa angani,rekodi kwa mwanamke, na yeye ni mwanaanga wa pili wa kike mwenye muda mrefu zaidi wa matembezi angani, akiwa na jumla ya saa 50 na dakika 40.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Barry "Butch" Wilmore, mwenye umri wa miaka 61, alipata Shahada ya Sayansi na Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uhandisi wa Umeme kutoka Chuo Kikuu cha Tennessee Tech na Shahada nyingine ya Uzamili ya Sayansi katika Mifumo ya Anga kutoka Chuo Kikuu cha Tennessee.
Ana uzoefu mkubwa wa kijeshi, akiwa afisa na mpigaji ndege katika Jeshi la Wanamaji la Marekani, akiwa na zaidi ya saa 8,000 ya ndege na kutua kwa ndege kwenye meli 663.
Alichaguliwa kuwa mwanaanga na NASA mwezi Julai mwaka 2000 na ni nahodha aliyejitoa katika Jeshi la Wanamaji la Marekani.
Butch ni mzoefu wa safari mbili za anga na amekusanya jumla ya siku 178 angani, kulingana na NASA. Hata hivyo, idadi hii itazidi kwa kiasi kikubwa kwani muda wa misheni yake ya mwisho bado haujaongezwa.
Katika misheni yake ya mwisho, alihudumu kama mhandisi wa ndege kwa Expedition 41, na alichukua uongozi wa ISS alipotua kwa ajili ya timu ya Expedition 42.
Alirudi duniani kutoka kwenye misheni hiyo mnamo Machi 2015. Wakati wa misheni hiyo, alikusanya jumla ya siku 167 angani na alifanya matembezi manne angani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Walikuwa wakifanya nini muda wote huu?
Misheni nyingi za anga huchukua takribani miezi sita, hivyo kukaa zaidi ya miezi tisa kwenye kituo cha anga, ISS ni jambo lisilo la kawaida, hasa ikiwa ulikuwa unatarajia kukaa kwa siku nane tu.
Hata hivyo, NASA na wanaanga wameshajiandaa kwa kila hali inayoweza kutokea.
"Hivyo ndivyo safari za anga za binadamu zilivyo, kupanga kwa ajili ya dharura zisizotarajiwa na ndivyo tulivyofanya," alisema Butch Wilmore katika mahojiano ambayo shirika liliyatangaza moja kwa moja tarehe 4 Machi.
NASA ilisema imepeleka safari mbili za usambazaji kwenye kituo cha anga ISS, zikiwa na chakula, maji, nguo na oksijeni. Zaidi ya hayo, kundi jipya la wanaanga limejiunga na wafanyakazi wa stesheni, chini ya kamanda Nick Hague.

Chanzo cha picha, Reuters
Hague alisema katika mahojiano ya tarehe 4 Machi kwamba misheni ya stesheni ya anga ni "kitu tunachokiamini kwa undani," akiongeza kuwa inawalazimisha kukubaliana na hatari za uchunguzi wa anga.
Kwa upande wao, Williams na Wilmore wameweza kuzoea vyema kwa misheni yao iliyoongezeka. Hawako kwenye likizo. Wanaanga huwa na shughuli nyingi, wakisaidia operesheni tata ya stesheni.
Walifanya matembezi angani pamoja na wamefanya majaribio kadhaa ya kisayansi. Utafiti wao unajumuisha uchunguzi wa jinsi mimea inavyokua angani, kufuatilia jinsi mwili wa binadamu unavyokabiliana na hali ya kutokuwa na uzito, na hata jinsi ya kupanda chakula.
Ni ratiba ambayo Wilmore huanza saa 10:30 alfajiri na Williams huanza saa 12:30 asubuhi. Wote pia hufurahia mazoezi ya kila siku kwa saa mbili au zaidi, ambayo ni muhimu kupambana na kupunguza uzito mifupa unapokuwa angani.

Chanzo cha picha, Reuters /NASA
Athari za binafsi za maisha angani
Licha ya kuwa na shughuli nyingi na majukumu yao kwenye ISS, Williams na Wilmore wanakiri kwamba haya yamekuwa ni nyakati changamano. Haswa katika suala la familia.
Suni Williams anasema kwamba matukio haya yamekuwa katika "mchanganyiko wa hisia" kwa familia zao, kutokana na kutokuwa na uhakika wa lini wataweza kurudi.
Hilo limekuwa jambo gumu zaidi, anasema.
Mara watakaporudi, wataingia katika kipindi kirefu cha kuzoea tena, alisema Dr. Simeon Barber wa Chuo Kikuu cha Open, Uingereza, alipozungumza na BBC.
"Unapopelekwa kwenye safari ya kazi inayotarajiwa kudumu wiki moja, huwezi kutarajia itachukua sehemu kubwa ya mwaka," alisema.
Lakini pia alizungumzia juu ya hisia kubwa ya uwajibikaji, kama vile kumsaidia mwenzake kuvaa mavazi yake ya kutembea angani na kisha kufungua mlango ili kumrudisha ndani. Hilo ndilo lilikuwa ni jambo la fahari zaidi, alieleza.














