Ipi nafasi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutatua mvutano wa Congo na Rwanda?

    • Author, Rashidi Abdallah
    • Nafasi, Mchambuzi

Kuna mivutano yenye pande mbili, ya pande tatu na ile yenye pande zaidi ya hizo. Mvutano wa nchi ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), una pande tatu: DRC yenyewe, jirani Rwanda na waasi wa M23.

Hakuna vita kati ya Rwanda na DRC, ila kuna vita kati ya waasi hao na DRC, na Rwanda anaingia kama mtuhumiwa anayefadhili shughuli za M23. Na hicho ndicho kiini cha uhasama wa nchi hizo kwa wanachama hao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

DRC haijawahi kupumzika kupambana na makundi ya waasi. Tangu kuingia madarakani Rais Félix Tshisekedi, Januari 2019, ameahidi mara kadhaa atatokomeza uasi Mashariki mwa nchi hiyo. Mafanikio ni madogo, waasi wakiwemo wa M23 wana nguvu za kushambulia raia na wanajeshi.

DRC siyo pekee inayoituhumu Rwanda

Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ya 2012, ilieleza kuna ushahidi Rwanda inaunga mkono kundi la M23. Kundi linaloundwa na idadi kubwa ya wapiganaji kutoka kabila la Watutsi.

Ripoti nyingine ya Juni 2013 ya Umoja wa Mataifa ilieleza, M23 inasajili wapiganaji nchini Rwanda kwa usaidizi wa Jeshi la nchi hiyo. Ripoti hizo zilipelekea Marekani na Umoja wa Ulaya kusitisha misaada ya kijeshi kwa Rwanda.

Julai 2013, Marekani iliitaka Rwanda kuacha kuunga mkono waasi wa M23. Ikieleza kuna ushahidi wa kutosha wa maafisa wa kijeshi wa Rwanda kuhusika kusaidia kundi hilo. Mzozo wa sasa umeiibua tena Marekani na kurudia kauli yake ya kuituhumu Kigali kuunga mkono M23.

Kila Rwanda inapotuhumiwa hukanusha. Hujibu kwa kusema DRC imeshindwa kutatua matatizo yake na waasi na inaitumia Rwanda kama kisingizio. Na badala yake huituhumu DRC kuunga mkono waasi wa FDLR, wapiganaji waliohusika na mauaji ya kimbari 1994.

Zipi athari za mvutano wa sasa?

Kufukuzwa kwa Balozi Vincent Karega wa Rwanda nchini DRC, ni dalili ya kuzidi kuharibika kwa uhusiano. Hatua hiyo ilikuja baada ya kundi la M23 kuteka miji miwili Mashariki mwa DRC.

Mvutano huu unazalisha jambo jingine baya zaidi; hatari inayowakumba watu wanaozungumza Kinyarwanda Mashariki mwa DRC. Kila mvutano wa nchi hizo unaposhika kasi na usalama wa jamii hiyo unazidi kuwa mashakani.

Kwa upande wa Rwanda, Naibu msemaji wa serikali, Alain Mukurarinda alitoa wito kwa raia kutosafiri DRC kwa sababu za kiusalama. Pia, nchi hiyo ikapeleka wanajeshi karibu na mpaka wake na DRC.

Mbali na DRC na Rwanda, mvutano huu hauwezi kuwa jambo la afya kwa ustawi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika shughuli za kiuchumi na kibiashara. Fauka ya yote, una athari katika harakati zinazoendelea za jumuiya kutafuta amani ya DRC.

Kumaliza vita kutaondoa mvutano?

Mvutano wa DRC na Rwanda ni matokeo ya vita vya Mashariki mwa DRC. Kujadili muafaka kati ya mataifa hayo mawili utapatikanaje, ni muhimu kwaza kujadili kile kinacholeta mvutano kinaweza kuisha kwa njia gani.

Vita vingi duniani huisha kwa namna moja kati ya tatu: Mosi, mazungumzo ya kisiasa, yanayowaleta katika meza moja wahusika na kutiliana saini makubaliano ya kusitisha mapigano, baada ya kutoka pande zote mbili kukubalika.

Moja ya vita ambavyo vimemaliza kwa mazungumzo ya kisiasa katika miaka ya hivi karibuni, ni kati ya Colombia na waasi wa FARC. Mgogoro wa miongo mitano, ulifikia tamati mwaka 2016, baada ya kusainiwa mkataba wa amani kati ya kundi hilo na serikali ya Colombia.

Pili, ni matumizi ya nguvu ambayo hupelekea upande mmoja kushindwa. Njia hii huzalisha vifo vingi kwa wahusika na raia. Mathalan; vita vya wenyewe kwa wenye nchini Rwanda vilivyoanza 1990, kwa misingi ya ukabila, viliondoka na maisha ya watu wengi.

Vita hivyo vilifikia tamati baada ya Serikali na Jeshi la Rwanda na Wahutu wa misimamo mikali, kushindwa na waasi wa Rwandan Patriotic Front (RPF), walioongozwa na Paul Kagame, Rais wa sasa wa taifa hilo.

Tatu, (frozen conflict); pale wahusika wanapoacha au kuchoka wenyewe kupigana na kuufanya mgogoro kufifia. Kama vita vya Georgia juu ya eneo la Ossetia Kusini, linalopigania kujitenga na Georgia na kuungwa mkono na Urusi.

Tangu mapigano ya 2008 hakuja shuhudiwa tena mapigano katika eneo hilo licha ya kuwa hakuna mkataba wa amani uliofikiwa wala upande uliosalimu amri. Hali ikibaki hivyo, mgogoro huisha polepole kwa mazingira kama hayo.

Mbinu ipi itumike kumaliza vita?

Wakati swali kuu ni namna gani Jumuiya ya Afrika Mashariki inaweza kuwapatanisha wanachama wenzao. Kuna maswali mawili makubwa ambayo ndio msingi wa namna gani upatanishi huo unaweza kufanyika.

Moja, kuna uwezekano wa DRC na Rwanda kupatana wakati M23 bado ina nguvu na uwezo wa kushambulia raia wa DRC? Pili, ama mvutano wao hauwezi kutatuka hadi M23 iwe imetoweka moja kwa moja?

Historia inaonesha, kuipatanisha DRC na Rwanda wakati M23 ikiendelea kuwa hai na kufanya mashambulizi ni jambo gumu. Ni ndoa ambayo haidumu kwa muda mrefu, kabla mambo kutibuka tena.

Ndani ya mwaka huu pekee; majaribio kadhaa ya kuipatanisha DRC na Rwanda yamefanyika. Mwezi Mei kulifanyika mazungumzo kwa njia ya simu kati ya Rais Kagame na Rais Tshisekedi yaliyosimamiwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Macky Sall.

Mwezi Julai, Kagame na Tshisekedi walikutana kwa mazungumzo ya upatanishi yaliyosimamiwa na Rais wa Angola, Joao Laurenco. Agenda kuu ni kuleta maelewano kati ya mataifa hayo juu ya sintofahamu zao.

Mwezi Juni, wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walikutana Nairobi, Kenya. Moja ya ajenda ni kuujadili uasi wa DRC. Kufeli kwa majaribio hayo kunatoa tafsiri ya kuwa, uwezekano wa nchi hizo kuwa majirani wema wakati M23 imeshika silaha, ni mdogo.

Kwa kuzingatia hayo, njia iliyobaki ya kuumaliza mvutano wa nchi hizo mbili ni kuumaliza uasi wa M23 ndani ya DRC, pengine na uasi wa makundi mengine. Hili linatokana na lile swali la pili.

Endapo Jumuiya ya Afrika Mashariki itafanikiwa kulitokomeza kundi la M23, ima kwa kutumia mazungumzo ya kisiasa na likakubali kuweka silaha chini au kulikongoa kwa kutumia nguvu za kijeshi. Kutakuwa na matumaini makubwa ya kurudi kwa uhusiano wa Rwanda na DRC.

Nafasi ya Jumuiya hiyo kuleta mtangamano, sio kuandaa vikao vya mara kwa mara kuwazungumzisha Kagame na Tshisekedi, bali ni kumaliza vita kwa kuukata mzizi wa fitina - M23. Na wala sio kwa kusubiri wachoke wenyewe, bali ni kwa njia ya kisiasa ama nguvu za kijeshi.