Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi watawala wa Iran walivyojenga mfumo wa kuwaweka madarakani
- Author, Luis Barrucho
- Nafasi, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Zaidi ya miongo minne baada ya Mapinduzi ya mwaka 1979 kuwaleta watawala wa Iran madarakani, sasa wanakabiliwa na wakati mbaya zaidi kuwahi kutokea.
Mashambulizi ya pamoja ya anga ya Marekani na Israel yamemuua Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei na makamanda wengine wakuu wa kijeshi, pamoja na kuharibu miundombinu muhimu.
Marekani na Israel zote zimeashiria kwamba zinataka mabadiliko ya utawala, na kuwataka Wairani kupindua serikali yao.
Hata hivyo wataalamu wanasema uongozi wa Iran kwa kukusudia umetengeneza utawala wenye nguvu wa kudumu na ambao hauwezekani kupinduliwa kwa urahisi.
Lakini, nini kimewezesha uthabiti wake, na ni tofauti gani na nchi zingine za Mashariki ya Kati?
Muundo wenye msingi wa: 'Unakata kichwa kimoja, vipya vinachipuka'
Tangu kupinduliwa kwa utawala wa kifalme wa Iran, Jamhuri ya Kiislamu imeendelea kujenga mfumo wa kisiasa uliopangwa kunusuru majanga kama majaribio ya mapinduzi, wanasema wataalam.
Hii inajumuisha taasisi inayodhibitiwa vilivyo, ufundishaji wa kiitikadi, mshikamano wa wasomi na upinzani uliogawanyika.
Ni muundo wenye msingi wa: "Unakata kichwa kimoja, vipya vinachipuka," anasema Sébastien Boussois, mtafiti wa Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Kisiasa ya Ulaya nchini Ubelgiji.
Ni muundo wa utawala wenye uwezo wa kubadilika, na kudumu hata wakati uongozi wao umesambaratishwa.
Siku ya Jumapili, Mojtaba Khamenei, mtoto wa Ali Khamenei, alichaguliwa kama mrithi wake, chini ya wiki mbili baada ya baba yake kuuawa.
Anatarajiwa sana kuendeleza utawala wenye msimamo mkali wa baba yake.
'Utawala wa Kiimla'
Wataalamu wanahoji kuwa, tofauti na nchi kama vile Tunisia, Misri na Syria, ambako viongozi walipinduliwa, Iran imeweza kukabiliana vyema na mitikiso ya nje ya aina hiyo kwa sababu ya vyombo vyake vya usalama vinavyoendeshwa na itikadi.
Badala ya kufanya kazi chini ya udikteta wa kawaida unaohusisha mtu mmoja, Iran ina "utawala wa kiimla wenye kujuisha watu wengi" - "muungano kati ya wafuasi wanaoamini uongozi wa Uislamu katika siasa na utaifa wenye msimamo mkali wa Iran," anasema Bernard Hourcade, mkurugenzi wa zamani wa Taasisi ya Utafiti ya Ufaransa yenye makao yake Tehran nchini Iran.
Mamlaka imegawanyika katika vituo vingi - vyombo vya kidini, vikosi vyenye kujihami, na sehemu kubwa za uchumi - na kuufanya kuwa mfumo mgumu zaidi kuuangusha kuliko udikteta wa kiongozi mmoja.
Mashirika mengine yenye nguvu ni pamoja na Baraza la Uongozi, ambalo linaweza kupiga kura kwa ajili ya sheria na wagombea wa uchaguzi.
Hii inapunguza zaidi uwezekano wa kundi lolote moja kuanzisha pingamizi kubwa dhidi ya serikali.
Wakati Iran inachukuliwa kwa kiasi kikubwa kama utawala wa kiimla, inatoa fursa kwa Wairani ya kupiga kura katika baadhi ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na uteuzi wa rais.
Hata hivyo, mchakato huo unadhibitiwa kwa ukaribu, na wagombea wanachunguzwa na Baraza la Uongozi kwa vigezo ikiwa ni pamoja na kujitolea kwao kwa Jamhuri ya Kiislamu.
Jukumu muhimu la Kikosi cha Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC)
Taasisi hiyo hutoa kanuni za msingi zinazodumisha mfumo wa kisiasa, na kikosi hicho cha usalama kinaonekana kuwa chenye 'nguvu'.
Kikosi cha Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC), kinafanya kazi pamoja na jeshi la kawaida na mara nyingi huchukuliwa kuwa ndiyo "msingi wa utawala", anasema Hourcade.
Zaidi ya jukumu lake la kijeshi, taasisi hii imekuwa na nguvu ya kisiasa na kiuchumi, yenye maslahi makubwa ya kibiashara na ushawishi kupitia wanamgambo wa Basij, shirika la kujitolea.
Muhimu zaidi, vikosi vya usalama vimebakia kuwa na umoja licha ya machafuko ya mara kwa mara. Boussois anaunganisha uaminifu huu na itikadi.
"Utamaduni huu wa kufa kama shahidi miongoni mwa Washi'a [wafuasi wa moja ya matawi mawili makuu ya Uislamu] na ndani ya makundi kama Hamas na Hezbollah yanachukuliwa kuwa sehemu ya kazi", anasema.
Naibu waziri wa ulinzi wa Iran, Reza Talaeinik, hivi karibuni alisema katika mahojiano ya televisheni kwamba kila kamanda wa IRGC ana mrithi aliyeteuliwa wakiwa safu tatu chini yake ili kuhakikisha mwendelezo.
Kasra Aarabi, mkuu wa utafiti kuhusu jeshi la Iran wa shirika la United Against Nuclear Iran, anasema muundo wa Iran uliogatuliwa ulitokana na mafunzo kutokana na kuanguka kwa vikosi vya Iraq mwaka 2003 wakati wa uvamizi wa muungano unaoongozwa na Marekani.
Ikiwa utawala utasalia, anaamini "Jeshi litakuwa na jukumu muhimu zaidi".
Mitandao ya ufadhili na mshikamano wa wasomi
Sehemu kubwa za uchumi wa Iran zinadhibitiwa na mashirika yaliyounganishwa na serikali kama vile bonyads – shirika la hisani ambalo limebadilika na kumiliki maelfu ya makampuni katika sekta mbalimbali za uchumi.
Mitandao hii inasambaza kazi na kandarasi kwa maeneo bunge ambayo ni waaminifu kwa serikali.
Himaya ya biashara ya IRGC, ikijumuisha muungano wa Khatam al Anbia, inaimarisha mfumo huu wa "ufadhili" wa biashara.
Ingawa vikwazo vya Magharibi vimeathiri uchumi mpana zaidi wa Iran, mitandao hii inasaidia kuwaweka wasomi wakuu na kulinda hisa zao katika kuendelea kwa mfumo huo, wataalam wanasema.
Kulingana na Boussois, mfumo huo "ni thabiti kiasi kwamba ni vigumu kuona kasoro zozote".
Itikadi na mapinduzi yaliyoleta mabadiliko
Dini pia ina nafasi kubwa katika kuhifadhi mamlaka.
Mapinduzi hayo yaliunda mtandao wa kudumu wa taasisi za kidini, kisiasa na kielimu ambazo zinaendelea kuunda mtazamo wa ulimwengu wa serikali.
"Muundo huu wa zamani sana, wenye nguvu kweli - wa kiitikadi, wa urasimu, wa kiutawala - unafanya mfumo kuwa imara," anasema Boussois.
Anasema itikadi "inakuwa kama chanzo halisi cha umoja, wito na usajili".
Upinzani uliogawanyika
Kihistoria, upinzani wa Iran umesambaratika.
Wanajumuisha wanamageuzi, wafalme, vikundi vya mrengo wa kushoto, vuguvugu la wanaoishi nje ya nchi kama vile Baraza la Kitaifa la Upinzani wa Iran, na mashirika mbalimbali ya kikabila.
Mgawanyiko huu umedumu kwa muda mrefu, anasema Ellie Geranmayeh, mshirika mkuu wa sera katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni, taasisi ya wataalam ya Uingereza.
Baada ya mapinduzi, mjadala kuhusu kuunda vyama vya siasa uliwekwa kando, anasema, kwa kiasi kikubwa kutokana na Iran kuingia katika vita na Iraq mwaka 1980, ambavyo vilidumu kwa karibu miaka minane.
Geranmayeh anasema kwamba katika nyakati tofauti, wapinzani wa makundi mblimbali ya msimamo wa wastani "yametengwa, kudharauliwa au kufungwa" na taasisi za utawala na makundi yenye misimamo mikali.
Kwa miaka mingi kumekuwa na vuguvugu kubwa la kupinga utawala huo, kama vile Vuguvugu la Kijani la 2009 na maandamano yaliyochochewa na kifo cha Mahsa Amini mwaka 2022.
Lakini maandamano hayo yalikosa uongozi thabiti na yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa serikali.
Hata hivyo, wimbi la hivi punde la maandamano mwaka huu na mwaka jana lilifuatia wito wa mwana wa marehemu shah aliyeuhamishoni wa "siku ya utekelezaji duniani" yaani "global day of action".
Iran pia inaendesha mojawapo ya mifumo ya uchunguzi wa hali ya juu zaidi katika kanda, yenye kuzima mtandao mara kwa mara, ufuatiliaji unaowezeshwa na AI na vitengo vya mtandao vinavyolenga wanaharakati nje ya nchi.
Tahadhari ya umma na kwanini unasambaratika
Kwa miaka mingi, Wairani wengi walisita kushinikiza mabadiliko ya utawala baada ya kushuhudia kusambaratika kulikochangiwa na uingiliaji kati ulioongozwa na Marekani nchini Afghanistan na Iraq, Geranmayeh anasema, akiongeza kuwa matokeo ya vuguvugu la Waarabu yalizidisha tahadhari.
Lakini anasema hili sasa limebadilika, huku Wairani wengi wakihisi kuwa serikali haiwezi tena kutoa mahitaji ya kimsingi, kuanzia ajira hadi maji safi, huku wakiongeza nguvu ya kikatili kukandamiza upinzani.
Ukandamizaji wa kikatili wa Januari dhidi ya wimbi jipya la maandamano - ambapo maelfu waliuawa kufuatia baadhi ya maandamano makubwa kuwahi kuonekana nchini - uliharakisha mabadiliko haya, anaongeza.
Hourcade inasema kuna "pengo la kiumri" kati ya Wairani na mtazamo wao kwa serikali.
Wairani wenye umri mdogo, ambao wengi wao wameelimika sana, wameunganishwa kimataifa na kushawishiwa na mitandao ya kijamii, wanaukataa utawala huo, wakiuona kuwa "ufisadi, dhuluma na usio na umuhimu kwa matarajio yao", anasema
'Kila utawala hatimaye huanguka'
Wachambuzi wanasema kuwa serikali za kidikteta huwa zinaanguka wakati hali tatu zinapotokea kwa wakati mmoja: uhamasishaji mkubwa wa watu, mgawanyiko katika uongozi na kujiondoa kwa vikosi vya usalama.
Wataalam wanasema kwamba zamani, Iran mara nyingi ilipakutana na hali ya kwanza lakini sio hali nginine mbili.
Hourcade anaamini mwisho wa Jamhuri ya Kiislamu ni jambo lisiloepukika, lakini sio karibu.
"Kila utawala hatimaye huisha. Swali ni wakati gani – na mpangilio."
Anasema kuwa kifo cha Khamenei kilikuwa pigo kubwa kwa utawala.
"Hakutakuwa na mwingine kama yeye. Mbadala wake hautakuwa na mamlaka ambayo Khamenei alikuwa nayo.
Lakini Boussois anasema kuanguka kwa Jamhuri ya Kiislamu ni jambo lisilowezekana kabisa.
Iwapo itatokea na kuchochewa na uingiliaji wa kijeshi wa kigeni, kinachofuata kinaweza kuwa kibaya zaidi, anasema.
Awali, Trump aliliambia gazeti la New York Times kwamba hatua ya Marekani ya kumkamata Rais wa zamani wa Venezuela, Nicolás Maduro, ingekuwa "hatua mwafaka" kwa Iran.
Lakini Boussois anasema: "Kinyume chake kinaweza kutokea - kama huko Korea Kaskazini au Cuba - kuimarika kwa msingi mgumu."