Mpelelezi wa virusi ambaye aligundua Ebola mwaka 1976

Zaidi ya miaka 40 iliyopita, mwanasayansi mdogo wa Ubelgiji alisafiri hadi sehemu ya mbali ya msitu wa Kongo kazi yake ilikuwa kusaidia kujua ni kwa nini watu wengi wanafariki kutokana na ugonjwa usiojulikana na wa kutisha.

Mnamo Septemba 1976, kifurushi kilichokuwa na chupa inayong'aa na ya buluu ya thermos kilifika katika Taasisi ya Tiba ya Kitropiki huko Antwerp, Ubelgiji.

Aliyefanya kazi katika maabara siku hiyo alikuwa Peter Piot, mwanasayansi wa umri wa miaka 27 wakati huo na aliyehitimu mafunzo ya shule ya matibabu kama mwanabiolojia wa kliniki

"Ilikuwa chupa ya kawaida tu kama nyingine yoyote ambayo ungetumia kuweka kahawa ya moto," anakumbuka Piot, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Shule ya Madawa ya Tropiki Londoni.

Lakini thermos hii haikuwa imebeba kahawa, ndani kulikuwa na shehena tofauti kabisa. Iliwekwa vipande vichache vya barafu viliyokuwa vikiyeyuka kulikuwa na bakuli za damu pamoja na noti.

Ilikuwa ni kutoka kwa daktari wa Ubelgiji anayeishi katika nchini iliyokuwa Zaire, ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ujumbe wake ulioandikwa kwa mkono ulieleza kuwa damu hiyo ilikuwa ya mtawa, pia kutoka Ubelgiji, ambaye alikuwa ameugua ugonjwa wa ajabu ambao haukuweza kutambuliwa.

Mzigo huo usio wa kawaida ulikuwa umesafiri kutoka mji mkuu wa Zaire, Kinshasa, kwa ndege ya kibiashara, ukiwa katika moja ya mizigo ya mkononi ya abiria.

"Tulipofungua thermos, tuliona kwamba bakuli moja ilikuwa imevunjwa na damu ilikuwa ikichanganyika na maji kutoka kwenye barafu iliyoyeyuka," anasema Piot.

Yeye na wenzake hawakujua jinsi hiyo ilivyokuwa hatari. Damu ilipovuja ndani ya maji ya barafu ndivyo pia virusi hatari visivyojulikana vilisambaa.

Sampuli zilichukuliwa kama zingine nyingi ambazo maabara ilikuwa ikijaribiwa hapo awali, lakini wanasayansi walipoweka baadhi ya seli chini ya darubini ya elektroni waliona kitu ambacho hawakutarajia.

"Tuliona mdudu mkubwa mwenye muundo kama mnyoo- mkubwa kwa viwango vya virusi," anasema Piot. "Ni umbo lisilo la kawaida sana kwa virusi, ni virusi vya aina moja tu ambavyo vina muundo kama huo mbavyo ni virusi vya Marburg."

Virusi vya Marburg vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 1967 wakati watu 31 walipougua homa ya kuvuja damu katika miji ya Marburg na Frankfurt nchini Ujerumani na Belgrade, mji mkuu wa Yugoslavia.

Mlipuko huu wa Marburg ulihusishwa na wafanyikazi wa maabara ambao walikuwa wakifanya kazi na nyani walioambukizwa kutoka Uganda - watu saba walifariki.

Piot alijua jinsi Marburg inaweza kuwa mbaya lakini baada ya kushauriana na wataalam ulimwenguni kote alipata uthibitisho kwamba kile alichokuwa akiona kwenye darubini haikuwa Marburg - hii ilikuwa kitu kingine, kitu ambacho hakijawahi kuonekana.

"Ni vigumu kuelezea lakini hisia kubwa niliyokuwa nayo ilikuwa ya msisimko wa kweli na wa ajabu," anasema Piot. "Kulikuwa na hisia ya kuwa na bahati sana, kwamba huu ulikuwa wakati wa ugunduzi."

Habari zilikuwa zimefika Antwerp kwamba mtawa huyo, ambaye alikuwa chini ya uangalizi wa daktari huko Zaire, alikuwa amefariki.

Timu hiyo pia iligundua kuwa wengine wengi walikuwa wakiugua ugonjwa huu wa kushangaza katika eneo la mbali kaskazini mwa nchi - dalili zao ni pamoja na homa, kuhara na kutapika na kufuatiwa na kutokwa na damu na hatimaye kifo.

Wiki mbili baadaye Piot, ambaye hakuwahi kufika Afrika hapo awali, alikuwa kwenye ndege kuelekea Kinshasa.

"Ilikuwa ni safari ya ndege ya usiku kucha na sikuweza kulala. Nilifurahi sana kuona Afrika kwa mara ya kwanza, kuhusu kuchunguza virusi hivi vipya na kuhusu kukomesha janga hili."

Safari haikuishia Kinshasa timu ililazimika kusafiri hadi katikati ya mlipuko huo, kijiji katika msitu wa Ikweta, kama kilomita 1,000 (maili 620) zaidi kaskazini.

"Daktari binafsi wa Rais Mobutu, kiongozi wa Zaire wakati huo, alitutafutia ndege ya usafiri ya C-130," anakumbuka Piot. Walipakia Landrover, mafuta na vifaa vyote walivyohitaji kwenye ndege.

Wakati ndege ya C-130 ilipotua Bumba, bandari ya mto iliyoko sehemu ya kaskazini kabisa ya Mto Kongo, hofu iliyozunguka ugonjwa huo wa ajabu ilikuwa dhahiri. Hata marubani hawakutaka kuzunguka kwa muda mrefu - waliacha injini za ndege zikiendelea kufanyakazi wakati timu ikipakua vifaa vyao.

"Walipoondoka walipiga kelele 'Adieu," anasema Piot. "Kwa Kifaransa, watu husema 'Au Revoir' kusema 'Tuonane tena', lakini wanaposema 'Adieu' - hiyo ni kama kusema, 'Hatutakuona tena.'

Wakiwa wamesimama kwenye lami wakitazama ndege ikiondoka, ili kukabiliana na virusi hatari visivyojulikana mahali pasipojulikana, huenda baadhi ya watu walijutia uamuzi wa kwenda huko.

"Sikuwa na hofu. Msisimko wa ugunduzi na kutaka kukomesha janga hilo ulikuwa ukichochea kila kitu. Tulisikia watu wengi zaidi wanakufa kutokana na ugonjwa huo kuliko tulivyofikiria hapo awali na tulitaka kuanza kazi," Piot anasema.

Udadisi na hali ya kusisimua iliyomleta Piot kufikia hatua hii ilikuwa imeanza kwa miaka mingi nyuma alipokuwa mvulana mdogo akikulia katika kijiji kidogo cha mashambani katika eneo la Flanders la Ubelgiji.

Jumba la makumbusho karibu na nyumba ya Piot liliwekwa maalumu kwa ajili mtakatifu wa ndani ambaye alifanya kazi na wagonjwa wa ukoma, na ilikuwa hapa ndipo alipopata mwanga wake wa kwanza katika ulimwengu wa magonjwa na uchunguzi wa vijidudu (microbiolojia).

“Niliamua siku moja kwenda kwenye jumba la makumbusho kwa baiskeli. Picha za zamani nilizoziona za wale wanaougua ukoma zilinivutia,” anasema. "Hilo lilizua shauku yangu katika dawa - ilinipa kiu ya maarifa ya kisayansi, hamu ya kusaidia watu na nilitarajia ingenipa haki ya kusafiri duniani."

Ilimpa Piot pasipoti kwa ulimwengu. Kituo cha mwisho kwa timu ya Piot ilikuwa kijiji cha Yambuku - kama kilomita 120 (maili 75) kutoka Bumba, ambapo ndege ilikuwa imewaacha.

Yambuku ilikuwa nyumbani kwa misheni ya Kikatoliki ya zamani - ilikuwa na hospitali na shule inayoendeshwa na makasisi na watawa, wote kutoka Ubelgiji.

"Eneo hilo lilikuwa zuri. Misheni ilikuwa imezungukwa na msitu mnene na ardhi ilikuwa nyekundu - kuna utajiri wa asili lakini watu walikuwa maskini sana," anasema Piot. "Joseph Conrad aliita mahali hapo 'Moyo wa Giza', lakini nilifikiri kulikuwa na mwanga mwingi huko."

Uzuri wa Yambuku ulipingana na tishio lililokuwa likiendelea kwa watu waliokuwa wakiishi hapo.

Piot alipofika, watu wa kwanza alikutana nao walikuwa kikundi cha watawa na makasisi ambao walikuwa wamekimbilia kwenye nyumba ya wageni na kuanzisha cordon sanitaire - kizuizi kinachotumiwa kuzuia kuenea kwa magonjwa kama karantini

Kulikuwa na alama kwenye kordo, iliyoandikwa kwa lugha ya Kilingala iliyosomeka, "Tafadhali simameni, mtu yeyote anayevuka hapa anaweza kufa."

"Tayari walikuwa wamepoteza wenzao wanne kutokana na ugonjwa huo," anasema Piot. "Walikuwa wakiomba na kusubiri kifo."

Piot aliruka juu ya kordo na kuwaambia kwamba timu ingewasaidia na kukomesha janga hilo. "Unapokuwa na umri wa miaka 27, unakuwa na ujasiri huu wote," anasema.

Watawa waliwaeleza wanasayansi wapya kilichotokea, walizungumza kuhusu wenzao na wale wa kijijini waliopoteza maisha na jinsi walivyojitahidi kusaidia kadri walivyoweza.

Kipaumbele kilikuwa kukomesha janga hili, lakini kwanza timu ilihitaji kujua jinsi virusi hivi vilikuwa vikihama kutoka kwa mtu hadi mtu kwa hewa, kwa chakula, kwa kugusa moja kwa moja au kuenezwa na wadudu. "Ilitubidi kuanza kuuliza maswali. Ilikuwa kama simulizi ya upelelezi," anasema Piot.

  • Haya ndiyo maswali matatu waliyouliza: Je, gonjwa hilo liliibukaje? Kujua wakati kila mtu alipata virusi alitoa dalili za aina gani ya maambukizi haya - kuanzia hapo hadithi ya virusi ilianza kuibuka.
  • Watu walioambukizwa walitoka wapi? Timu ilitembelea vijiji vyote vinavyozunguka na kuainisha idadi ya maambukizi - ilikuwa wazi kuwa mlipuko huo ulihusiana kwa karibu na maeneo yanayohudumiwa na hospitali ya eneo hilo.
  • Nani huambukizwa? Timu iligundua kuwa wanawake wengi zaidi kuliko wanaume waliugua ugonjwa huo na haswa wanawake kati ya miaka 18 na 30 - ilibainika kuwa wanawake wengi wa rika hili walikuwa wajawazito na wengi walikuwa wamehudhuria kliniki ya wajawazito hospitalini.

Siri ya virusi hivyo ilianza kufichuka.

Timu ndipo ikagundua kuwa wanawake waliohudhuria kliniki ya wajawazito wote walichomwa sindano ya kawaida. Kila asubuhi, sindano tano tu zilisambazwa, sindano zilitumiwa tena na hivyo virusi vilienezwa kati ya wagonjwa.

"Hivyo ndivyo tulivyoanza kubaini," anakumbuka Piot. "Unafanya kwa kuzungumza, kuangalia takwimu na kupata hitimisho."

Timu hiyo pia iligundua kuwa watu walikuwa wakiugua baada ya kuhudhuria mazishi. Mtu anapofariki kutokana na Ebola, mwili wake hujaa virusi - mguso wowote wa moja kwa moja, kama vile kuosha au kuandaa mwili wa marehemu bila ulinzi kunaweza kuwa hatari kubwa.

Hatua iliyofuata ilikuwa kukomesha maambukizi ya virusi.

"Tulienda kwa utaratibu kutoka kijiji hadi kijiji na ikiwa mtu alikuwa mgonjwa aliwekwa kwenye karantini," anasema Piot.

"Pia tuliweka karantini mtu yeyote anayewasiliana moja kwa moja na wale walioambukizwa na tulihakikisha kila mtu anajua jinsi ya kuwazika wale waliopoteza maisha kutokana na virusi."

Kufungwa kwa hospitali hiyo, matumizi ya karantini na kuhakikisha jamii ina habari zote muhimu hatimaye ilimaliza janga hilo lakini karibu watu 300 walifariki.

Piot na wenzake walikuwa wamejifunza mengi kuhusu virusi wakati wa miezi mitatu huko Yambuku, lakini bado havikuwa na jina.

"Hatukutaka kukipa jina la kijiji, Yambuku, kwa sababu inanyanyapaa sana. Hutaki kuhusishwa na hilo," anasema Piot.

Timu hiyo iliamua kukiita virusi hivyo jina la mto. Walikuwa na ramani ya Zaire, ingawa haikuwa na maelezo ya kina sana, na mto wa karibu ambao wangeweza kuona ulikuwa Mto Ebola. Kuanzia wakati huo na kuendelea, virusi vilivyofika kwenye chupa huko Antwerp miezi yote iliyopita vilijulikana kama virusi vya Ebola.

Mnamo Februari 2014, Piot alirejea Yambuku kwa mara ya pili tu tangu 1976, kuadhimisha miaka 65 ya kuzaliwa kwake. Alikutana na Sukato Mandzomba, mmoja wa wachache waliopata virusi hivyo mwaka 1976 na kunusurika. "Ilikuwa nzuri kukutana naye tena, ilikuwa wakati wa kusisimua sana," anasema Piot.

Hapo zamani, Mandzomba alikuwa muuguzi katika hospitali ya eneo hilo na aliweza kuzungumza Kifaransa kwa hivyo wawili hao walifanikiwa kujenga urafiki.

"Bado anaishi Yambuku na bado anafanya kazi hospitalini - sasa anaendesha maabara huko na haina dosari. Nilifurahishwa sana," Piot anasema.

Ebola ilibadilisha maisha ya Piot - kufuatia kugunduliwa kwa virusi hivyo, aliendelea na utafiti wa janga la Ukimwi barani Afrika na kuwa mkurugenzi mkuu mwanzilishi wa shirika la UNAIDS. "Iliniongoza kufanya mambo ambayo nilifikiri yalifanyika tu kwenye vitabu. Ilinipa dhamira maishani kufanya kazi ya afya katika nchi zinazoendelea," anasema. "Haikuwa tu ugunduzi wa virusi lakini pia mimi mwenyewe."